Tughe wapongeza likizo ya uzazi kina mama wanaojifungua njiti

Muktasari:

  • Wiki iliyopita katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei mosi), Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alisema likizo ya wanaojifungua watoto njiti, Serikali inaipa muhimu mkubwa

Dar es Salaam. Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (Tughe), kimesema hatua ya Serikali kuongeza muda wa likizo kwa waliojifungua watoto njiti itawezesha wanawake kupata muda wa kutosha wa kuhudumia watoto hao.

 Wiki iliyopita katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei mosi), Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alisema likizo ya wanaojifungua watoto njiti, Serikali inaipa muhimu mkubwa.

“Likizo ya uzazi ni miongoni mwa haki za wafanyakazi na hutolewa kwa muda wa siku 84 endapo mfanyakazi atajifungua mtoto mmoja au siku 100 endapo atajifungua mtoto zaidi ya mmoja,” alisema.

Kutokana na hilo, Dk Mpango alisema mfanyakazi husika ataruhusiwa kutoka kazini saa saba mchana kila siku kwa muda wa miezi sita baada ya kumalizika kwa likizo ya uzazi ili kumpa ruhusa ya kwenda kunyonyesha.

Leo Jumanne Mei 7, 2024 Makamu Mwenyekiti wa Tughe, Jenny Madete akifanya ziara katika wodi ya watoto ya Hospitali ya Rufaa ya Temeke, jijini Dar es Salaam, ameishukuru Serikali kwa kuongeza muda kwa waliojifungua.

“Wafanyakazi wa kike wanapitia changamoto mbalimbali ikiwamo ya afya, hivyo wanahitaji muda mwingi wa kupumzika ili kumhudumia mtoto hadi wanaporuhusiwa kutoka hospitali.

“Kupitia muda huu wa nyongeza itasaidia wanawake kupata muda wa kutosha kuhudumia mtoto au watoto pasipo wasiwasi wa kupoteza ajira yake,” amesema Madete.

Madete amebainisha kwa watalamu wa afya, mtoto anapozaliwa anahitaji zaidi ya mwezi ili kuimarika kwa afya yake.

Daktari wa zamu wa Hospitali ya Temeke, Joseph Kimaro ameungana na Madete kuishukuru Serikali kwa kuongeza muda huo kwa wanawake wanaojifungua watoto njiti, akisema itawapa muda wa kumpumzika wazazi hao.

Mbali na hilo, Dk Kimaro amesema hosptilali hiyo, wamejipanga kutoa elimu bora kwa wanaojifungua watoto njiti sambamba na kuwa na mashine zaidi ya 20 zitakazowasaidia watoto kupumua vizuri baada ya kuzaliwa.

“Tumeandaa marathoni kwa ajili ya kuchangisha fedha zitakazowezesha ununuzi wa vifaa vya kuwasaidia watoto njiti,” amesema Dk Kimaro.