Tiwa Savage alivyoteswa na ndoa miaka mitano

Muktasari:

Miongoni mwa vitu anavyomshukuru Teebills ni kumbadilisha kutoka kuwa tomboy


Hivi karibuni mwanamuziki supastaa wa Nigeria, Tiwa Savage ametoboa kuwa ndoa yake na Tunji Balogun a.k.a Teebillz, inaelekea ukingoni kwani yuko katika hatua za kukamilisha talaka.

Pamoja na kuwa anaachana na mwanamume huyo, anasema siku zote atamshukuru kwa kumfikisha alipo katika muziki kwani ndiye aliyembeba akiwa ‘underground’ na kumfanya mmoja kati ya mastaa wakubwa Afrika.

Anasema alipokutana na Teebills kwa mara ya kwanza alimshangaa kutokana na tabia zake kwa kuwa alionekana kuwa mwanamume anayejiamini kupita kiasi jambo ambalo lilimfanya asivutiwe naye kimapenzi.

“Huwezi kuamini aliniambia inabidi uchague moja kati ya mawili, ‘nikuoe au niwe msimamizi wa kazi zako’. Nikamwambia wewe vipi, yaani sio kunioa tu hata kuwa wapenzi sitaki kwa sababu huna sifa zozote za kiume,” anasema Tiwa.

Anasema baada ya kuanza kufanya naye kazi aliona upande mwingine wa Teebills ambao ulimfanya ampende ingawa alijitahidi kujizuia lakini alijikuta akiwa hoi na kukubali kuolewa naye.

Miongoni mwa vitu anavyomshukuru Teebills ni kumbadilisha kutoka kuwa tomboy (mwanamke anayevaa kama mwanamume) na kuwa mmoja wa wanawake wa kupigiwa mfano linapokuja suala la mavazi.

Chini ya usimamizi wa mumewe na lebo ya Marvin inayomilikiwa na Don Jazzy, mwaka 2013 aliachia albamu yake ya kwanza Once Upon a Time ikiwa na nyimbo kwamba “Kele Kele Love’’, “Love Me (3x)”, “Without My Heart”, “Ife Wa Gbona”, “Folarin”, “Olorun Mi” na “Eminado’’.

Ndoa yake iligundulika kuwa na mushkeli baada ya mumewe Teebillz kutaka kujirusha kutoka darajani kwa lengo la kujiua kwa madai kuwa mkewe amekuwa akichepuka.

Baada ya kuokolewa na Tiwa Savage kupewa nafasi ya kujitetea alifufua uovu wa mwanamume huyo akiusindikiza na ujumbe mfupi wa maandishi (sms) alioubamba katika simu ya mumewe akiwasiliana na wanawake zaidi ya wawili.

Baada ya vita ya maneno kwa muda wa takribani mwezi mmoja, Teebillz alikiri makosa ikiwamo la kutumia fedha vibaya na ulevi uliopitiliza, hata hivyo, inaonekana wameshindwa kufikia muafaka na Tiwa Savage ameamua safari yao pamoja ifikie tamati.