Utata wanafunzi kufungua shule Rufiji, mafuriko yakiongezeka

Mkazi wa Kijiji cha Mohoro wilayani Rufiji akihamishia vyombo vyake darasani mwishoni mwa wiki iliyopita kutokana na mafuriko yaliyoikumba wilaya hiyo.

Muktasari:


  • Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele, amesema ratiba za shule hazitasitishwa kutokana na mafuriko yaliyoikumba wilaya hiyo, badala yake wanafunzi watapangiwa shule nyingine.

Dar es Salaam. Wakati Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani, Aboubakar Chobo akishauri shule za msingi na sekondari zisitishwe kwa muda kutokana na mafuko yaliyoikumba wilaya hiyo, mkuu wa wilaya hiyo, Meja Edward Gowele amesema ratiba ya masomo inaendelea kama kawaida.

 Mafuriko hayo yanayotokana kufunguliwa kwa bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere (JNHPP) kutokana na ongezeko la mvua nchini, yamewakosesha makazi mamia ya wananchi na kufunika mashamba vijijini.

Akizungumzia utata wa wanafunzi kwenda shule zilizofunguliwa leo Aprili 8, 2024 Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele amesema ratiba za shule hazitasitishwa, bali wanaandaa utaratibu wa wanafunzi kusoma hata kwenye shule ambazo sio zao.

“Hatujabadilisha utaratibu, ila tunachofanya kuna watoto wanaosoma shule upande mwingine, hivyo wanalazimika kuvuka kwa boti, tumewaambia wabaki upande waliopo, ili wasome kwenye shule za upande huo na wale wa upande mwingine wabaki huko huko wasome hata kama shule sio zao,” amesema.

Amesema maofisa elimu wametumwa kuratibu suala hilo, ili kuhakikisha ratiba za masomo zinaendelea kama kawaida.

“Kwenye maeneo yasiyo na shule tumeaagiza wenye boti wasiwatoze wanafunzi nauli, ili wawahi shuleni,” amesema.

Amesema wanaendelea kufanya uchambuzi wa hali hiyo kwa kushirikiana na timu ya uokozi kutoka mkoani iliyotumwa kuratibu usalama wilayani humo.

Kuhusu madarasa ya mitihani ya kitaifa, amesema wanafanya utaratibu wa kuwabakiza wanafunzi mahali pamoja, ili wasilazimike kusafiri mara kwa mara.

Kuhusu shule shikizi, amesema wanaangalia kama maeneo wanayosomea hayapitiki, watoto wasiende shule.

Awali, akizungumza na Mwananchi Digital leo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Rufiji, Aboubakar Chobo amesema wanakusudia kumshauri mkuu wa wilaya hiyo kusitisha masomo kwa muda, ili yasije yakatokea maafa.

“Tutamshauri mkuu wa wilaya tusitishe masomo kwa muda kwa sababu maji yamezingira maeneo yote. Mtoto atapitaje kwenda shule. Kumbuka hizi shule zina wanafunzi wengi, shule ya Mohoro ina wanafunzi zaidi ya 1,500 na Nyampaku nayo ina zaidi ya 1,500, wanatoka maeneo mablimbali na wakifika shule watatoka kwenda kunywa chai na chakula cha mchana, sasa watatoka kwa hali hiyo?” amehoji.

Mbali na shule hizo za msingi, Chobo amesema kuna shule shikizi ikiwemo ya kitongoji cha Nyandote yenye wanafunzi 150 wa shule ya awali na darasa la kwanza na Nyamudege yenye wanafunzi zaidi ya 70, ambako amesema kumejaa maji na hakufikiki.

“Kufika shule ya Nyandote ni kilometa sita kwa boti na Nyamudege ni kilometa nane kwa boti, kiusalama si vizuri kuwapeleka watoto hawa kwa boto kila siku. Hivi boti ikizama watoto wakifa unadhani Serikali itatuelewa? Ni afadhali tuombe wasitishe masomo angau kwa mwezi mmoja, ili maji yapungue,” amesema.

Hata hivyo, amesema kwa madarasa ya mitihani ya kitaifa wameiomba Serikali isaidie magodoro na chakula, ili watoto wakae eneo moja.

Hata hiivyo, amesema baadhi ya wazazi waliokuwa wamehamia shule ya msingi Mohoro, wameondoka na zimebaki familia za walimu pekee.

Mwalimu anayefundisha katika shule ya msingi Nyampaku, ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema wazazi waliokuwa shule wameondoka na masomo yanaendelea.

Serikali kujenga mabwawa

Katika hatua nyingine, Wizara ya Kilimo imepanga kutatangaza zabuni ya kuanza ujenzi wa mabwawa mawili katika eneo chini la bwawa wa kuzajilisha umeme la Julius Nyerere (JNHPP), hatua itakayosaidia pia kukabiliana na mafuriko kwenye wilaya za Rufiji na Kibiti mkoani Pwani.

Akijibu maswali ya nyongeza ya Mbunge wa Viti Maalum Subira Mgalu leo bungeni jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Kilimo David Silinde amesema ni kweli Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji watatangaza zabuni ya kujenga mabwawa makubwa mawili katika eneo la chini la JNHPPP katika maeneo ya Ngorongo na Umwe.

Amesema ujenzi huo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa alipotembelea bwawa la Mwalimu Nyerere na hivyo wanakwenda kulitekelezeka kuhakikisha wanapunguza athari za mafuriko katika mto Rufuji.

Kuhusu kuandaa mwongozo, Silinde amesema ushauri wameupokea na watafanyaia kazi kwa sababu jukumu la Serikali ni kuwasikiliza wananchi wake.

Katika swali lake, Subira amehoji Serikali haioni haja ya ujenzi wa mradi huo kuendana na mradi wa kujenga kesho iliyobora (BBT).

Pia amesema panapotokea masuala ya mafuriko huwa mashamba ya umwagiliaji yanapata changamoto ya kuharibika kwa mazao na kutoa mfano skimu ya umwagiliaji ya Bagamoyo.

Katika swali la msingi, Subira amehoji Serikali ina mpango gani wa kuanzisha mradi wa BBT katika Bonde la Mto Rufiji.

Akijibu, Silinde amesema hadi kufikia Machi, 2024 jumla ya ekari 340,245.3 zimebainishwa na kupimwa afya ya udongo kwa ajili ya programu ya BBT katika mikoa ya Dodoma, Kigoma, Mbeya, Singida, Tanga, Njombe na Kagera.

Silinde amesema katika mwaka wa fedha 2024/2025, wizara imepanga kuanza mradi wa BBT kwa halmashauri 100 zitakazotenga maeneo (hekta 200) kwa kujenga miundombinu ya umwagiliaji na kutoa utaalamu.