Walemavu walia kunyimwa ajira nchini

Baadhi ya vijana wenye ulemavu aina tofauti wanaoshiriki tamasha la vijana wenye ulemavu jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwajengea uwezo katika masuala ya uchechemuzi na tafiti. Picha Julieth Ngarabali

Muktasari:

  • Vijana wasomi wenye ulemavu nchini, wamepaza sauti zao wakidai kunyimwa fursa za ajira na kutoaminiwa japokuwa wana elimu na uwezo wa kufanya kazi hizo.

Dar es Saalam. Vijana wasomi wenye ulemavu nchini wametoa kilio chao cha kukosa nafasi za ajira huku wakiwa na sifa zote ikiwemo ya elimu katika nafasi mbalimbali nchini.

Hayo yamesemwa leo Aprili 18, 2023 jijini Dar es salaam na mmoja wa vijana wenye ulemavu (kiziwi), Daniel Ruben kwenye tamasha la vijana wenye ulemavu lililoandaliwa na shirika la kimataifa  linalotetea haki za watu wenye ulemavu la ‘ADD International’ tawi la Tanzania kwa lengo la kuwajenga uwezo katika masuala ya uchechemuzi na tafiti.

“Changamoto kubwa inayotukabili vijana wenye ulemavu hapa nchini ni ajira ambapo pamoja na wengi wetu kuhitimu fani mbalimbali katika ngazi ya stashahada na shahada bado kupata ajira imekua ni jambo gumu  kwasababu jamii na taasisi nyingi zinaona hatuwezi kazi, jambo ambalo sio kweli,”amesema.

Naye Dorice Mkiva ambaye ni mlemavu wa viungo amesema wamebaini vijana wengi wenye ulemavu wamekuwa wakiachwa nyuma kushiriki majukwaa yanayoweza kuwafanya waweze kupata stadi mbalimbali hususani za ajira na sasa wameamua kuwa mstari wa mbele kuyatumia.

"Hii inatupa changamoto vijana wenye ulemavu tukienda kushindana kwenye ajira wanakuwa wanashindwa kwa sababu hawana stadi zozote zile ambazo zitawawezesha wao kuweza kufanya vizuri katika usaili,” amesema Dorice

Mratibu wa miradi wa ADD International tawi la Tanzania, Elineca Ndowo amesema vijana wenye ulemavu kwa namna moja au nyingine hawajajumuishwa kwenye masuala ya uchechemuzi kwa kipindi kirefu au kwa kiasi kinachoitajika  huku wengi wakiwa ni wasomi na kupelekea kukutana na changamoto za ajira.

"Kwa hiyo ndio maana shirika la ‘ADD International’ tawi la Tanzania kwa kushirikiana na chuo kikuu cha Bournemouth cha Uingereza wakaandaa tamasha hili nchini kuwaleta vijana kufahamu masuala ya uchechemuzi na haki za watu wenye ulemavu na baadae watakua na vipindi vya mitandaoni vya kuwajengea uwezo na matumizi ya mtandao" amesema Ndowo

Mkurugenzi wa kitengo cha walemavu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu, Rashid Maftah amesema Serikali kupitia sheria ya watu wenye ulemavu Namba tisa ya mwaka 2010 imeelekeza kuendeleza haki na ustawi kwa kundi hilo wakiwemo vijana.

Amesema tayari Sh7 Bilioni zimeidhinishwa kutumika mwaka huu wa fedha  kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi na marekebisho ya watu wenye ulemavu na hiyo ni katika kuhakikisha vijana wote wenye ulemavu na wasio na ulemavu wanapata fursa ya elimu kwa sababu Serikali inaendeleza ile sera ya ujumuishwaji ili kuondokana na dhana ya unyanyapaa.

Hata hivyo, ripoti ya ‘Tanzania in figures 2021’ iliyotolewa na Ofisi nya Taifa ya Takwimu, inaonyesha kiwanmgo cha watu wasiokuwa na ajira nchini kinazidi kupungua kadri miaka inavyoenda.

“Mwaka 2017 kiwango cha wasio na ajira kilikuwa asilimia 9.9, mwaka 2018 kilikuwa asilimia 9.7, mwaka 2019 ilikuwa asilimia 9.6 huku mwaka 2020 kikifika asilimia 9.5 kabla ya kufika asilimia tisa mwaka 2021,” ilisema ripoti hiyo.