Waislamu kuliombea Taifa Ijumaa

Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir (wa pili kutoka kulia), akizungumza na waandishi wa habari leo Jumannde Desemba 12, 2023 ofisini kwake Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Bakwata yaandaa dua maalumu siku ya Ijumaa kwa ajili ya kuliombea Taifa na waathirika wa maafa ya maporomoko ya mawe, matope na magogo yaliyosababisha vifo vya watu 89 wilayani Katesh mkoani Manyara.

Dar es Salaam. Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir amewaagiza masheikh na maimamu nchini kufanya dua maalumu ya kumuomba Mungu aliepusha Taifa na maafa mbalimbali kama yaliyotokea wilayani Katesh mkoani Manyara.

 Maafa hayo yaliyosababisha vifo vya watu 89 hadi sasa yalitokea alfajiri ya Desemba, 2023 katika Mji Mdogo wa Katesh na vitongoji vya karibu vikiwemo vya Jorodom, Ganana, Katesh na Dumbeta pamoja na vijiji vya Gendabi na Sarijandu.

Chanzo cha maafa hayo ni kumeguka sehemu ya Mlima Hanang yenye miamba dhoofu iliyonyonya maji ya mvua, hivyo kupomoroko na kutengeneza tope lililokwenda katika makazi na maeneo ya biashara.

Katika janga hilo watu 139 walijeruhiwa kati yao 120 wameruhusiwa huku 17 wakiendelea na matibabu hospitalini.

Mufti Zubeir ametoa maagizo hayo leo Jumanne Desemba 12, 2023 wakati akizungumza na wanahabari kuhusu masuala mbalimbali yaliyojitokeza likiwemo la maafa ya Hanang, huku akitoa pole kwa waathirika wa tukio hilo.

“Suala hili litawahusu walimu wa madrasa na kila Muislamu kufanya dua. Tumuombe Mungu dua ya kutupa mvua nyepesi nyepesi na laini kama ambayo alivyokuwa akifanya Mtume Muhammad (S.a.w), ambapo kukiwa na ukame na watu wanataabika mvua, basi Mtume anamuomba Mungu ili kupata mvua nzuri yenye manufaa sio na madhara.

“Ikitokea mvua imeleta madhara basi anamuomba Mungu kuondosha madhara hayo na kuleta ahueni, nawaomba masheikh, maimamu, viongozi wa taasisi mbalimbali za Kiislamu wakiwa katika sehemu za ibada wamuombe Mungu atufanyie wepesi katika Taifa na kutuondolea majanga,” amesema Mufti Zubeir.

Sheikh Zubeir amewataka masheikh na maimamu, kufanya dua kila baada ya sala, kila Ijumaa kufanya dua kamili kwa ajili ya kumuomba Mungu.

Kutokana na hilo, Mufti Zubeir amesema Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), limeandaa dua maalumu baada ya sala ya Ijumaa itakayofanyika Msikiti wa Mohamed VI uliopo Kinondoni katika makao makuu ya baraza hilo.

“Tunatoa pole kwa Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na maafa hayo yaliyojitokeza, hawa ni wananchi wake tunampa pole sana jambo hili ni kubwa, Mungu ampe moyo wa subira. Pia tunawapa pole wafiwa na wale majeruhi walioko hospitalini,”amesema.