Wanawake wakodi 'waume’ wa kuwasindikiza kliniki

Dar es Salaam. Utaratibu unaowataka wajawazito kuambatana na wenza wao kila wanapokwenda kliniki, umelazimisha baadhi yao kukodi watu wa kwenda nao ili kuepuka kuchelewa kupata huduma wanazokusudia.

Utaratibu huo umekuwa ukifanyika hasa katika zahanati, vituo vya afya au hospitali za umma kuhamasisha wanaume wawasindikize wake zao kliniki ili kuboresha afya ya mama na mtoto.

Katika kufanikisha hilo, kila mjamzito anayefika akiwa na mumewe hupewa kipaumbele na kuhudumia kabla ya wengine.

Hata hivyo, imebainika kuwa wanaume wengi bado hawajawa tayari kuwasindikiza wake zao kliniki kutokana na sababu mbalimbali, hali inayowalazimu wake zao kutafuta njia mbadala ili wawahi kupata huduma na wakati mwingine kuepuka maswali.

Hayo yamebainika katika hospitali, vituo vya afya na zahanati ambazo Mwananchi imezitembelea jijini Dar es Salaam huku baadhi ya wajawazito wakieleza usumbufu wanaokumbana nao.

Akisimulia hali hiyo, Khadija Juma mkazi wa Buguruni anasema “mume wangu alinileta mara moja tu siku ya kwanza ya kliniki, tuliporudi nyumbani aliniambia nitakuwa naenda mwenyewe.”

“Aliniambia ‘siwezi kwenda kujichoresha kwenye wanawake wengi’,” anasimulia.
Awali, Khadija anasema alipogundua ni mjamzito walikubaliana na mumewe kuanza kliniki na walipanga kituo cha afya cha kuanzia, ili kumpa nafasi mumewe kuwahi kwenye shughuli zake jirani na kituo hicho.

Siku hiyo, Khadija anasema wakiwa moja na mumewe walifika kliniki saa 1 asubuhi wakisubiri huduma kwa kuwa ilikuwa ni siku yao ya kwanza, walichukua namba na kusubiri utaratibu mwingine.

“Kulikuwa na foleni hiyo siku nilipata namba 10, wapo tuliowakuta tangu saa 12 asubuhi, hivyo hatukuona shida ila mle ndani tulikaa hadi saa sita mchana, ndipo mume wangu aliniambia hatakanyaga tena, hawezi kupoteza muda wake,” anasema Khadija.

Anasema licha ya kupewa kipaumbele kwa waliofika na wenza wao, mzunguko hadi kukamilisha huduma ulichukua muda.
Baada ya mume kukataa kwenda, Khadija alimwambia atakuwa anapelekwa na shemeji yake.

“Shemeji nilikuja naye siku moja kwa sababu ya ukuaji wa tumbo sikuwa tayari kuchunguliwa na shemeji yangu,” anasema Khadija.

Simulizi ya Khadija inafanana na ya Tausi Mohamed aliyekutwa katika kituo cha afya kilichopo katika Wilaya ya Ilala, kuwa katika siku ambazo mume wake hana nafasi, hulazimika kwenda na shemeji yake.

Hata Happyness Shayo, mkazi wa Mbagala aliyekutwa katika kituo kimoja cha afya kilichopo katika Wilaya ya Temeke, aliyesema mwenza wake hataki kufika kliniki kwa kuhofia kupimwa Virusi vya Ukimwi (VVU), akidai hajajiandaa kupokea majibu.
Anasema akipima yeye (mwanamke) ni sawa na wamepima wote.

Happyness anasema kutokana na kauli hiyo ameamua kuchukua pesa kwa mumewe ili kumlipa mtu atakayemsindikiza kliniki kwa kuwa wanapewa kipaumbele katika huduma.

“Najua kabisa leo nakuja kliniki, nampanga rafiki yangu mmoja anaendesha pikipiki, hata leo (wiki iliyopita) nimekuja naye baada ya kuingia kupata huduma ya awali, nimemruhusu aende maana panaposumbua ni kuingia humo ndani,” anasema.
Anasema utaratibu huo unawaumiza wale waliowahi mapema ambao wanajikuta wanakaa muda mrefu wakipisha watu waliokwenda na wenza wao, hivyo wanaamua ‘kukodi’ watu.

“Ukijua unafika kliniki huna mwenza unamchukua mtu, tunawalipa Sh10,000, kwa hiyo nina bajeti ya kumpa mtu kila nikija kliniki. Tukiingia ndani hakuna anayejua kama si mtu wangu, hapa hospitali kuna maigizo zaidi ya kwenye tv,” anasema.
 

Sababu kukacha kliniki

Baadhi ya wanaume wanasema hawawapeleki wake zao kliniki kutokana na kauli za watoa huduma kuwasema vibaya wajawazito wanaofika bila wenza wao.

“Tulipewa nafasi tuliokuwa na wake zetu, lakini maneno ambayo walikuwa wanawasema wasiokuwa na wenza yalikuwa yananiumiza, hivyo sikuona sababu ya kumpeleka tena mke wangu,” anasema Khalid Kisaka, mkazi wa Mbezi.
Kwa upande wake Aboubakar Njovu, alisema hawezi kumpeleka mwenza wake kliniki kutokana na kuwa na wanawake tofauti.

“Napata wapi nguvu, mimi sijatulia ni vigumu kwenye hilo, huwezijua unafika huko watu wanamfahamu mwanamke uliye naye na taarifa zinafika kwa muhusika,” alisema Njovu na kuongeza kwa kufanya hivyo anaepukana na mambo mengi ambayo amefanya sirini ili kuinusuru ndoa yake.
 

Ushuhuda wa wanaume

Baadhi ya wanaume wanaokodiwa kusindikiza wajawazito kliniki wameeleza uzoefu wao, akiwamo Emmanuel Isaya aliyesema hulipwa kati ya Sh10,000 hadi Sh15,000 kufanya kazi hiyo.

"Wapo ambao huhitaji mtu kwa siku ya kwanza tu kwa ajili ya kupima virusi vya Ukimwi na baada ya hapo anaendelea mwenyewe lakini wengine wanaletwa na waume zao,” anasema Isaya.

Kijana huyo alisema wapo ambao hupewa na maelekezo wenza wa wajawazito hao wakiwemo ambao huwatumia wafanyakazi au madereva wao kuwasindikiza wake zao.
“Jina na umri vinatumika vya mume wa mjauzito na anakuwa makini kwenye kukariri jina na umri ili usichanganye,” anasema.

Said Zuberi, mkazi wa Kawe anasema alishawahi kuombwa na rafiki yake wa kike ampeleke kliniki baada ya kugombana na mwenza wake na alifanya hivyo.
"Alinipigia simu kuniomba, tukaenda hospitali moja ipo maeneo ya Mwenge, kipindi kile ukipima majibu unafuata kesho yake," anasema Zuberi.

Mkazi mwingine wa Mwenge, Ibrahim Frank anasema kwake ilikuwa changamoto kumpeleke mkewe, “kule unakwenda kupimwa Ukimwi na mimi siko tayari. Akipimwa mke wangu ndio majibu yangu, kwa hiyo si kazi rahisi sana kwenda kupimwa na hiki ndicho kinaniogopesha.”
 

Kwa nini waende na wenza?

Hata hivyo kwa mujibu wa watoa huduma, mume ni muhimu apimwe afya ikiwemo magonjwa ya zinaa na VVU ili ikiwa baba ana maambukizi na mama hana, wajue mapema namna ya kumlinda mtoto.

Mhudumu wa kituo cha afya kilichopo Tabata aliyeomba kutotajwa jina lake gazetini, alisema wamekuwa wakitoa elimu kwa wajawazito wanaokwenda kliniki kuhusu umuhimu wa kwenda na wenza wao halisi na si wa kuokota barabarani kwa kuwa kuna hali ya hatari ambayo inaweza kutokea muda wowote kwa mjamzito.

"Tunataka waje na wenza wao ili tukitoa elimu anajua cha kufanya, anapokuja mtu feki siku linatokea jambo la hatari, ukimuuliza muhusika atajibu hajui chochote wakati kwenye kadi tunaona alikuja na mwenza wake," anasema.
Mhudumu wa kituo cha afya cha Mbagala aliyejitambulisha kwa jina moja la Sara, anasema wanaokwenda na watu wengine wanakosea na Serikali inapokea takwimu za uongo.

"Kuna mtu aliwahi kuja na mwenza feki, tukawapima HIV mwanaume alikutwa nao, sasa tukaona mtu kapaniki na kukimbia. Tunamuuliza mwanamke vipi mwenza wake amekimbia, ndipo alisema si mwenza wake bali amemtoa nje ya kituo," alisema Sara.
Anasema siku hizi wanawake hawana aibu akitaka jambo lake liende, maana wapo wanaotoa nguo mbele ya mtu aliyemkodi na anakwambia ni mwenza wake, hivyo ni ngumu kutofautisha.

"Tuliamua kufanya vipimo huku wenza wao wakiwa wanaona na kama atakuwa wa kukodi atakuwa na aibu, lakini huku hakuna hayo, anakuja na mtu baki na anavua nguo mbele yake," anasema.

Akitoa mfano, anasema yupo aliyekwenda na shemeji yake alipopanda kitandani wakaona anahangaika kujificha ndipo walipomuuliza anaogopa nini wakati yupo na mwenza wake ambaye wanashirikiana kimwili.
 

Vituo binafsi

Uchunguzi uliofanyika katika kliniki binafsi ulibaini hali tofauti, kwani huku wanafuata utaratibu wa namba ambapo kila mtu aliyekwenda na mwenza wake watafuata utaratibu uliopo wa foleni.


Imeandaliwa na kushirikiana na Bill & Melinda Gates.