Wafuga kuku wafundwa kufuga kisasa

Washiriki wa mafunzo ya ufugaji bora wa kuku kibiashara wakimsikiliza mwasilishaji, Dk Fidelis Malthine kutoka kampuni ya Silverlands.

Muktasari:

  • Lengo la  elimu ni kuwajengea uwezo wa kufuga kuku wa kienyeji kwa njia za  kisasa na kibiashara ili kuinua uchumi wa kila mfugaji ambapo  Kampuni ya (Silverlands Tanzania Limited) mpaka sasa imefanikiwa kuwafikia wafugaji kuku milioni 10  nchini.

Kagera. Wafugaji zaidi ya 400 kutoka wilaya saba za Mkoa wa Kagera wamepatiwa mafunzo ya ufugaji kuku wa kienyeji kwa njia za kisasa na kibiashara ili wapate tija na kuinua uchumi wao.

Mafunzo hayo yamefanyika leo Jumapili Mei 5, 2024 na kampuni ya uzalishaji kuku na vifaranga ya Silverlands Tanzania Limited inayopatikana mkoani Iringa yakiwashirikisha wafugaji kutoka wilaya za Karagwe, Muleba, Missenyi, Biharamulo, Ngara na Kyerwa.

Wafugaji hao wamepewa elimu na mbinu sahihi za kufuga kuku kisasa na kibiashara kwa kuzingatia vyakula sahihi vya kuwalisha kuku, namna ya kutibu magonjwa na kutafuta masoko.

Meneja Masoko mkuu wa kampuni ya Silverlands, Mwanamvua Ngocho amesema lengo la kuwapatia elimu wafugaji wa kuku mkoani Kagera ni kuwabadilisha wafuge kwa njia za kisasa na kutambua fursa wanazoweza kuzipata pale wanapozalisha kuku kwa wingi.

“Tunaendelea kuunga mkono juhudi za serikali kuinua wakulima na wafugaji kwa kuwapatia elimu ya kuwawezesha kulima na kufuga kisasa, ili waweze kupata faida zenye tija kiuchumi na kuinua uchumi wao.”

Philibert Vedasto, mfugaji wa kuku kutoka kata ya Miembeni, manispaa ya Bukoba amesema ameanza kufuga kuku miaka miwili iliyopita, kila mwezi anachukua vifaranga vya kuku visivyopungua 1,000 ikipita miezi miwili anapata faida kubwa.

Ameiomba Serikali  kutafuta wadau wengine kuongeza elimu ya nadharia na vitendo kuliko elimu ya vitabu iliyozoeleka ambayo haina faida yoyote kwao.

Mustafa Kahangwa, mkulima na mfugaji wa kuku wa mayai kutoka Bukoba Vijijini, amesema ana kuku zaidi ya 500, hivyo ameshiriki mafunzo hayo kupata uelewa wa kufuga kwa njia za kisasa.

“Ninajitahidi kwenye kilimo na ufugaji ila changamoto ni vyakula vya mifugo na dawa, naiomba  Serikali  ipunguze  bei za pembejeo za kilimo na ufugaji ili tufuge  kwa tija.”

Mjasiriamali wa kuku na mayai, Irene Mwananugu ameshukuru kwa mafunzo hayo kwani alikuwa hajui kufuga kitaalamu lakini kupitia elimu hiyo anaamini atapata faida zaidi.

Kwa upande wake Dk Phidelis Malthine kutoka kampuni ya Silverlands amesema utafiti unaonyesha kuwa utumiaji wa dawa za  kuku kiholela unasababisha madhara  kwa binadamu na kuku ikiwamo kutengeneza usugu.