Wadau mazingira wajizatiti kudhibiti chupa za plastiki         

Muktasari:

  • Wadau wa mazingira nchini wamedhamiria kuokoa mazingira kwa kuweka nguvu katika ukusanyaji na urejeshaji wa chupa za plastiki na kuzigeuza kuwa malighafi viwandani.

Dar es Salaam. Wadau wa mazingira nchini wamedhamiria kuokoa mazingira kwa kuweka nguvu katika ukusanyaji na urejelezaji wa chupa za plastiki na kuzifanya kuwa malighafi viwandani.

Akizungumza kwenye kikao na wakusanyaji chupa hizo kilichofanyika jana Februari 16, 2024  jijini hapa, Mratibu wa mjumuiko wa kampuni nane za uzalishaji wanaotumia chupa za plastiki kama vifungashio (PETPro Tanzania), Nicholaus Ambwene amesema lengo ni kutunza mazingira kwa kushirikiana na kampuni zinazozalisha chupa hizo.

Katika kutekeleza hilo amesema wamesajili baadhi ya viwanda vinavyokusanya chupa za plastiki kwa kuwapatia fedha za kuratibu pamoja na miundombinu, lengo likiwa ni kuweka mazingira safi ambapo kwa sasa wanaratibu hapa Dar es Salaam kisha kote nchini.

"Kwa takwimu zilizopo mwaka jana 2023 zimekusanywa chupa za plastiki tani 30,200 na zilizochakatwa ni tani 15,000 zingine zimepelekwa nje ya nchi, tumeanza na chupa za plastiki lakini tutakwenda na aina nyingine ya taka za plastiki," amesema.

Ambwene amesema jambo hilo ni wajibu wa ziada wa mzalishaji ambapo kwa hapa nchini wameanza mwaka 2022.

Amesema kwa nchi kama Afrika Kusini mchakato huu wameuanza miaka 30 iliyopita, hivyo inahitajika nguvu kubwa ili kufikia malengo.

Akizungumzia changamoto zilizopo, amesema bado kuna kampuni zinazozalisha kutumia chupa za plastiki lakini hazina mikakati ya kuzidhibiti na kuzirejeleza.


"Wengine ukiwafuata wanaona sheria bado ni changamoto kwani  uliopo ni mwongozo tu ambao hauwalazimishi kufanya hivyo. Ukiangalia  nchi nyingine kama Kenya tayari wanayo sheria," amebainisha Ambwene.

Amesema vilevile, bado kuna changamoto ya uelewa kwa jamii ikiwaona wanaookota chupa hizo kama watu wanaotumia dawa za kulevya na pombe kupitiliza, wezi au wahuni tu lakini bado wanaendelea kutoa elimu kwa jamii waipe thamani kazi hiyo.

Ameongeza pia, bado wazalishaji wanajivuta katika kuweka nguvu hivyo inawawia vigumu.

Kwa upande wake mmoja wa wakusanyaji chupa, Nassibu Kitabu amesema bado kuna unyanyapaa kwa jamii kwa kuwaona kama watu waliochanganyikiwa.

Kitabu ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya waokotaji taka rejeshi ya (JWPI), amesema wanaitaka Serikali itambue mchango wao katika kutunza mazingira pamoja na kuongezewa nguvu na wanaozalisha taka hizo.

"Taka rejeshi ni fursa na chanzo cha mapato na zinaboresha maisha ya watu kama zitatazamwa kwa mtazamo chanya, Serikali inapaswa kutambua kazi hii," amesema.

Naye, Richard Gabriel kutoka SB Plastiki inayojihusisha na uchakataji wa chupa za plastiki amesema changamoto iliyopo ni uwepo wa chupa za rangi ambazo zinachafua mazingira, hivyo mkakati uliopo ni kuona namna ya kuziondoa.