Vigogo 13 Chadema kikaangoni uchaguzi wa kanda

Muktasari:

  • Kanda hizo zinafanya uchaguzi baada ya kukamilisha mchakato huo kuanzia ngazi ya chini hadi mkoa

Dar es Salaam. Vigogo 13 wanaowania uenyekiti wa kanda nne kati ya  10 za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa sasa wanasubiri usaili ili kuteuliwa na kamati kuu baada ya mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu kukamilika.

Kanda hizo ni Victoria, Magharibi, Nyasa na Serengeti zinazounda mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera, Mara, Simiyu, Iringa, Mbeya, Njombe, Songwe, Rukwa na Shinyanga.

 Kanda hizi zinafanya uchaguzi baada ya kukamilisha mchakato huo kuanzia ngazi ya chini hadi mkoa.

Uchaguzi huo utakwenda sambamba na kuwapata makamu wenyeviti wa kanda hizo, wahazini, wenyeviti wa mabaraza ya Chadema katika ngazi ya mikoa yakiwamo ya Bazecha (Baraza la Wazee la Chadema) Bawacha (Baraza la Wanawake la Chadema) na Bavicha (Baraza la Vijana la Chadema).

Kwa mujibu wa tangazo la uchaguzi lililotolewa hivi karibuni na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (bara), Benson Kigaila, lilieleza kutafanyika pia uchaguzi wa kuwapata wekahazina.

Hadi sasa wagombea uenyekiti wa kanda ya Magharibi waliochukua na kurejesha fomu ni  Martin Daniel, Gaston Garubindi (anatetea nafasi yake) mawakili Dickson Matata na Nsassa Mboje, kwa mujibu wa katibu wa kanda hiyo, Ismail Kangeta.

Katibu wa kanda ya Victoria, Zakaria Obadi amewataja waliochukua na kurejesha fomu ni  Ezekiah Wenje anayetetea nafasi hiyo na John Pambalu ambaye ni mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha).

Wakati kanda ya Nyasa inayotajwa kuwa na ushindani mkali waliochukua fomu ni Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini na Mchungaji Peter Msigwa mbunge wa zamani wa Iringa Mjini anayetetea nafasi hiyo kwa awamu ya tatu.

Katika kanda ya Serengeti, yenye mikoa ya Mara, Simiyu na Shinyanga katibu wa kanda hiyo, Jackson Mnyawani amewataja waliochukua na kurejesha fomu ni Emmanuel Ntobi (mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Shinyanga) Lucas Ngoto, Butiko Mwija, James Mahangi na Gimbi Masaba.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema ameambia Mwananchi Digital leo Ijumaa Aprili 26, 2024 kuwa kikao cha kamati kuu cha kufanya usaili wa wagombea hao kitakafanyika baada ya kumalizika kwa maandamano ya amani ya chama hicho.

Alipoulizwa tarehe mahsusi ya kikao hicho cha kamati kuu, Mrema amesisitiza kuwa, “tukimaliza maandamano kamati kuu itaketi.”

Maandamano yanayoendelea maeneo mbalimbali nchi, yalianza Aprili 22 yatahitimishwa Aprili 30 mwaka huu.

Hata hivyo, taarifa ambazo Mwananchi imezipata kikao hicho cha kamati kuu huenda kikaketi kuanzia Mei 4 mwaka huu  na kitafanya usaili wa wagombea wa uenyekiti wa kanda, watakaohojiwa maswali mbalimbali ikiwamo sababu za kutaka nafasi hizo.

Taarifa hizo zinadokeza kuwa huenda uchaguzi wa kuwapata viongozi wapya wa kanda ukafanyika kuanzia Mei 15 au mwishoni, kulingana na uamuzi utakaotolewa au kufikiwa na wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Kwa sasa viongozi wakuu wa Chadema, wakiongozwa na mwenyekiti wao Freeman Mbowe na makamu wake bara, Tundu Lissu wapo kwenye wiki ya maandamano yaliyoanza Aprili 22 hadi 30 katika mikoa mbalimbali.

Lengo la maandamano hayo ni kufikisha kilio cha wananchi kuhusu ugumu wa maisha, madai ya Katiba mpya na kupata Tume Huru ya Uchaguzi iliyoanza kutumika na kupaza sauti ya namna Taifa litakavyoweza kukabiliana na majanga yakiwamo ya mafuriko.

Akizungumzia hatua hiyo, wakili Matata amesema yupo tayari kwa usaili wa mchakato huo, akisema ameshajiandaa kiakili kujibu maswali atakayoulizwa na wajumbe wa kamati kuu.

“Nipo tayari uzuri wenyewe nimeshaandaa ilani ya ndogo inayoelezea kwa nini ninahitaji kuwania nafasi hii, kikubwa nataka kuibadilisha Magharibi ili iwe na mvuto na amsha amsha kama iliyokuwa kipindi cha nyuma.

“Sasa hivi tumepoa nataka kuleta morali endapo nikifanikiwa kushinda uenyekiti wa kanda hii,” amesema Matata aliyewahi kuwa katibu anayesimamia idara ya haki za binadamu katika kanda hiyo yenye mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi.

Kama ilivyokuwa kwa wakili Matata, naye Ntobi amesema yupo tayari kwa mahojiano akisema anasubiri tarehe itakayopangwa na viongozi wakuu wa Chadema.

Sugu, Msigwa

Uchaguzi wa Kanda ya Nyasa unaokutanisha vigogo Mchungaji Msigwa na Sugu walioingia bungeni mwaka 2010, unasubiriwa kwa hamu na wanachama wa chama hicho hasa katika kanda hiyo.

Mchakato huo Nyasa utamaliza ubishi na tambo za vigogo zilizoshuka hadi kwa wafuasi wanaowaunga mkono, waliojigawa katika makundi tofauti katika kuhakikisha wagombea hao kila mmoja anaibuka kidedea.

Mchuano wa Sugu na Msigwa ulinogeshwa zaidi baada ya wafuasi wanaowaunga mkono kuamua kuwachukulia fomu kwa nyakati tofauti wagombea hao na kuwafikishia katika makazi yao.

Kama hiyo haitoshi baadhi ya wabunge wa zamani na wagombea ubunge wa 2020 kupitia chama hicho, wameweka wazi kuwa kambi za Sugu na Msigwa wakidai kuwa na imani na watu hao wanaowania nafasi hiyo.

Wawili hao ambao wote ni wajumbe wa kamati kuu kwa nyakati tofauti wamesema wako tayari kufanya mhadalo ili kuwawezesha wapiga kura wao wa Nyasa kuwafahamu.

Mtazamo wa wachambuzi

Baadhi ya wachambuzi wa siasa wamesema uchaguzi wa Nyasa utakuwa na mchuano mkali kulingana na aina ya wagombea waliojitokeza. Hata hivyo, wamewataka wagombea wanaowania uenyekiti kuwa makini na watulivu wakati wa usaili wao.

“Sugu ni mtu mwenye siasa za kiharakati zaidi, ana jazba na haraka katika kuwasilisha hoja yake, hata hivyo ni kiongozi anayejua kusimamia ukweli wa jambo analolipigania kwa wananchi. Akitoa hoja lazima atoe mifano halisi ya suala fulani.

“Msigwa ni kiongozi msikivu na mnyenyekevu wakati anawasilisha hoja yake, lakini yote kwa yote wapigakura ndio watakaofanya uamuzi,” amesema Kiama Mwaimu, mchambuzi wa masuala ya kisiasa.

Pia, Mwaimu amewataka wagombea 13 wa uenyekiti kuhakikisha wanajibu maswali kwa ufasaha na kuepuka kuwatuhumu washindani au mshindani husika ili kuleta utulivu katika mchakato huo.

“Kingine wagombea hawa lazima wajitofautishe wakati wanapotoa maelezo yao na waseme kwa kina nini wameamua kuwania uenyekiti wa kanda,” amesema Mwaimu.

Naye, Nassor Seif, mchambuzi wa kisiasa amewataka wagombea hao kujipanga vema kujibu maswali watakayoulizwa na wajumbe wa kamati kuu wakati wa usaili ili kuepuka kuenguliwa katika ngazi hiyo.

“Waepuke kuchafuana au kutuhumiana, kila mgombea ajieleze yeye mwenyewe husika pasipo kuingilia au kumsema vibaya mpinzani wake,” amesema Seif.

Kuhusu mchuano wa kanda ya Nyasa, Seif amesema:“Msigwa sio maarufu sana, lakini ni mtendaji kazi nzuri katika uongozi, lakini Sugu ni maarufu anayeungwa mkono.

“Kikubwa wagombea wote 13 wajiepushe na vitendo vya rushwa kwa sababu Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa) itakuwa kazini pia wakati mchakato huo ukiendendelea,”amesema.