Uteuzi Profesa Assad kusuluhisha kampuni za mafuta ngoma bado mbichi

Muktasari:

  • Profesa Assad aliteuliwa na kampuni ya Oilcom kuwa mmoja wa wasuluhishi katika mgogoro wake na kampuni za Oryx, lakini Oryx zilimkataa. Hata hivyo Profesa Assad aligoma ndipo Oryx zikaenda kumpinga mahakamani, mvutano unaoendelea mpaka sasa baina ya kampuni hizo mbili.

Dar es Salaam. Hatima ya uteuzi wa aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, kuwa mmoja wa wasuluhishi wa mgogoro wa kampuni mbili za mafuta, unaopingwa mahakamani bado iko njia panda.

Hii inatokana na uamuzi wa Mahakama ya Rufani kukataa harakati za kampuni ya Oilcom Tanzania Limited kutaka kuzima rufaa ya kupinga uteuzi wake kuwa msuluhishi wa mgogoro baina ya kampuni hiyo na kampuni za Oryx Oil company Limited na Oryx Energies SA.

Oilcom ilifungua shauri la maombi mahakamani hapo ikiiomba Mahakama hiyo iitupilie mbali notisi ya rufaa iliyowasilishwa na kampuni za Oryx, ikikusudia kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliobariki uteuzi wa Profesa Assad kuwa msuluhishi katika mgogoro huo.

Kampuni hiyo ilidai Oryx zilishindwa kukata rufaa hiyo ndani ya muda wa siku 60 uliowekwa na Kanuni za Mahakama ya Rufaa, tangu tarehe ya kuwasilisha notisi ya rufaa.

Hata hivyo, kampuni hiyo imekwaa kisiki katika harakati hizo baada ya Mahakama hiyo kutupilia mbali shauri hilo.

Uamuzi huo umetolewa Aprili 9, 2024 na jopo la majaji watatu waliosikiliza shauri hilo, Dk Gerald Ndika (Kiongozi wa jopo), Patricia  Fikirini na Issa Maige, baada ya kukubaliana na hoja za kampuni za Oryx.

Mahakama hiyo imekubaliana na hoja za kampuni za Oryx kuwa kuchelewa kwake kukata rufaa kulitokana na kuchelewa kupata nyaraka muhimu kutoka kwa msajili licha ya kwamba waliziomba mapema, huku zikiwasilisha barua ya msajili ya kuthibitisha kuchelewa kuwapatia nyaraka hizo.

Wakili wa Oilcom, Thomas Laizer katika kiapo chake na wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo alidai nyaraka za rufaa zilikamilika mapema na wao walijulishwa na msajili kuwa nyaraka hizo zilikuwa tayari Julai 19, 2023.

Hoja hizo zilipingwa na Mkuu wa Idara ya Sheria ambaye pia ni Katibu wa kampuni za Oryx, Antonia Kilama katika kiapo chake, na wakili Gaspar Nyika wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo.

Walidai nakala ya amri ya Mahakama haikuwa tayari  kuchukuliwa mpaka Januari 17, 2024 msajili alipowaandikia kuwajulisha nyaraka zote ziko tayari, na akatoa hati ya uchelewaji, na Januari 23, 2024 walikata rufaa iliyosajiliwa kwa namba 47 ya mwaka 2024.

Mahakama imekubaliana na hoja hizo pamoja na ushahidi wa barua za kuomba nyaraka hizo, na za kumkumbusha msajili sambamba na ya msajili kuwajulisha kuwa nyaraka hizo ziko tayari na hati ya ucheleweshaji.

Hivyo imesema kuwa kwa kuzingatia hati ya ucheleweshwaji ambayo inaondoa muda wa kusubiria kupata nyaraka hizo kutoka kwa msajili katika kuhesabu siku 60 za kukata rufaa, rufaa iliyokatwa na kampuni hizo Januari 23, 2024, ni halali na imekatwa ndani ya muda.

"Matokeo yake tumeamua kuwa shauri la maombi (lililofunguliwa na Oilcom ikiomba kutupilia mbali notisi ya rufaa ya kampuni za Oryx) halina ustahilifu na linatupiliwa mbali na mdaiwa anapaswa alipe gharama za kesi."

Kwa uamuzi huo rufaa ya kampuni za Oryx inaendelea kusimama na inasubiri kusikilizwa jambo ambalo linauweka njia panda uteuzi wa Profesa Assad, katika kuendelea na jukumu la usuluhishi wa mgogoro wa kampuni hizo, kutegemeana na uamuzi wa Mahakama ya Rufani.


Historia ya mgogoro uteuzi wa Profesa Assad

Awali, kampuni hizo ziliingia katika mgogoro uliotokana na kutokubaliana katika tafsiri ya baadhi ya vifungu vya makubaliano zilizoingia  Novemba 18 na Desemba 5, 2016.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo mgogoro au tofauti baina yao utawasilishwa katika jukwaa la usuluhishi linaoundwa na wasuluhishi watatu, huku kila upande ukiwa na haki ya kuchagua msuluhishi wake na yule anayechaguliwa na pande zote kuwa mwenyekiti.

Hivyo kampuni ya Oilcom ilimteua Profesa Assad, lakini Oryx zilimkataa kutokana na taarifa zilizoko katika hati ya wasifu wake  (curriculum Vitae - CV), zinaonyesha kuwa Machi 2006 alifanya kazi na kampuni ya Oilcom akiwa  mshauri pekee katika mpango wa biashara.

Kwa taarifa hizo ambazo hazikuwa zimewekwa wazi kwao ziliibua mashaka kuhusu uhuru wake akikaa kama msuluhishi katika mgogoro wao. 

Hivyo Machi 11, 2022 zilimwandikia barua Profesa Assad zikimtaka ajiondoe, lakini Profesa Assad aligoma.

Katika majibu yake kupitia barua yake ya Machi 16, 2022 alikana kufanya kazi na kampuni ya Oilcom katika wakati wowote, alidai kuwa mradi huo ulikuwa ukiendeshwa kwa kushirikiana na Manispaa ya Ilala ambayo ndio mteja aliyemuhusisha.

Hivyo alidai kuwa wakati wote huo hakuwahi kuwa na mawasiliano wala kukutana na mtu yeyote kutoka katika menejimenti ya kampuni ya Oilcom, na yupo huru haoni mgongano wa masilahi kuwa msuluhishi wa mgogoro huo.

Kutokana na msimamo huo wa Profesa Assad, kampuni hizo za Oryx zilikwenda kumpinga mahakamani, ambapo zilifungua shauri la  maombi namba 138 la mwaka 2022, Mahakama Kuu zikiiomba imuondoe katika nafasi hiyo na imteue msuluhishi mwingine.

Shauri hilo lilisikilizwa kwa njia ya maandishi na Oryx pamoja na mambo mengine zilifafanua hoja zake na hofu yake kuwa katika mazingira hayo yanaathiri uhuru wa Profesa Assad, kuwa hataweza kutenda haki kwenye shauri ambalo mteja wake ni mdaawa ambaye anaweza kumpendelea.

Hivyo Oryx zilihitimisha kuwa Oilcom haikutimiza matakwa ya sura ya 15 (Sheria ya Usuluhishi, kwa kumteua msuluhishi ambaye ana mahusiano naye).

Hata hivyo Oilcom ilidai kuwa hofu ya Oryx haina uthibitisho bali ni nia ovu iliyopangwa kuchelewesha mchakato wa usuluhishi, ikidai kuwa Profesa Assad peke yake haiwezi kuwa na ushawishi kwa jopo zima.

Oilcom ilidai kuwa sababu zilizotolewa hakidhi kuhitimisha kuwa kuna uwezekano wa msuluhishi huyo kuwa na upendeleo.

Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Mustapha Ismail Oktoba 18, 2022, ilitupilia mbali shauri hilo la kampuni za Oryx baada ya kukataa hoja za Oryx,  ikisema kuwa hazikukidhi vigezo vya tafsiri ya upendeleo.

Jaji Ismail alisema kuwa kilichodaiwa na waombaji (Oryx) ni dhana ya kufikirika na kwamba ingeleta maana kama msuluhishi huyo, Profesa Assad angekuwa msuluhishi pekee, lakini ni mmoja tu katika jopo la wasuluhishi watatu.

"Uamuzi katika shauri la usuluhishi ni wa wasuluhishi walio wengi. Msuluhishi mmoja pekee hawezi hata awe na ushawishi, kuyumbisha uamuzi wa jopo", alisema Jaji Ismail.

Hivyo Jaji Ismail alihitimisha kuwa hisia za upendeleo, zilizodaiwa na Oryx ni za kimtazamo zaidi kuliko uhalisia, ambazo hazijafaulu katika kiwango cha juu cha ufahamu au tuhuma zenye mashiko

Kufuatia uamuzi huo, Oktoba 28, 2022, siku 10 baadaye kampuni hizo iliwasilisha katika Mahakama ya Rufani notisi ya kukata rufaa kupinga uamuzi huo wa Mahakama Kuu.

Baada ya notisi hiyo zilipaswa zikate rufaa rasmi ndani ya siku 60, tangu tarehe hiyo ya notisi ya rufaa ambazo ziliishia Desemba 27, 2022.

Hata hivyo takribani miezi 10 ilikatika bila kampuni za Oryx kufungua rufaa hiyo, ndipo Oilcom ikafungua shauri la maombi kuiomba Mahakama ya Rufani iitupilie mbali notisi hiyo ya rufaa ya Oryx.