Wanasayansi kujadili utafiti wa Tanzania virutubisho kinga mwili

Mhadhiri mbobezi kwenye kinga ya mwili na lishe kutoka chuo Kikuu Kishiriki cha Kikristo cha Tiba, Kilimanjaro (KCMUCo), Dk Godfrey Temba Akizungumza leo katika kongamano la kwanza la Kimataifa la Sayansi ambalo linafanyika mkoani  Kilimanjaro kwa mara ya kwanza. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Miongoni mwa mawasilisho 16 ya tafiti zilizofanywa na Chuo Kikuu Kishiriki cha Kikristo cha Tiba, Kilimanjaro (KCMUCo) ni utafiti ambao uliangazia suala la kuhusika kwa lishe katika kuboresha kinga ya mwili na kuongeza uwezo wa mwili kupambana na magonjwa ya kuambukiza na yale yasiyoambukiza.

Hai. Wanasayansi kutoka mataifa zaidi ya sita duniani wamekutana mkoani Kilimanjaro kujadili tafiti mbalimbali za kisayansi ambazo zimekuwa zikifanywa na watafiti kutoka chuo kikuu kishiriki cha Kikristo cha Tiba, Kilimanjaro (KCMUCo) ili kuona ni namna gani ya kukabiliana na magonjwa yanayoambukiza na yale yasiyoambukiza.

 Miongoni mwa mawasilisho ya tafiti zilizofanywa na chuo hicho ni utafiti ambao uliangazia suala la kuhusika kwa  lishe katika kuboresha kinga ya mwili na kupelekea uwezo wa mwili kupambana na magonjwa ya kuambukiza na yale yasiyoambukiza.

Akizungumza leo katika kongamano la kwanza la Kimataifa la Sayansi ambalo linafanyika mkoani hapa, Mhadhiri mbobezi kwenye kinga ya mwili na lishe kutoka chuo hicho, Dk Godfrey Temba amesema kupitia kongamano hilo watawasilisha machapisho zaidi ya 16 yanayohusu tafiti mbalimbali za kisayansi ambazo zimefanywa na chuo hicho.

"Kongamano hili limekuja wakati mwafaka kwa sababu kipindi cha miaka michache huko nyuma tumeona jinsi janga la Uviko 19 namna ilivyoikumba dunia na nchi yetu, kinga ya mwili ni mfumo wa mwili ambao unachukua nafasi kubwa katika kupambana na magonjwa yote ya kiwa ya kuambukiza na yale ambayo siyo ya kuambukiza," amesema.

"Hii ni kama sehemu ya chuo kuweza kushirikisha matokeo ya tafiti za kisayansi ambazo zimekuwa zikifanywa na watafiti katika chuo chetu, katika mwaka huu tumekuwa na mada ambayo  inayozungumzia ushiriki wa kinga ya mwili katika kupambana na magonjwa ya kuambukiza na yale ambayo sio ya kuambukiza,” amesema.

"Uwepo wa kinga imara ya mwili ni uthibitisho wa mwili wa binadamu kuweza kupambana na magonjwa haya, kwa hiyo katika kuanzisha kongamano hili chuo kikafikiri ni wakati sahihi kuweza kuwakutanisha wanasayansi waliopo ndani ya nchi na wanasayansi waliopo nje ya nchi," amesema.

Amesema wataendelea  kufanya makongamano ya kisayansi kila mwaka ili kuweza kuwasilisha machapisho mbalimbali ya kitafiti ya kisayansi yanayofanywa na chuo hicho ikiwashirikisha washiriki wa ndani na nje ya nchi.

"Lengo kubwa ni kwamba kama chuo chochote kikuu nchini kazi yake kubwa ni kufundisha, kufanya tafiti lakini kuweza kutoa ushauri wa kitaalamu katika jamii, hii ni moja ya sehemu ya chuo kutekeleza jukumu lake la kufanya tafiti na baada ya kufanya tafiti kuweza kuepeleka machapisho na majibu ya tafiti katika jamii," amesema.

"Utafiti ambao umefanywa na KCMC ikishirikiana na washirika wake wa nje wa Mataifa mengine ambapo tumebaini kwamba lishe zetu za asili ambazo kwa kaisi kikubwa zimesahaulika katika jamii zetu zinao mchango mkubwa wa kuimarisha kinga za mwili na kuifanya iweze kupambana na magonjwa mbalimbali kwa kiasi kikubwa," amesema.

"Tumeona wale wenzetu wanaoishi maeneo ya vijijini ambao bado wanaendelea kutumia lishe zao za asili kinga zao za mwili zimekuwa na uwezo mkubwa wa kupambana na magonjwa ukilinganishwa na sisi ambao tunaishi mijini ambao kwa kiasi kikubwa tumeacha lishe zetu za asili," amesema.

Mkuu wa chuo hicho, Profesa Efatha Kaaya amesema matokeo ya tafiti zinazofanywa na chuo hicho yataweza kutatua matatizo na changamoto zilizopo katika jamii na kuleta suluhu ya kudumu katika Taifa.

"Zipo tafiti nyingi zinafanyika lakini tunakosa zile njia ya kuzipeleka kwa jamii lakini mojawapo ya njia hizo ni sisi wenyewe tunatoa hizi tafiti kuhakikisha tunaweka mikakati ya kuzipeleka kwa jamii, kwa mfano kongamano kama hili hili ni la kimataifa maana yake sio Tanzania," amesema.

"Serikali iweke mazingira mazuri ya kufanya tafiti na pale ambapo inaweza kuwekeza nguvu kubwa ili tafiti ziweze kufanyika lakini kuzipeleka kwa walengwa, lakini sisi wenyewe watafiti tuwe na njia mwafaka ambapo kila anayelengwa ataweza kuelewa ili ilete mafanikio," amesema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya KCMC, Askofu Fredrick Shoo amesema pamoja na tafiti zinazofanywa na baadhi ya vyuo vikuu hapa nchini ipo haja ya serikali kuwekeza nguvu kubwa ya  rasilimali fedha kwani tafiti zinahitaji gharama kubwa.

Amesema ipo haja ya serikali kuanzisha mfuko wa pamoja wa kusaidia vyuo vikuu vyote hapa nchini ili kuweza kufanya tafiti mbalimbali ili kujibu na kutatua changamoto zinazowakabili Watanzania.