Wakulima kunufaika na huduma za ugani kiganjani

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Zaidi ya wakulima milioni 5 wanatarajia kunufaika na huduma za ugani kiganjani kufuatia Wizara ya Kilimo kuweka mfumo wa kupiga simu (huduma kwa wateja) na kupata ufafanuzi kuhusu huduma za kilimo na ugani.

Dodoma. Zaidi ya wakulima milioni 5 wanatarajia kunufaika na huduma za ugani kiganjani kufuatia Wizara ya Kilimo kuweka mfumo wa kupiga simu (huduma kwa wateja) na kupata ufafanuzi kuhusu huduma za kilimo na ugani.

Idadi hiyo ya wakulima inahusisha wakulima waliosajiliwa kwenye mfumo wa ‘mobile’ kilimo kuanzia mwezi Julai mwaka 2021.

Hata hivyo mfumo wa mobile kilimo ulionekana kuwa na changamoto kwa baadhi ya wakulima ambao hawana uwezo wa kumiliki simujanja na ambao wapo kwenye sehemu zenye mtandao hafifu kwa kushindwa kuwafikia maafisa ugani kwa ajili ya kupata ufafanuzi.

Akizungumza kuhusu mfumo huo, Mratibu wa mfumo wa Mobile kilimo Rajabu Mkalage amesema mfumo huo utasaidia kutatua changamoto ya ufinyu wa maafisa ugani waliopo 6986 waliosajiliwa ambao wanahitajika kuhudumia idadi kubwa ya wakulima hivyo kufanya ufinyu wa huduma za ugani.

Amesema idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kwa kuwa wapo baadhi ya wakulima ambao hawana simujanja watakaonufaika na mfumo huo ambao umehusisha huduma ambazo hazikupatikana kwenye mfumo wa mobile kilimo ambazo ni uuzaji wa pembejeo na masuala ya hali ya hewa kwa misimu tofauti.

"Kadri tunavyozidi kuimarisha huu mfumo ndio tunavyozidi kuondoa changamoto ambazo zinajitokeza kwa wakulima na wadau wote na kuwarahisishia upatikanaji wa huduma ambazo zilikuwa hazijawekewa utaratibu wa kupatikana kiurahisi"alisema

Mratibu wa mradi wa kilimo himilivu wa usalama wa chakula kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Mponda Malozo amesema tayari Shirika hilo limeandaa muongozo kwa maafisa ugani kutekeleza majukumu yao.

Naye mtaalamu wa hali ya hewa na uratibu wa mazao na tahadhari za chakula kutoka Wizara ya  Kilimo, Hidaya Senga amesema taarifa za hali ya hewa ni muhimu kwa wakulima kwa kuwasaidia kufahamu muda gani sahihi wa kupanda, kuvuna au kuweka mbolea ili kufanya kilimo chenye tija.

"Huu mfumo unatoa taarifa za hali ya hewa ambazo zitamsaidia mkulima namna gani ya kukabiliana nazo ili kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa"alisema.

Sabina Chiteto ni mkulima kutoka jijini Dodoma ambaye ameishukuru Serikali kwa kuwaletea mfumo huo ambao utawawezesha wakulima wote kupata huduma bila kubagua wasio na simujanja.

"Awali nilikuwa nausikia mfumo huo kwa wenzetu wenye simu za bei kubwa,,, lakini sasa hivi hata sisi wenye simu ndogo tutaweza kupata ufafanuzi kutoka kwa wataalamu kwa kupiga tu namba *152*00# na tunaweza kuhudumiwa"aliongeza