Ubovu wa barabara Dar unavyowaliza wananchi

Kazi ya ujenzi wa mitaro ya maji ikienmdelea katika eneo la Kinzudi, Kata ya Goba mkoani Dar es Salaam, ambapo wakati wa Mtaa wa Kinzudi wanachangisha Sh180 milioni kwa ajili ya ujenzi huo ili kukabiliana na adha wanayopitia msimu wa mvua. Picha na Tuzo Mapunda

Muktasari:

  • Miundombinu ya barabara jijini Dar es Salaam imegeuka kero kwa wananchi kutokana na kuharibika kwa barabara nyingi huku Serikali ikiahidi kujenga kilomita 250.

Dar es Salaam. Idadi ya watu na makazi ikiendelea kuongezeka, ubovu wa barabara jijini Dar es Salaam umekuwa kero kwa wananchi na zaidi kwa wanaoanzisha makazi mapya.

Matokeo ya Mwanzo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 yanaonyesha Mkoa wa Dar es Salaam una zaidi ya wakazi milioni 5.38.

Ongezeko la idadi ya watu limesababisha kuanzishwa makazi mapya ambayo pia huongeza barabara zinazohitaji kuhudumiwa na mamlaka husika.

Kwa mujibu wa taarifa ya hali za barabara kwa halmashauri hadi Juni 2022, iliyotolewa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), Mkoa wa Dar es Salaam una jumla ya kilomita 5,090.78 za barabara.

Kati ya hizo, kilomita 2,965.83 ni za vumbi ambazo kati yake zenye hali nzuri ni kilomita 82.4 pekee.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, Mkoa wa Dar es Salaam una kilomita 514.43 za barabara za lami na zilizotengenezwa kwa changarawe ni kilomita 1,610.53.

Kwa upande wa barabara zilizo chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mkoa wa Dar es Salaam una jumla ya barabara za mkoa zenye urefu wa kilomita 401 na kati ya hizo, kilomita 159 hazijajengwa. Pia mkoa una jumla ya kilomita 599 za barabara kuu.


Kilio cha wananchi

Takwimu hizo zinazoonyesha uwepo wa barabara nyingi ambazo hazijajengwa, zinaendana na kilio halisi cha wananchi wa maeneo mbalimbali, Mbezi-Mpiji-Magohe iliyo chini ya Tanroads yenye urefu wa kilomita 9.5 ikiunganisha barabara za Morogoro na Bagamoyo.

Barabara nyingine zinazolalamikiwa muda mrefu, ni Tabata Majichumvi-Chang’ombe-Barakuda hadi Vingunguti, Banana-Kivule hadi Msongola, Kitunda-Kibeberu-Magole; Kitunda Mwanagati-Kwa Mpalange na Pugu-Majohe-Viwege na nyingine nyingi.

Wakizungumza na Mwananchi Digital hivi karibuni, baadhi ya wananchi wa Mpiji wamesema ni kama vile barabara hiyo imesahaulika.

Mmoja wa wakazi hao, Mbaraka Tika, amesema nyakati za mvua barabara hiyo inapitika kwa shida. 

“Mvua zikinyesha mashimo yote yanajaa maji kila sehemu haipitiki, usiku hali inakuwa ngumu zaidi magari yanaharibika kwa kujigonga-gonga kwenye mashimo. Ukimaliza safari salama bila gari kupata hitilafu unamuomba Mungu,” amesema.

Amesema safari za kwenda Mpiji inatumia muda mrefu hadi kufika kwa kuwa kila mmoja anahofia kutembea mwendo wa haraka kutokana na mashimo mengi yanayohatarisha usalama wa vyombo vyao.

Mkazi wa Msakuzi, Sabrina Joseph amesema asubuhi na jioni huwepo msongamano na zaidi mvua zinaponyesha daladala hazifanyi safari maeneo hayo.

Kwa chache zinazofanya safari kwa wakati huo, amesema hutoza nauli kati ya Sh2,500 hadi Sh3,000.

Amesema iwapo barabara hiyo itatengenezwa, nauli haiwezi kuzidi Sh1,000.

“Kwa tunaotegemea kutafuta riziki zetu katikati ya mji tunakuwa na wakati mgumu zaidi kwenda utumie Sh3,000 na kurudi kiwango hicho unaona kabisa maisha yetu yanakuwa magumu kwa kuwa fedha yote inashia kwenye nauli,” amesema.

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa Mpiji Magohe, Orest Mubofu amesema kilio cha matengenezo ya barabara hiyo inayoenda stendi kuu ya ya mkoa (Magufuli) ni kikubwa kwani nauli hupanda wakati wa mvua.

“Usafiri unakuwa wa shida, magari ni machache, wananchi ni wengi na wakati mwingine watu wanapaki gari zao njiani kutembea kwa miguu kurudi nyumbani, hivyo usalama unakuwa mdogo,” amesema.

Amesema kutokana na ubovu wa barabara daladala hazifiki maeneo mengine, akieleza Magohe ni kituo kikubwa kilichopo, na kwamba Kwa Kengega ni mbali kwa kuwa walio wengi wanaishi Kibesa.

“Tunaomba daladala zifike Kibesa kuna wananchi zaidi ya 5,000 wanapanda pikipiki hadi Kwa Kengega ili wapate daladala kwenda mjini. Tujengewe lami kuondoa adha hizi,” amesema.

Mbunge wa Kibamba, Issa Mtemvu amesema lazima wananchi wakubali maendeleo ni mchakato na wanapaswa kuelewa Serikali ina mpango mzuri wa kuweka lami.

“Serikalini ili barabara ijengwe lazima mipango ifanyike ikiwemo usanifu wa kina kabla ya kuja kwenye bajeti, na katika bajeti ya mwaka jana ilikuwepo na wataiombea tena bajeti ijayo,” amesema.

Mtemvu amesema barabara hiyo inaitwa Victoria au Mpiji Shule na ikikamilika itaenda kutokea Bunju, ikiwa chini ya mkoa, hivyo ana imani kwa mwaka wa fedha 2024/25 itakuwa imefanyiwa upembuzi.

“Barabara hii itakuwa kipaumbele changu iingiziwe fedha, ijengwe na changamoto kwa wananchi wangu iishe, pamoja na barabara ya Makabe iliyoanza kujengwa,” amesema.

Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi John Mkumbo, akizungumza na Mwananchi Digital wiki hii, amesema wana taarifa kuhusu changamoto ya barabara hiyo, hivyo wapo kwenye mpango wa kuifanyia kazi.

“Changamoto yao tumeshaipata kwa sasa tunahangaikia mipango, lakini tunalifahamu,” amesema.


Kilio kama cha Mpiji Magohe kipo pia katika Wilaya ya Ilala, ambako mkazi wa Kivule, Mwita Samwel amesema kwao hali ni mbaya wakati wote na inakuwa mbaya zaidi katika kipindi kama hiki cha mvua.

“Tumeambia kuna mradi wa DMDP, lakini hatuamini maana ndivyo wanavyotwambia miaka yote. Huwezi kuamini kwamba huku ni sehemu ya Jiji la Dar es Salaam. Daladala zinapakimbia na chache zinazokuja zinajipangia bei,” amesema Samwel akiongeza kuwa “Ukitaka kuona balaa nenda Banana jioni uone shida wanayopata wakazi wa Kivule na Msongola.”


Balaa, mateso

Amina Mwintanga, mkazi wa Viwege amesema “mvua ni neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ila sisi watu tunaoishi huku Viwege imekuwa ni balaa, mateso na adhabu tunayopata pindi mvua zinaponyesha kwa sababu barabara inayoka Pugu – Majohe –Viwege inaharibika na kusababisha shida kubwa ya usafiri.”

Amina amesema anakumbuka kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, alimsikia mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli akitoa ahadi ya barabara hiyo kujengwa kwa kiwango cha lami lakini hadi sasa hakuna kitu kinachoendelea, jambo linalowakatisha tamaa kutokana na mateso wanayoendelea kuyapata.


Mchepuko waingiliwa

Kutokana na hali iliyopo, hara barabara zinazotumika kama mbadala (za mchepuko) wakati wa msongamano wa magari, nyingi zikiwa za udongo na changarawe, wakati wa mvua za elnino mwishoni mwa 2023 na sasa masika zimeathiriwa kwa kiasi kikubwa.

Taarifa ya Tarura ya Agosti, 2023 ilieleza mvua iliharibu maeneo 83 katika wilaya zote na kwa kiasi kikubwa bado hali haijarejeshwa kuwa kawaida kwa kuwa ukarabati bado haujafanyika.


Wakarabati barabara

Kutokana na kuchoshwa na hali hiyo, baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Kinzudi, Kata ya Goba, wilayani Ubungo wameanza kuchangishana fedha ili kupata Sh180 milioni ili kuboresha barabara na kuchimba mitaro kukabiliana na adha wanayopitia wakati wa msimu wa mvua.

Wananchi hao wameanza kuchimba mitaro baada ya kuwa wamepata Sh22 milioni, wakisema kwa zaidi ya miaka 10 wameiomba Serikali kuboresha barabara bila mafanikio.

Hata hivyo, Meneja wa Tarura, Mkoa wa Dar es Salaam, Geoffrey Mkinga alipoulizwa kuhusu ujenzi huo, amesema anafahamu suala hilo na wametenga bajeti kuongezea nguvu ya wananchi.

“Serikali kupitia Tarura tumetenga kwenye bajeti Sh239 milioni kwa ajili ya kwenda kuunga mkono juhudi zao kwa kuitengeneza barabara hiyo kwa kilomita zote mbili,” amesema.

Mkazi wa eneo hilo, Edson Misana aliyechaguliwa na wakazi hao Machi 19, 2024 ili kuwawakilisha, amesema:

“Sisi wananchi wa eneo hili tunaitumia njia hii kwenda kwenye shughuli zetu na kurudi katika makazi yetu, hatuna njia nyingine mbadala. Kipindi hiki cha mvua gari likikwama unaliacha njiani, unaenda nyumbani kwa miguu maana hata pikipiki haipiti,” amesema.

Katika mtaa huo kuna bango lenye kichwa cha habari, ‘Wakazi wa Barabara ya Awadh-KKKT Kinzudi (KM2)’ lililojengwa mita 100 kutoka usawa wa barabara hiyo, ili kutoa taarifa na kuhamasisha wakazi wa eneo hilo kuchangia ujenzi.

“Baada ya kuweka bango matokeo yamekuwa mazuri, tumepata Sh3 milioni ina maana mwamko umekuwa mkubwa kila mmoja anajua anatakiwa kuchangia kufanikisha ujenzi,” amesema.

Mwenyekiti wa usimamizi wa ujenzi huo, Joseph Mboya amesema:

“Tuliona kusubiria bajeti ya Serikali tunaweza kuchelewa kufanya mambo yetu mengine na kuna wakati tunawabeba watoto hadi barabarani wakapande magari waende shule.”


Ahadi ya Mchengerwa

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu wiki hii jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa, alisema kwa kuangalia kero ya barabara Dar es Salaam, Tarura inatarajia kujenga kilomita 250.

“Hivi karibuni tumesaini mikataba ya kuhakikisha eneo la mjini Dar es Salaam tunajenga kilomita zaidi ya 250 na kazi hizi tutazitangaza mwezi huu (Machi) na tukichelewa wa nne (Aprili) mwanzoni kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami,” alisema.

“Maana yake ni kwamba, hakuna jimbo la uchaguzi, hakuna halmashauri ya wilaya itakayokosekana katika mpango wa ujenzi wa barabara zaidi ya kilomita 250,” alisema.