VIDEO: Mji wa wavuvi uliogeuka magofu Mtera

Baadhi ya nyumba zilizoachwa na wavuvi waliokuwa wakiishi kwenye Kitongoji cha Chamdumbi A, kilicho Kijiji cha Mtera, mkoani Dodoma. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Miaka mitano iliyopita samaki waliovunwa Bwawa la Mtera walikuwa tani zaidi ya 2,000 kwa mwaka, tofauti na sasa hata kufikia tani 1,000 kwa mwaka ni changamoto.

Dodoma. Ukiangalia pande zote unakuta nyumba zilizobomoka, nyingine mazingira yake yameota majani.

Majengo haya yalitumika kibiashara zikiwamo za baa, migahawa na maduka.

Baadhi hivi sasa yamegeuka stoo na wengine wakiyatumia kwa malazi.

Kulikoni hali imekuwa hivyo? Sababu inaelezwa ni kutokana na kupungua samaki kwenye Bwawa la Mtera, hivyo wavuvi kuhama kuelekea maeneo mengine kutafuta maisha.

Hapa ni Kitongoji cha Chamdumbi A, katika Kijiji cha Mtera mkoani Dodoma.

Mwenyekiti wa kijiji, Simon Lukui, anakadiria hadi mwaka 2018 kitongoji kilikuwa na wavuvi zaidi ya 1,000 lakini sasa hata 100 hawafiki.

Lukui anasema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 kijiji kilikuwa na wakazi 7,992 lakini sasa hawazidi 3,000.

Kisa cha uhaba wa samaki kwenye bwawa la Mtera kilivyosababisha wavuvi kukimbia maeneo yao

Akizungumza na Mwananchi Digital, Lukui anasema hali ya uvuvi kwa zaidi ya miaka mitatu imekuwa mbaya, hivyo wavuvi wamehama kuelekea Bahi mkoani Dodoma, Manyara na Tabora.

“Kitongoji hiki kilikuwa na watu wengi lakini kimebaki magofu kutokana na ukosefu wa samaki, hivyo kuwafanya kukimbilia maeneo mengine kutafuta riziki,” anasema Lukui ambaye pia ni mvuvi.

Ingawa hafahamu sababu halisi za samaki kupungua, Lukui anasema walianza kuadimika miaka minne iliyopita baada ya maji kujaa bwawani yakiwa na rangi tofauti na waliyoizoea. Yalikuwa ya kijani badala ya bluu bahari.

Anaeleza wavuvi walianza kuhangaika kutokana na kipato kupungua kwa sababu shughuli waliyoitegemea ni uvuvi.

Lukui anayeishi kitongoji hicho, anaeleza awali alipata faida ya hadi Sh50,000 kwa siku tofauti na sasa hata Sh5,000 ni nadra kuipata.

Anaeleza kijiji kiliingiza mapato kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa lakini hakuna kinachopatikana hivi sasa zaidi ya kitoweo pekee.

Ukosefu wa samaki anasema umeathiri shughuli nyingine za kiuchumi, ikiwemo ufugaji kwani wafugaji waliwauzia wavuvi nyama na maziwa.

John Kwasisi, mvuvi katika Kitongoji cha Kenya, wilayani Iringa akizungumza na Mwananchi Digital kwenye mwalo wa samaki uliopo kitongojini hapo. Picha na Merciful Munuo

Utafiti ufanyike

Ameomba mashirika yasiyo ya kiserikali kufanya utafiti kubaini chanzo cha samaki kupungua.

Slyvester Fabian, aliyeanza uvuvi mwaka 2002 anasema wakati huo alipata samaki 1,000 kwa mitego 10 lakini sasa hata atege 50 kupata samaki 200 ni ngumu.

Anasema kulikuwa na magugu mengi bwawani ambayo watu waliyakata kwa ajili ya kuezeka nyumba, hali iliyosababisha kupungua mazalia ya samaki.

Fabian anasema yalipofunguliwa maji, watu waishio kando mwa bwawa kutoka Dodoma hadi Mikumi walivua samaki wengi kwa kutumia ndoano na wavu.

Mkoani Iringa

Mvuvi kutoka Kitongoji cha Kenya wilayani Iringa, John Kwasisi anasema alifika Mtera Januari Mosi, 1984.

Anaeleza kupungua samaki kunatokana na matumizi ya nyavu zisizoshauriwa kitalaamu na shughuli za kilimo maji yanapopungua bwawani.

“Wenzetu maji yanapopungua wanalima nyanya, matikiti na wanatumia dawa za kuua wadudu, wanapomwagilia maji yanarudi bwawani. Samaki wanadumaa,” anaeleza.

Ameiomba Serikali kudhibiti shughuli za kilimo pembezoni mwa bwawa.

Pia anasema wafugaji hupeleka ng’ombe bwawani kunywesha maji, hivyo huvuruga mazalia ya samaki.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kenya, Mariam Njowoka anasema ufugaji na kilimo vimechangia kupungua samaki bwawani.

“Ukianzia Pawaga (wilayani Mpwapwa) mashamba yameshamiri kwa hiyo mbolea inakuja hadi huku na kuathiri samaki. Serikali tunaomba mtusaidie,” anasema akionyesha jiko alilotengeneza kukaushia samaki likiwa halina matumizi.

Waiangukia Serikali

Fabian ameiomba Serikali kupanda samaki aina ya perege kuongeza idadi japo waliopo hufika bwawani kupitia mito asili lakini hawatoshelezi mahitaji.

Anasema samaki wanaopatikana wamedumaa hivyo kutofikiwa katika nyavu yenye ukubwa wa nchi tatu ambayo ndiyo inayotakiwa na Serikali.

Fabian anasema sheria ya uvuvi inataka mtu mwenye mtumbwi unaozidi urefu wa futi 12 kukata leseni, lakini wao wamekuwa wakilipa leseni hadi katika mitumbwi iliyo chini ya urefu huo.

“Leseni tunayokata Halmashauri ya Mpwapwa ukifika Iringa unatakiwa kuwa na nyingine ya huko. Najiuliza kwa nini madereva leseni zao zinakuwa za nchi nzima lakini siyo sisi. Tunalipia leseni ya uvuvi, na chombo tunalipia Sh21,000 kwa mwaka,” anasema.

Baadhi ya nyumba zilizoachwa na wavuvi waliokuwa wakiishi kwenye Kitongoji cha Chamdumbi A, kilicho Kijiji cha Mtera, mkoani Dodoma. Picha na Merciful Munuo

Mfanyabiashara wa samaki, Andrew Fredrick, maarufu Mambetani, ameiomba Serikali isaidie ufugaji samaki kwenye vizimba kuepusha changamoto ya upatikanaji wa kitoweo hicho.

“Kutokana na hali mbaya ya upatikanaji samaki, utafiti ufanyike wa kupanda wengine,” anasema.

Anaeleza mapato yake awali yalimwezesha kusomesha wanafunzi hadi chuo kikuu, lakini sasa hawezi kutokana na biashara kuyumba.

Fredrick anasema alianza ujenzi wa nyumba ya wageni ambayo ameshindwa kuikamilisha kutokana na biashara kuyumba na mtaji kupotea.

Mvuvi na mchuuzi wa samaki, Christoms Lupindu anasema samaki wa asili wa bwawa hilo ni perege ila baada ya maji kufunguliwa wametoweka kwa zaidi ya miaka mitano.

“Yametoweka maji ya asili ambayo ni rafiki kwa perege, hawapo tena, sasa tunavua kidogo kambale, ngogo mchena, ngalala, na vitoga. Perege waliokuwa wanatamba Mtera hakuna tena, ukiona mtu anakuuzia wametoka Tabora au Bahi,” anasema.

Josephat anasema alivua kilo 200 hadi 300 za samaki awali, ambazo alizigandisha kwenye jokofu na kuziuza Ruvuma, Mbeya na Iringa.

Daines Lutambi, anasema miaka mitano iliyopita alinunua samaki kwa Sh2,500 kwa kilo lakini sasa ananua Sh8,000 kwa kilo moja, hivyo faida ya biashara hutegemeana na bei ya samaki kwa siku husika.

Rehema Mwambetani, ameiomba Serikali iwapatie mikopo ili waachane na inayotolewa mtaani, maarufu ‘kausha damu’.

“Asilimia kubwa ya wanawake hapa getini (geti la Mtera), tuko hatarini kunyang’anywa vitanda, wengine wamepata changamoto ya hata nyumba kuuzwa kwa sababu ya mikopo hii ambayo ina riba kubwa,” anasema.

Sababu za kitaalamu kupungua samaki

Ofisa Uvuvi Mkoa wa Iringa, Peter Nyakigera anasema miaka mitano iliyopita walikuwa wanavuna samaki tani zaidi ya 2,000 kwa mwaka tofauti na sasa kufikia tani 1,000 kwa mwaka ni changamoto.

"Kwa mfano tukichukua robo ya mwaka kuanzia Oktoba hadi Desemba, 2023 zimevunwa tani 235. Ukiangalia kwa mwaka huwezi kufika tani 2,000. Bado ni changamoto tunaiona uvuvi umekuwa ukishuka kila mwaka,” anasema.

Nyakigera anataja sababu kuwa ni uharibifu wa mazingira, ukataji wa miti, uvuvi haramu, mvua nyingi na ukame kwa baadhi ya miaka, uvamizi wa watu katika maeneo ya makazi, kina cha bwawa kupungua na mabadiliko ya tabianchi.

Anasema baadhi ya vijiji ambavyo vingine vimesajiliwa viko eneo la hifadhi, hivyo kuwa na shughuli za kibinadamu kama vile za makazi na kilimo.

Kaimu Ofisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Mathew Sanga anasema shughuli za kilimo ndani ya bwawa zina athari kubwa kwa sababu zinaondoa mazalia ya samaki kwenye kingo.

Anasema wakati maji yanapopungua wakulima hulima ndani ya bwawa.

Sanga anaeleza matumizi ya viuatilifu yamechangia kuathiri uzaaji na ukuaji wa samaki kwa kuwa vinaua vifaranga na mazalia.

Pia anasema uharibifu wa uoto wa asili, kando mwa bwawa kwa watu kukata miti kwa matumizi ya kuni na shughuli nyingine za kibinadamu kunaathiri samaki.

“Samaki wanazaliana kando mwa miti asili, hutaga mayai yao lakini uoto huu umeondolewa kwa kuwa watu wengi wameanza kufanya shughuli za kilimo katika maeneo hayo,” anasema.

Amewataka wananchi kutolima ndani ya bwawa kulinda uoto wa asili na kuacha shughuli za uvuvi usiku, akihimiza wavuvi kutii sheria kwa kutumia nyavu halali zenye matundu si chini ya nchi tatu ili kufanya uvuvi endelevu.

Sanga anasema hatua zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwapeleka mahakamani wanaovunja sheria.


Nini kinafanyika

Akieleza hatua zinazochukuliwa na Serikali, Ofisa Uvuvi wa Mkoa wa Iringa, Peter Nyakigera anasema wako kwenye majadiliano kuona watafanya nini kwa sababu suala hilo ni mtambuka, likihusisha wizara zaidi ya moja.

“Tunajua umuhimu wa bwawa katika kunufaisha nchi, samaki wanapatikana lakini pia ni chanzo cha nguvu ya nishati ya umeme. Kutokana na hilo tumekuwa tukipambana na mambo yanayoharibu,” anasema.

Anasema wamekuwa wakipambana na uvuvi haramu, hivyo wameanzisha vikundi shirikishi vya ulinzi vya rasilimali za uvuvi kwenye maeneo hayo.

Nyakigera anasema wapo katika mchakato wa kuhimiza ufugaji samaki kupunguza kasi ya kwenda kwenye hifadhi za bwawa.

Anasema wamekuwa na mikakati ya ujirani mwema na Mkoa wa Dodoma kuwezesha wanapolinda Iringa nao wajue namna ya kulinda.

Anasema mkakati huo unagusa changamoto zote zikiwamo za mazingira, uvuvi haramu, barabara, miundombinu ya masoko, ukitumia Sh9.154 bilioni.

Nyakigera anasema mkakati huo unashirikisha kamati za ulinzi za wilaya na mikoa ya Iringa na Dodoma, ambao ni wadau wa kuhakikisha rasilimali hizo zinakuwa endelevu.

“Tumekuwa tukiwashirikisha wadau wakiwemo TFS (Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania) na watu wa Tanapa (Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania) katika kulinusuru bwawa,” anasema.

Anaeleza wanashirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Samaki Tanzania (Tafiri) na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambao wanaenda kufanya utafiti kwenye bwawa hilo.

Anasema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imechukua hatua ya kupeleka ofisa uvuvi anayeshirikiana na jamii katika kuhifadhi rasilimali za bwawa hilo.

Kuhusu kupandikiza samaki, anasema SUA wanafanya utafiti utakaowezesha upandikizaji kongeza uzalishaji kwenye bwawa.

Anasema wataangalia mbegu bora, na watashauriana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuangalia namna ya kutenga mazalio ya samaki, ili wakati shughuli hiyo ikiendelea maeneo hayo yawe yamehifadhiwa kisheria na kikanuni.

Ametoa wito kwa wananchi kuhifadhi mazingira kwa kuwa suala hilo lina faida mtambuka kwa kizazi kilichopo na kijacho. Pia wajikite katika ufugaji kwenye mabwawa madogo na vizimba.

Amesisitiza vijiji vinavyozunguka bwawa kuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi, akieleza nusu yake havina mipango hiyo.

Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk Careen Kuhangwa anasema halijafanya utafiti katika bwawa hilo kujua iwapo kuna sababu ya mazingira iliyosababisha kupungua samaki.

Anasema kutokana na kutofanyika utafiti ni vigumu kusema sababu hasa za upungufu huo.


Usuli

Bwawa la Mtera lenye ukubwa wa kilomita za mraba 660, lilitengenezwa kuhifadhi maji ya kufua umeme, likianza kazi mwaka 1981.

Bwawa lipo eneo linalozunguka Halmashauri za Wilaya za Chamwino na Mpwapwa mkoani Dodoma na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Mkoa wa Iringa.

Uwepo wa bwawa hili umekuwa na faida kwa wananchi, likiwawezesha kufanya shughuli za uvuvi.

Aina ya samaki wanaovuliwa kwa kutumia mitumbwi ni perege, mchena, katoga, kambale, sulusulu, nkunga, ngobero, ndua, ngogo, mbapala, ngogomawe, justin, dagaa msumari, dagaa kamba, pua, ngalala na kimbumbu.

Habari hii imeandaliwa kwa kushirikiana na Bill & Mellinda Gates.