Upembuzi yakinifu waanza kuongeza kiwango cha umeme Zanzibar

Wadau wa umeme wakiwa katika kikao cha uwasilishaji wa hatua za awali kwa Tanesco na Zeco kuhusu ujenzi wa njia kuu za kusafirisha umeme ili kuongeza upatikanaji wa nishati hiyo kisiwani Zanzibar.

Muktasari:

  • Kampuni hizo zikiongozwa na  CECI ni  ELC kutoka nchini Italia sambamba na Colenco ya Nigeria.

Unguja. Serikali imeanza mchakato wa kuimarisha njia zinazosafirisha umeme kwa njia ya bahari kutoka Tanzania Bara, ili kuondoa changamoto za upatikanaji wa huduma hiyo zinazotokana na kuzidiwa na mahitaji yaliyopo.

Kazi hiyo inafanywa kwa ushirikiano kati Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na  Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) kwa kubadilisha nyaya zinazopeleka umeme kutoka Ubungo Dar es Salaam hadi Fumba Unguja, na ule unaotoka Tanga hadi Wesha Pemba.

Hayo yameelezwa  baada ya kikao kazi kilichowakutanisha watendaji wa Tanesco na Zeco, wadau wa wizara za ardhi na nishati pamoja na timu ya wataalamu wanaofanya upembuzi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya  kikao hicho jana Ijumaa, Aprili 26, 2024 Meneja Mipango, Uwekezaji na Biashara wa Zeco, Ibrahim Mussa Haroun, amesema nyaya zinazotumika sasa ni za miaka mingi na zimezidiwa na ongezeko la matumizi ya nishati ya umeme nchini.  

“Serikali zetu zimeona ipo haja sasa kuziongeza uwezo njia hizo zinazoleta umeme visiwani mwetu, kutoka Dar-Fumba megawati 132 itakayoongezwa hadi megawati 220.”

Amesema, kutoka megawati hizo za sasa kwenda megawati 220, ni lazima kuangalia upya maeneo yatakayopitishwa nyanya hizo ambazo bila shaka utapita kwenye maeneo yenye makazi ya watu, mashamba na shughuli nyingine za kijamii.

Amefafanua kuwa  kazi inayofanywa sasa na wataalamu walioajiriwa kutoka kampuni tatu za kigeni inalenga kupata taarifa za kiufundi, athari za kimazingira zinazoweza kujitokeza, gharama za kukamilisha mradi huo pamoja na kutoa ushauri elekezi.

Kampuni hizo zikiongozwa na  CECI ni  ELC kutoka nchini Italia sambamba na Colenco ya Nigeria.

Amesema mradi   huo pia utahusisha kukiunganisha kisiwa cha Mafia na gridi ya Taifa kutokea Mkuranga mkoani Pwani, na kuwawezesha wananchi wa huko kuondokana na matumizi ya vinu kupata nishati hiyo. 

Kwa mujibu wa Zeco, Pemba kwa sasa inapata megawati 20 wakati matumizi yake yamefikia Kilovati (Kv) 13, hali inayoonyesha zinapungua uwezo hivyo Serikali zimeamua kupeleka megawati 132 kupitia mradi huo.

Amesema ripoti itakayotolewa baada ya upembuzi huo, itaelekeza namna bora ya kufanikisha mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB).

Meneja wa maandalizi ya mradi huo kutoka Tanesco, Alex Gerald Heruka amesema hatua hiyo ni muhimu kutokana na ongezeko la mahitaji ya umeme linalotokana na uwekezaji mkubwa wa miradi katika mataifa hayo.

Meneja wa kampuni ya CECI, Dario Provenzano amesema mradi huo ni muhimu kwa visiwa hivyo ili kuwezesha kukua kwa uchumi wa nchi na kuvutia uwekezaji zaidi.

Amesema kwa sasa wanaendelea kufanya utafiti na kuangalia mazingira ya maeneo yanayotarajiwa kupita nyaya hizo, akiahidi kuifanya kazi hiyo kwa viwango vinavyotarajiwa.

“Wakati tukiendelea kufanya kazi, huku kwa mara vya kwanza kisiwa cha Mafia kinakwenda kuunganishwa na umeme wa gridi ya Taifa, ni matarajio kampuni zetu zitaacha alama kubwa ya ufanisi uliotukuka,”amesema.

Mkataba wa upembuzi huo ulisainiwa Februari 20, 2024, ukitarajiwa kudumu hadi Agosti mwaka huu, timu hiyo itakapokutana tena  kuchambua matokeo yake kabla kuingia kwenye hatua ya utekelezaji wake.

Kisiwa cha Pemba kiliunganishwa na gridi ya Taifa kutoka Tanga Juni, 2010 kwa urefu wa kilomita 70, wakati Unguja iliunganishwa mwaka 1978, na kubadilishwa mnamo 2013 kutokana na uchakavu.