Uchunguzi wabaini mmoja kati ya watu saba ana tatizo la macho

Mkurugenzi wa Huduma ya Afya Saidizi katika Hospitali ya Rufaa Kanda Bugando, Dk Cosmas Mbulwa akizungumza katika hafla ya wafanyakazi wanawake iliyofanyika hospitalini hapo. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

  • Hospitali ya Rufaa Kanda ya Buganda (BMC) jijini Mwanza imeendesha kliniki ya macho na kubaini watu zaidi 100 wakiwa na shida ya macho kati ya watu zaidi ya 700 waliofikiwa.

Mwanza. Uchunguzi uliofanywa kwa siku tatu na jopo la madaktari wanawake katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Buganda (BMC) jijini Mwanza, umebaini watu zaidi 100 wakiwa na matatizo mbalimbali ya macho kati ya watu zaidi ya 700 waliofikiwa.

Takwimu hizo zimetolewa jana Alhamisi, Machi 7, 2024 na Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Fabian Massaga kwenye hafla ya siku ya wanawake wafanyakazi hospitalini hapo, akisema sababu kubwa ni jamii kutojenga utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya zao ikiwa ni pamoja na macho.

Dk Massaga amesema ili macho yaendelee kuwa na afya lazima jamii ijenge tabia ya kuyafanyia uchunguzi mara kwa mara ili kubaini changamoto zikiwa katika hatua za mwanzo.

"Uchunguzi uliofanyika jijini Mwanza ambapo takribani wananchi zaidi ya 700 wamenufaika na huduma hiyo huku idadi kubwa ya wagonjwa wakiwa na tatizo la macho na presha.

“Hali hii imechochewa na kasumba iliyojengeka miongoni mwa jamii ya kutofanya uchunguzi wa afya zetu mara kwa mara na kusubiri tatizo likiwa limeshajitokeza,” amesema.

Amesema tatizo likishakuwa kubwa linasababisha ongezeko la gharama za matibabu na muda mwingine kushindwa kutibika.

Muuguzi katika hospitali hiyo, Marium Monsuri amesema uchunguzi huo umewashtua, hivyo wanaomba uchunguzi zaidi kufanyika ili kubaini chanzo cha ugonjwa huo.

"Nilishtuka kidogo kuona idadi kubwa wana shida ya macho kwa hiyo inatakiwa kuanza kufanya uchunguzi mapema kwa sababu inawezekana tatizo linaanza kidogo kidogo lakini kwa vile hatufuatilii, basi tunajikuta tatizo linakuwa sugu kwa sababu tunakuwa tumechelewa sana," amesema Marium

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa magonjwa ya wanawake katika Hospitali ya Rufaa Kanda Bugando, Amina Yusuph amesema mbali na tatizo hilo pia kina mama wengi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa hubainika wakiwa na saratani ya matiti, mlango wa kizazi na pia kuna tatizo la saratani ya tezi dume kwa watu wote, bila kujali jinsia.

"Huwa tunatumia fursa kama hiyo kuwafundisha wanawake ili wazijue afya zao hasa hasa kwa magonjwa hayo ambayo yanahatarisha afya zao.

‘Kitu kinachotusumbua huku Kanda ya Ziwa na sehemu zingine za nchi zinazoendelea ni saratani ya mlango wa kizazi, hili ni tatizo kubwa sana," amesema.

"Wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani wanawake wanatakiwa kuchunguzwa mara kwa mara, kwa yule ambaye amewahi kujamiiana na ana miaka kuanzia 25 mpaka 50 achunguzwe kila baada ya miaka mitatu katika kituo kinachofanya uchunguzi na huwa ni bure," amesema Dk Amina.

Mbali na uchunguzi wa macho hospitali hiyo imeendesha uchunguzi wa saratani ya matiti, magonjwa ya pua na koo, tezi dume na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukizwa.