Wanafunzi Hanang wajengewa miundombinu kudhibiti magonjwa ya milipuko

Baadhi ya wanafunzi wa Wilayani Hanang' mkoani Manyara, walionufaika na miundombinu hiyo wakinawa mikono. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Kufuatia mafuriko wilayani humo, makazi ya watu na miundombinu mbalimbali iliharibiwa ikiwemo vyoo shuleni na chanzo cha maji, jambo ambalo liliwaweka hatarini kupata magonjwa ya mlipuko wakati wa wilaya hiyo.

Hanang. Wanafunzi 3,000 wa shule za msingi na sekondari Wilaya ya Hanang mkoani Manyara, wamejengewa miundombinu ya usafi ili kudhibiti magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.

Hali hiyo imetokana na tukio la Desemba 3, 2023 ambapo wilaya hiyo ilikumbwa na maporomoko ya tope, magogo na miti yaliyotokea Mlima Hanang' na kusababisha vifo vya watu 89 na wengine kujeruhiwa.

Katika mafuriko hayo, makazi ya watu na miundombinu mbalimbali iliharibiwa ikiwemo vyoo shuleni na chanzo cha maji, jambo ambalo liliwaweka hatarini kupata magonjwa ya mlipuko wakati wa wilaya hiyo.

Ili kudhibiti magonjwa ya milipuko ikiwemo kipindupindu na homa ya matumbo kwa wanafunzi, Shirika la Amref Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Marekani la Kudhibiti Magonjwa (CDC), wamezindua maeneo ya kunawa mikono na kukarabati vyoo.

Mkurugenzi Mkazi wa Amref Tanzania, Dk Florence Temu, amesisiza umuhimu wa mbinu jumuishi za kuimarisha magonjwa ya mlipuko katika jamii kupitia

ufuatliaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira.

Amesema maendeleo makubwa yamepatikana katika ufuatiliaji wa mapema na kukabiliana na vitisho vya afya ya umma katika kanda hiyo hasa magonjwa ya mlipuko,

Dk Temu amesema ushirikiano kati ya Amref Tanzania na Kituo cha serikali ya Marekani (CDC Tanzania), umekuwa na mchango mkubwa katika kutoa ushauri na uhamasishaji katika uboreshaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira, hivyo kusababisha kuzuia magonjwa ya kuambukiza katika kanda hiyo.

Kwa upande wake, mkuu wa usalama na udhibiti wa uchafuzi wa mazingira Wizara ya Afya, Dk Honestus Anicetus,  amewapongeza CDC Tanzania na Amref Tanzania kwa juhudi zao za

kuunga mkono Serikali katika kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa mazingira.

Dk Anicetus amesema Serikali imeboresha sekta ya afya kupitia miradi mbalimbali ya afya nchini,  kwa uwajibikaji wa utunzaji wa maeneo hayo na amesisitiza haja ya kuchukuliwa hatua za kisheria kwa yeyote atakayesababisha uharibifu au uzembe.

Mkurugenzi wa Kitengo cha ulinzi wa afya, katika kituo cha serikali ya Marekani cha kudhibiti na kuzuia magonjwa (CDC) Tanzania, Dk Wangeci Gatei, amesema dhamira ya CDC Tanzania kuimarisha mbinu za kuzuia maambukizi ya magonjwa ya mlipuko Tanzania kupitia juhudi za ushirikiano na Serikali na washirika wa ndani.

Mwanafunzi wa shule ya msingi Jorodom, Magdalena Richard,  amewashukuru wadau hao wa maendeleo kwa kusaidia kukarabati vyoo na kuweka miundombinu ya kunawia katika shule yake.

“Bado tupo kwenye kumbukumbu mbaya ya maafa ya mwaka jana ambayo pia yalichukua maisha ya baadhi ya wanafunzi wenzetu, tunashukuru kwa kuwekewa miundombinu hii,” amesema.