Waliotuhumiwa kukodi wauaji kwa Sh1 milioni kwa maelekezo ya mganga waachiwa huru

Muktasari:

  • Ilikuwa inadaiwa na upande wa mashitaka kuwa Oktoba 07, 2022 katika kijiji cha Mabibo wilaya ya Sikonge mkoani  Tabora, washtakiwa walidaiwa kumuua Kayeji kwa kumkatakata kwa mapanga maeneo mbalimbali ya mwili wakimtuhumu ni mchawi.

Tabora. Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, imewaachia huru watu watano, waliokuwa wanakabiliwa na shitaka la kumuua kwa makusudi, Bundala Kayeji (60) kwa maelekezo ya mganga wa jadi anayedaiwa kulipwa Sh1 milioni ili kukodi wauaji.

Ilikuwa inadaiwa na upande wa mashitaka kuwa Oktoba 07, 2022 katika kijiji cha Mabibo wilaya ya Sikonge mkoani  Tabora, washtakiwa walidaiwa kumuua Kayeji kwa kumkatakata kwa mapanga maeneo mbalimbali ya mwili wakimtuhumu ni mchawi.

Kwa kuegemea ushahidi wa mashahidi wa upande wa Jamhuri na maelezo ya onyo ya washtakiwa, upande wa mashitaka ulikuwa unamtuhumu mganga huyo kupiga ramli kuwa marehemu alikuwa amemtupia mapepo mwanaye yaliyomsumbua miaka 13.

Miongoni mwa washtakiwa hao ni Juma Ramadhan, mkwe wa marehemu na alikuwa mshtakiwa wa tatu  ambaye alikuwa amemuoa mtoto wa marehemu, Elizabeth Bundala na mke wa zamani wa marehemu, Katarina Lucas aliyekuwa mshtakiwa wa nne.

Washtakiwa wengine walioachiwa huru ni pamoja na Juma Ramadhan na Katarina Lucas, ni Seni Nhungu aliyekuwa mshtakiwa wa kwanza, Jilala Tosogoro aliyekuwa mshtakiwa wa pili, na Daniel Fredrick ambaye alikuwa mshtakiwa wa tano katika kesi hiyo.

Hata hivyo, katika hukumu aliyoitoa Aprili 22,2024, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Tabora, Dk Mwajuma Kadilu, ambaye alisema upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha shitaka dhidi ya washtakiwa na kuacha mashaka makubwa.

Jaji alisema ushahidi wa mashahidi tisa wa upande wa mashitaka ulikuwa hautoshelezi na hauaminiki kuwatia hatiani washtakiwa kwa kosa zito la mauaji ya kukusudia, ambapo kwa mujibu wa kifungu 196 na 197 cha kanuni ya adhabu, adhabu yake ni kifo.

Kulingana na Jaji Kadilu, baada ya kuchambua ushahidi wote kwa ujumla wake, mahakama imeona kuwa kuna dosari kubwa na kupishana kwa ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri, huku akihoji sababu za kutokamatwa kwa mganga wa jadi aliyetajwa.

Jaji alitolea mfano kuwa shahidi wa sita aliyekuwa ni Polisi aliyepeleleza kesi hiyo, alieleza kuwa malipo ya awali ya Sh200,000 kama malipo ya kufanya mauaji hayo yalifanyika kwa njia ya muamala wa simu, lakini hakupeleleza ni simu gani ilipokea fedha hizo.

Kulingana na Jaji, kulikuwa pia na kupishana kwa mashahidi kuhusu malipo hayo ya awali kwa waliodaiwa kukodiwa kufanya mauaji,  huku baadhi wakisema mshtakiwa wa kwanza na wa pili walilipwa Sh200,000 na wengine Sh250,000.

“Mashahidi walipishana katika masuala ya msingi kama sababu za kifo, ushiriki wa washtakiwa na mazingira mazima ya mauaji hayo. Lakini kulikuwa na ukiukwaji wa kanuni. Mfano ni kushindwa kuandaa gwaride la utambuzi,” alieleza Jaji Kadilu.

Jaji alisema hayo pamoja na mapungufu katika ushahidi wa upande wa mashtaka kunatia mashaka kuhusu kuaminika kwa ushahidi uliowasilishwa na Jamhuri.

“Mbali na hilo, lakini upande wa utetezi uliibua mashaka kuhusiana na kukubaliwa kwa maelezo ya onyo ya washtakiwa na kushindwa kwa upande wa mashitaka kuwaita baadhi ya mashahidi muhimu wanaotajwa,” alisema Jaji Kadilu.

Jaji alisema kwa kuzingatia kanuni ya shitaka kuthibitishwa pasipo kuacha mashaka, anaona upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha shitaka la mauaji ya kukusudia, hivyo anawaachia huru washtakiwa wote kutokana na kukosekana kwa ushahidi.

Ushahidi wa Jamhuri ulivyokuwa

Ushahidi wa upande wa Jamhuri ulikuwa unaeleza kuwa mshtakiwa wa tatu, Juma Ramadhan, alikuwa amemuoa mtoto wa marehemu aitwaye Elizabeth Bundala ambaye alikuwa akisumbuliwa na mapepo wabaya

kwa takribani miaka 13 mfululizo.

Kwa kuongezea, ushahidi wa upande wa mashitaka ukaeleza kuwa marehemu alikuwa amemuoa mshtakiwa wa nne, Katarina Lucas lakini alimuacha na kuoa mwingine.

Ilielezwa kuwa mshtakiwa huyo wa tatu, alikwenda kwa mganga wa jadi ambaye hata hivyo hakuwahi kukamatwa wala kuhojiwa na polisi, ambaye baada ya kupiga ramli yake ya kiganga, alimweleza kuwa mkewe alikuwa analogwa na baba yake mzazi.

Mganga huyo alidaiwa kumshauri mshtakiwa wa tatu ambaye ni mume wa mtoto wa marehemu kuhakikisha baba mkwe wake anauawa, ambapo mganga huyo alimweleza anahitaji Sh1,050,000 ili kukodi wauaji.

Baada ya kutoka kwa mganga, ushahidi ulikuwa unamtuhumu mshtakiwa wa tatu kwamba alipofika nyumbani aliitisha kikao cha familia kilichohudhuriwa na yeye mwenyewe, mama mkwe (mshtakiwa wa nne) na mkewe, Elizabeth ambaye ni mtoto wa marehemu.

Kikao hicho kilikuwa mahususi kuchangisha fedha kwa ajili ya mauaji ya Bundala Kayeji na walikubaliana kuuza ng’ombe wanne ili kupata Sh1,050,000 ambapo mganga alimsaidia mshtakiwa wa tatu na wa nne ili kuwakodisha mshtakiwa wa kwanza na wa pili.

Mshtakiwa wa kwanza, Seni Nhungu ni mdogo wa mganga huyo na kulingana na ushahidi wa Jamhuri, mshtakiwa wa tano, Daniel Fredrick ndiye aliyedaiwa kuwapeleka mshtakiwa wa kwanza na wa pili nyumbani kwa marehemu na kumuua kwa mapanga.

Washtakiwa wote walikanusha mashitaka hayo huku wote wakilalamika kukamatwa na polisi kwa siku tofauti na kupelekwa kituo cha polisi, ambako huko ziliandaliwa karatasi zenye maelezo wasiyoyajua na kuwatesa ili wakubali kuweka saini zao.