Wakazi Bonde la Msimbazi walia fidia kiduchu, mmoja ashangaa kulipwa Sh1.2 mil

Muktasari:

  • Utata umeibuka katika uthamini wa majengo la wakazi wanaopisha utekelezaji wa mradi wa uendelezaji wa Bonde la Msimbazi.

Dar es Salaam. Utata umegubika uthamini wa nyumba za wakazi wanaopisha mradi wa uendelezaji wa Bonde la Msimbazi, wakisema fidia walizopangiwa kulipwa ni kinyume na thamani halisi ya nyumba hizo.

Kufanyika kwa uthamini huo, kunatokana na mpango wa Serikali wa kuendeleza bonde hilo unaofanyika kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia (WB).

Kampuni binafsi ya NORPLAN Limited ndiyo iliyopewa kazi na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kufanya uthaminishaji makazi ya wananchi hao na imeshalitekeleza hilo mapema mwaka huu.

Juzi, katika ukumbi wa DRIMP kampuni hiyo ilianza kutoa ripoti ya uthamini kwa wananchi hao, shughuli ambayo iliibua utata kwa miongoni mwa wakazi hao.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo, Machi 10, 2023 mmoja wa wananchi hao, Teresia Thadei amesema anashangaa nyumba yake yenye vyumba viwili anatakiwa kulipwa Sh1.2 milioni.

"Sasa nikilipwa kiasi hicho cha fedha nitafanya nini maana haitoshi hata kununua hata kiwanja mjini," amesema.

Matilda Kalumba amesema nyumba yake yenye ukubwa wa vyumba 12 anatakiwa kulipwa fidia ya Sh4 milioni kiasi ambacho amedai ni kidogo kulingana na thamani halisi ya nyumba hiyo.

Mwananchi mwingine, Kheri Said amesema kulingana na maelezo ya wathamini hao, uthamini haukuhusisha viwanja bali ni majengo pekee.

"Kama wamefanya uthamini wa majengo tupu ina maana hayakuwa kwenye ardhi? Hii inashangaza Sana," ameeleza.

Walipotafutwa kuzungumzia hilo, mmoja wa ofisa anayeshughulika na kazi hiyo, amesema saa 9:00 alasiri wanatarajia kutoa taarifa kuhusu kinachofanyika.