VIDEO: Chacha Heche ashinda uenyekiti Chadema Mara akiwa nje ya nchi

Chacha Heche

Muktasari:

  • Chacha Heche amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Mara baada ya kupata kura 59, sawa na asilimia 53 akiwa nje ya nchi, akiwashinda wenzake wawili waliopata kura 25 kila mmoja.

Musoma.  Aliyewahi kuwa katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mara, Chacha Heche amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa mkoa wa chama hicho akiwashinda wenzake wawili.

Heche ambaye yupo nchini India alikomsindikiza ndugu yake kwa matibabu, ameomba kura kwa njia ya mtandao, kwenye uchaguzi uliofanyika mjini Musoma jana Machi 27, 2024.

Akitangaza matokeo hayo, mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi huo, Suzan Kiwanga amesema Heche amepata kura 59 sawa na asilimia 53; huku wenzake Bashiri Selemani na Jacob Maiga wakipata kura 25 kila mmoja, kwenye awamu ya pili ya upigaji kura.

Uchaguzi huo ulirudiwa baada ya awamu ya kwanza wagombea wote kutokufikisha nusu ya kura zinazohitaji kwa mujibu wa kanuni.

Awali Heche alipata kura 52 huku wagombea wenzake kila mmoja akipata kura 29.

“Kwa nafasi ya uenyekiti wa mkoa, namtangaza ndugu Chacha Heche aliyepata kura 59, sawa na asilimia 53 dhidi ya Selemani aliyepata asilimia 22.7 na Maiga ambaye pia amepata asilimia 22.7,” amesema Kiwanga.

Katika uchaguzi huo ambao ulimalizika usiku wa manani, Donald Mwembe alichaguliwa kuwa katibu baada ya kupata kura 60 dhidi ya Angela Lima aliyepata kura 45 na Deus Kaki aliyepata kura sita.

Heche ashinda uenyekiti Chadema Mara akiwa nje ya nchi

Akizungumza kwa njia ya mtandao baada ya kuchaguliwa, Heche amewashukuru wajumbe kwa kumwamini na kumpigia kura licha ya kuwa hakuwepo ukumbini.

Amesema kazi kubwa aliyonayo ni kuongeza mfumo wa namna ya kukiunganisha chama zaidi na kwamba kutakuwepo vikao vya ndani ya chama na sera ambazo zitatangazwa kwa wananchi, zikiwa na lengo la kuwaunganisha zaidi.

“Natamani viongozi wa ngazi zote wafanane na wananchi, walie na wanachi, wapaze sauti za wananchi. Tusipaze sauti zetu sisi wenyewe badala yake tupaze sauti za wananchi, tuwe na sera zinazoendandana na itikadi na falsafa za chama chetu, sera ambazo lazima ziguse maisha ya kila siku ya wananchi, ndipo chama chetu kitakuwa chama kinachotokana na wananchi,” amesema.

Pia, ameushukuru uongozi wa chama hicho kwa namna ulivyokiwezesha kupiga hatua, hasa katika masula ya teknolojia na kidigitali, hali iliyomwezesha kushiriki mchakato wa uchaguzi tangu awali hadi mwisho kwa njia ya kidijitali.

Amesema mfumo huo utaendelea na hivyo umbali hautakuwa kikwazo tena katika utendaji wa kazi wa kila siku na mfumo umeonekana uko imara na msaada hasa kwa viongozi, ambao kwa namna moja au nyingine wanajikuta hawapo nchini au eneo la tukio kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo za kimaisha.