Upelelezi wakwamisha kesi vigogo TPA

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande (wa pili kutoka kushoto) akiwa na wenzake wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi. Picha na maktaba

Muktasari:

  • Wakili wa Serikali, Monica Ndekidemi ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Aprili 29, 2024, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Dar es Salaam. Upelelezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Madeni Kipande (66) na wenzake watano, bado unaendelea.
Wakili wa Serikali, Monica Ndekidemi ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Aprili 29, 2024, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Kipande na wenzake wakikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya Dola za Marekani 1.85 milioni sawa na Sh4.8 bilioni.
Ndekidemi alitoa maelezo hayo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Mabutu, anayesikiliza shauri hilo wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Alidai kutokana na upelelezi kutokukamilika, anaomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama umekamilika.
Hakimu Mabutu amekubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hadi Mei 29, 2024, itakapoitwa kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.
Mbali na Kipande, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 38/2022 ni Peter Gawile (58) aliyekuwa Ofisa Rasilimali Watu wa TPA na mkazi wa Mianzini; Casmily Lujegi (65) mkazi wa Mbezi Juu na Mwenyekiti wa Bodi ya Manunuzi wa TPA; Mashaka Kisanta (59) Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi, Kilian Chale (51) Kaimu Mkurugenzi Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, na Andrew John. Machi, 27, 2023, Serikali ilisema ipo katika hatua za mwisho kuwasilisha taarifa muhimu Mahakama Kuu, baada ya upelelezi wa shauri hilo kukamilika.

Hata hivyo, Aprili 25, 2023, Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) aliagiza jalada la kesi hiyo, lifanyiwe mapitio upya kabla ya kuendelea na hatua nyingine.
Hatua hiyo ilitokana na washtakiwa kupeleka barua za malalamiko kwa DPP kuhusu kesi hiyo ilikiwemo kucheleweshwa kuendelea na hatua nyingine baada ya upelelezi kukamilika. Pia, Julai 11, 2023 Mahakama ilitoa siku 30 kwa Serikali kulifanyia kazi jalada hilo ili liendelee na hatua nyingine ambayo ni kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo washtakiwa hao.
Mahakama ilifikia uamuzi huo baada ya kuelezwa na upande wa mashtaka kuwa jalada halisi la kesi hiyo lipo Dodoma, makao makuu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) kwa ajili ya kufanyiwa kazi. Hata hivyo, baadaye upande wa mashtaka, waliieleza mahakama kuwa bado wanaendelea na upelelezi wa shauri hilo.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kati ya Oktoba Mosi, 2014 na Oktoba Mosi 2020 jijini Dar es Salaam, walikula njama ya kutenda kosa la kuisababishia TPA hasara ya Sh4.2 bilioni.

Pia, kati ya Januari Mosi, 2015 hadi Februari 17, 2015 washitakiwa kwa pamoja wakiwa maofisa wa TPA, walitumia madaraka yao vibaya kwa kutangaza zabuni namba AE/016/2014-15/CTB/G/39 kwa nia ya kujipatia Dola za Marekani 1,857,908.04.
Shitaka la tatu, inadaiwa kati ya Oktoba Mosi, 2014 na Oktoba Mosi, 2020 eneo la TPA na maeneo mengine ya Dar es Salaam, washtakiwa kwa makusudi walitangaza zabuni ya Enterprises Planning Resources (ERP) bila kupata kibali cha bodi ya zabuni ya mamlaka hiyo na kushindwa kufuata kanuni za zabuni, , hivyo kutoa malipo ya awali ya asilimia 40 bila idhini ya bodi hiyo, jambo lililosababisha TPA hasara ya Dola 1.8 milioni ambazo ni sawa na Sh4.2 bilioni.