Wajawazito wanaoendekeza ulevi hatarini kujifungua watoto njiti

Sababu za shinikizo la damu kwa wajawazito

Muktasari:

  • Watoto wanaozaliwa njiti wanatakiwa uangalizi mkubwa kwenye makuzi yao kwa sababu wana hatari ya kupata magonjwa ya moyo, figo ini na matatizo ya akili.

Dodoma. Wazazi wenye watoto waliozaliwa kabla ya miezi tisa wametahadharishwa kutotumia vileo ili kuwakinga watoto wao na magonjwa ya moyo, figo, ini na matatizo ya akili.

Aidha wazazi hao wametakiwa kutowapa watoto hao dawa yoyote bila ushauri wa daktari kwani dawa hizo japo zinatibu magonjwa kwa watu wengine kwa watoto hao zinaweza kusababisha matatizo.

Akizungumza na Mwananchi digital leo Oktoba 13 jijini hapa, Mhadhiri wa Chuo cha Afya Muhimbili (MUHAS), Profesa Fransis Furia amesema watoto njiti wako kwenye hatari kubwa ya kupata magonjwa hayo kutokana na viungo vyao kutokomaa wakati wanazaliwa.

Profesa Furia amesema watoto njiti wanatakiwa huduma bora za afya na uangalizi wa karibu kutoka kwa wazazi na jamii inayowazunguka kwa sababu huwa wanashambuliwa na magonjwa hayo wanapokuwa watu wazima kutokana na kukosa huduma bora wakati wa utoto.

"Watoto njiti wanapozaliwa viungo vyao vinakuwa havijakomaa, moyo unakuwa haujakomaa, maini yanakuwa hayajakomaa, figo zinakuwa hazijakomaa na ndiyo maana wanapokuwa wakubwa wanashambuliwa na magonjwa ya moyo, ini, figo na matatizo ya akili," amesema Profesa Furia.

Amewataka wazazi wanapokuwa wajawazito kujiepusha na vilevi na matumizi ya tumbaku kwa sababu huwa yanachangia watoto kuzaliwa kabla ya miezi tisa na hivyo kuwapelekea kupata changamoto hizo za kiafya.

Ameishauri Serikali na wadau kuwekeza rasilimali nyingi kwenye afya ya watoto njiti ili waweze kukua wakiwa na afya njema na kuwaepusha na magonjwa hayo.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Dk Eusebi Kessy amesema watoto wanaozaliwa njiti wanatakiwa kupewa Vitamin K kwa wingi ili kuimarisha viungo vyao ambavyo havijakomaa pamoja matibabu ya macho.

Amesema watoto njiti wapo kwenye hatari ya kupoteza maisha kwa sababu wakati wa kusubiri viungo vyao vikomae wanaweza kupata tatizo dogo linalodhoofisha afya zao.

Dk Kessy amesema huduma za watoto njiti zinatakiwa zitolewe na wataalamu wa afya wanaojua historia ya watoto hao ili wanapowahudumia wawape dawa ambazo hazitaleta madhara kwao pamoja na chakula bora.

Naye daktari wa watoto kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk Halima Kassim amesema hivi sasa Serikali imetoa vifaa vya kutosha kwa ajili ya watoto njiti kwenye hospitali na vituo vya afya.

Amesema hata huduma ya kuwapa watoto hao joto kwa njia ya kangaroo imesaidia kwa kiasi kikubwa kuokoa maisha yao tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.