Ukame wakosesha maji wananchi Monduli

Muktasari:

Kufuatia ukame wa ulioukumba Mkoa wa Arusha, baadhi ya wananchi wameiomba Serikali kuwapatia maji safi na salama.

Arusha. Vijiji vinane katika Kata ya Lepurko, Wilaya ya Monduli mkoani Arusha vinakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji uliotokana na ukame hali ambayo inasababisha kunywa maji machafu.

Wilaya hiyo na Wilaya za Longido na Ngorongoro zimeathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi na zaidi ya mifugo na wanyamapori 40,000 wamekufa kwa kukosa maji na malisho.

Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Frank Mwaisumbe akizungumza na Mwananchi leo Oktoba 20, 2022 amesema baada ya kusambaa video inayoonesha watoto wakichota maji machafu amekwenda kutembelea eneo hilo.

"Hili ni tukio la ukweli Kata ya Lepurko na vijiji vinane wana hali mgumu kutokana na ukame. Hivyo nimeagiza halmashauri kuwapelekea maji kwa kutumia maboza kwani katika vijiji hivyo maji ya kuchimba hayapatikani," amesema.

Hata hivyo, amesema hatua nyingine ni kupeleka mradi wa maji katika maeneo hayo jambo ambalo linaweza kuchukua muda zaidi kwani vijiji hivyo hakuna huduma ya umeme.

Julius Mollel mkazi wa Lepurko aliomba Serikali kuwaokoa ili wapate maji kwani miaka mitatu sasa hawana mvua za kutosha.

"Tunaomba kupatiwa maji ya kunywa sisi na mifugo yetu kwani visima vyote vimekauka," amesema.