Waislamu wasisitizwa kuendeleza mema ya Mwezi wa Ramadan

Muktasari:

  •  Waislamu na wanajamii kwa ujumla wametakiwa kuutumia mwezi Mtukufu wa Ramadhani kubadili tabia kwa kutenda yaliyo mema na kuyaendeleza hata baada ya kumalizika mfungo.

  

Dar es Salaam. Waislamu na wanajamii kwa ujumla wametakiwa kuutumia mwezi Mtukufu wa Ramadhani kubadili tabia kwa kutenda yaliyo mema na kuyaendeleza hata baada ya kumalizika mfungo.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni GF Truck & Equipments LTD, Mehboob Karmali mara baada ya kufuturisha wadau mbalimbali na wafanyakazi wa kampuni hiyo.

Alisema mara nyingi mwezi huo umekuwa ukileta utulivu katika jamii, “Haijalishi ni kijana, mzee, Muislamu na asiyekuwa mwislamu, ilimradi wengi hutulia na kuuheshimu, hivyo ni vyema kuendeleza yale mema hata katika nyakati nyingine ili jamii iwe salama.

“Kipindi hiki pia ni vyema kuwapa wahitaji sadaka kwa kile kidogo tutakachojaaliwa kwa sababu tunazidiana,” alisema Karmali.

Kwa upande wa mgeni mualikwa katika Iftari hiyo, Sheikh wa Msikiti wa Khoja Shia Ishnashri Jamaat ya nchini Uingereza, Syed Ali Raza Rizvi aliwasihi Waislamu hususani vijana kudumisha amani na upendo baina yao.

Pia, alitumia fursa hiyo kuwashauri wafanyakazi wa kampuni hiyo kufanya kazi huku wakimtanguliza Mungu ili wanapofanya maamuzi yoyote yawe kwa faida ya kazi yao na Taifa kwa ujumla.

“Ukimtanguliza Mungu katika kila jambo lazima utafanikiwa, ila ukiwajali wengine na kuwahurumia utafanya maamuzi ya busara siku zote, hivyo tuyazingatie haya ili kufikia mafanikio tunayoyakusudia,”alisema Raza Rizvi.

Hii ni kawaida Kampuni ya GF Trucks & Equipemnts LTD, kujumuika na wafanyakazi wake na wadau katika matukio mbalimbali ikiwamo kufuturisha pamoja na kutoa misaada kwa yatima na wasiojiweza. Kampuni hiyo inajishungulisha na uuzaji wa magari makubwa (trucks)  na mitambo ya kutengenezea barabara.