Wananchi Ulanga wapatiwa gari la wagonjwa

Morogoro. Licha ya Serikali kuendelea kuboresha na kuongeza majengo ya kisasa katika Hospitali ya wilaya ya Ulanga, bado hospitali hiyo haikidhi mahitaji kulingana na ongezeka la watu ambao baadhi yao wamekuwa wakilazimika kwenda hospitali ya St Francis Ifakara kufuata huduma.

Hospitali hiyo ni miongoni mwa hospitali kongwe nchini, imenzishwa mwaka 1905 kabla ya uhuru wa Tanzania.

Kufuatia hivyo Mbunge wa Ulanga, Salim Hashim Juni 12, 2023 ametoa gari la kubebea wagonjwa lenye thamani ya Sh120 milioni, ametoa gari hilo mbele ya makamu mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Rehema Sombi walipotembelea hospitali hiyo na kufanya usafi.

Hasham amesema gari hilo pia litatumika na wananchi wa Ulanga kusaidia pindi watakapopata misiba ndani na nje ya jimbo hilo kuweza kusafirisha na kuongeza kuwa kama wilaya imepokea Sh3 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na ukarabati kwa vituo vilivyochakaa.

“Hapa kwetu tuna hospitali ya wilaya lakini naweza kuifananisha na kituo cha afya kwa sa babu watu wameongezeka na huduma ya afya imekuwa mbaya,hapa mjini tulipata fedha ya kujengwa Kituo cha Afya Mahenge mjini lakini nilikata ili kiende kikajengwe kule Ilagua kwa sasa wananchi wa kule wanatoka mbali kuja kupata huduma wilayani,”amesema.

“Kilio chetu hapa mjini ni kupata hospitali mpya ya wilaya kwani ongezeko la watu wengi, hospitali ni chakavu, hata ikiboreshwa bado itaendelea kuwa ndogo na ardhi haitosherezi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora,” amesema

Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Dk Stephano Liwemba amesema baadhi ya huduma za kitabibu hushindwa kufanyika hospitalini hapo na wagonjwa kulazimika kupelekewa Hospitali ya St Francis Ifakara kwa matibabu zaidi.

Dk Liwemba ambaye hakutaja moja kwa moja magonjwa yanayowalazimu watu kwenda kutibiwa Ifakara.mbali na kuishukuru serikali kwa uboreshaji wa huduma za afya wilayani humo, amesema bado wanauhitaji wa jengo la maabara.

Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Rehema Sombi ameeleza namna Wizara ya Afya inavyoendelea kuboresha sekta ya afya kwenye maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa vifaa tiba na kuongeza majengo ya kutolea huduma kwa wananchi.


Sombi amepongeza juhudi za serikali ambayo imefanikisha kupatikana kwa mashine ya x-ray hospitalini hapo.

Wakati huo Hashim ametoa simu janja 63 na kadi za bima ya afya 63 kwa viongozi wa CCM wa kata 21 za wilaya ya Ulanga kwa nia ya viongozi hao kuwasiliana na kutoa taarifa wakati wote panapotokea changamoto za wananchi.

UVCCM wilaya ya Ulanga iliandaa hafla ya kumpongeza Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa namna ilivyoipatia wilaya hiyo fedha za Miradi ya maendeleo ambapo katika hafla hiyo ilifanya zoezi la usafi na upandaji miti hospitalini hapo.