Wanafunzi wenye changamoto za kifedha kupata ahueni DarTu

Makamu Mkuu wa DarTu (zamani Tudarco), Profesa Burton Mwamila akizungumza na waandishi wa habari

Muktasari:

  • Mfuko huo utasaidia wanafunzi wasio na uwezo wa kifedha kutimiza malengo yao ya kitaaluma, chuo hicho chapanda hadhi na kuwa chuo kamili

Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (DarTu) kipo mbioni kuzindua mfuko wa ufadhili kwa wanafunzi wasio na uwezo wa kuhimili gharama mbalimbali za masomo ya elimu ya juu.

Hayo yamezungumzwa leo Jumatano Aprili 17, 2024 na Makamu Mkuu wa DarTu (zamani Tudarco), Profesa Burton Mwamila akizungumza na waandishi wa habari chuoni hapo kuhusu kupandishwa hadhi kwa taasisi hiyo na kuwa chuo kamili.

“Kutokana na baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu kusitisha masomo kwa sababu za ugumu wa maisha unaopelekea kukose ada, chuo chetu kipo mbioni kuzindua mfuko wa ufadhili kwa wanafunzi wasio na uwezo  utaoitwa (Students Scholarship Endowment Fund –SSEF),”amesema Profesa Mwamila.

Profesa Mwamila ameongeza kuwa mfuko huo utasaidia wanafunzi wasio na uwezo wa kifedha kutimiza malengo yao katika elimu.

“Sherehe za uzinduzi wa chuo pamoja na mfuko wa kusaidia wanafunzi wasio na uwezo zitafanyika Aprili 19, 2024 kuanzia saa tatu asubuhi chuoni hapa na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi,”amesema Profesa Mwamila.

Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Andrew Mollel amesema siku ya kesho Aprili 18, 2024 skuli ya Sheria na Haki chuoni hapo itaendesha Mahakama igizi (moot court) ikiwa ni njia ya kuipamba siku hiyo.

 “Kama nilivyoeleza siku ya Alhamisi kuna hayo mawili lakini sasa nazungumzia tukio la pili ambalo ni mahakama igizi, mahakama igizi inahusu kuigilizwa kikamilifu yale mambo yanafanyika mahakama za kawaida lakini ni sehemu ya mafunzo ya wanafunzi wanaosoma shahada ya sheria na hata shahada ya pili, wanaonesha umahiri wao kwa walichojifunza sasa kuyaweka kwenye vitendo,”amesema Profesa Mollel

Awali chuo hicho kinachomilikiwa na Dayosisi ya Mashariki na Pwani Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)  kilikuwa Chuo Kikuu Kishiriki kikiwa chini ya usimamizi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira kilichopo Arusha .