Wasomi wachambua ripoti ya CAG, wainanga Takukuru

Wasomi wachambua ripoti ya CAG, wainanga Takukuru

Muktasari:

  • Baada ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere kubainisha kwamba kampuni ya Ndege nchini (ATCL) imepata hasara ya Sh60 bilioni mwaka 2019/20, baadhi ya wasomi wamelitetea shirika hilo huku wakilitaka kujipanga zaidi.


Dar es Salaam. Baada ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere kubainisha kwamba kampuni ya Ndege nchini (ATCL) imepata hasara ya Sh60 bilioni mwaka 2019/20, baadhi ya wasomi wamelitetea shirika hilo huku wakilitaka kujipanga zaidi.

Pia, wasomi hao wamechambua maagizo mbalimbali yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwamo kumwagiza CAG kukagua fedha zilizotoka Benki Kuu kati ya Januari na Machi, kuunganisha mifumo ya ukusanyaji mapato na Taasisi ya Kuzui na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuacha kukusanya madeni bali wajielekeze kwenye kazi zao za msingi.

Mhadhiri wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Profesa Humphrey Moshi alisema hasara ambayo ATCL wanaipata imetokana na kuyumba kwa soko kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19.

Pia, alisema bado shirika hilo halijaanza kufanya safari za masafa marefu kwenda nchi za Ulaya kama Uingereza na Asia. Alisema safari za ndege za ATCL kwenda Guangzou, China zilitakiwa kuanza lakini zikakwama kutokana na Covid-19.

“Kupata hasara ni jambo la kawaida, hata mashirika makubwa yanapata hasara, jambo la muhimu ni kuanza kwenda safari za masafa marefu. Kwa hiyo, hasara hiyo siyo suala la kiutendaji, ni suala la soko,” alisema.

Wasomi wachambua ripoti ya CAG, wainanga Takukuru

Profesa Moshi alisema bado kuna umuhimu wa kuwekeza kwenye shirika hilo, ili kuliwezesha kutoa huduma hasa katika mataifa yanayoleta watalii wengi hapa nchini. Alisema shirika imara la ndege ndilo litachochea kasi ya watalii hapa nchini.

Mifumo ya malipo serikalini

Ingawa Serikali ilianza kutumia mfumo wa malipo ya kielektroniki (GePG) tangu mwaka 2017 ambao unakusanya mapato mengi ya umma kidijitali, Samia alisema kuna zaidi ya mifumo sita inayotumika hivi sasa.

Rais alisema hayo baada ya Kichere kueleza kuwa mifumo tofauti ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) inayotumika nchini haiwasiliani na mingine usalama wake si wa uhakika hali inayoweza kusababisha upotevu wa mapato.

Alipotafutwa kwa ufafanuzi jana, Kichere alisema ni kweli mifumo ipo mingi na GePG inatumika kama lango la kuingilia kwenye hiyo mifumo.

Mwananchi lilipotaka ufafanuzi, Kichere alisema “subiri siku nafanya kikao na waandishi wa habari kuhusu taarifa ya CAG ambayo niliiwasilisha jana kwa mheshimiwa Rais.”

Hata hivyo, Dk Severine Kessy wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) aliyefanya utafiti wa malipo ya kielektroniki na ukusanyaji mapato kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa na kuchapishwa mwaka 2019, alibainisha baadhi ya changamoto.

“Ingawa kila anayetaka kulipa serikalini anapewa ‘control number,’ bado anaweza kuchagua kulipia kwa kutumia simu ya mkononi au akaenda benki. Wengine wanatumia vituo vya huduma (PoS), internet banking (huduma za benki kwa intaneti) au manually (kupewa risiti iliyojazwa kwa mkono),” alisema Dk Kessy.

Takukuru na madeni

Mwanasheria kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe aliunga mkono kauli ya Rais Samia kwamba Takukuru imekuwa ikifanya majukumu mengine ambayo siyo yake hasa kwa kukusanya madeni.

Alisema taasisi zinazotoa mikopo zina mamlaka yake ya udhibiti ambayo inaongozwa na sera ya mikopo, hivyo halikuwa jukumu la msingi la Takukuru kujitwisha mzigo huo ambao umekuwa ukizalisha kesi nyingi za madai.

“Kesi nyingi zimekuwa zikifunguliwa lakini ushahidi unakuwa mdogo. Takukuru wamekuwa na mbwembwe wanapotaka kuwapeleka watuhumiwa mahakamani, wanafanya mikutano na wanahabari, lakini baada ya siku chache wale watu wanaachiwa kwa sababu hakuna ushahidi,” alisema Massawe.

Mwanasheria huyo alibainisha kwamba kazi ya Takukuru siyo tu kupambana na rushwa bali pia kutoa elimu. Alisisitiza kwamba Takukuru imejikita katika kupambana lakini haijaweka nguvu katika kuelimisha jamii juu ya rushwa.

Ukaguzi BOT

Mtaalamu wa uchumi, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema Rais Samia amemwagiza CAG kukagua hesabu za BoT kuanzia Januari hadi Machi kwa sababu kulikuwa na tetesi za matumizi mabaya ya fedha na yeye hakuwa na taarifa.

Alisema Rais Samia hakuwa na taarifa kwa sababu imezoeleka Makamu wa Rais ni mtu ambaye hahusiki na masuala ya fedha, hivyo, baada ya kuwa Rais, anahitaji kupata hizo taarifa kutoka kwenye mamlaka husika.

Alichosema CAG

Juzi, CAG aliwasilisha ripoti zake za ukaguzi za mwaka 2019/20 kwa Rais Samia jijini Dodoma ambapo alibainisha kwamba ATCL imekuwa ikipata hasara katika miaka mitano iliyopita.

Kichere aliitaka Serikali kuchukua hatua ili kuisaidia kampuni hiyo kujiendesha kwa ufanisi zaidi na kuiepusha na hasara inayopatikana.

Hii si mara ya kwanza kwa ripoti za CAG kunyooshea kidole utendaji wa ATCL. Ripoti ya CAG ya mwaka 2017/18 ilibainisha kwamba ATCL imekuwa ikipata hasara kwa muda wa miaka 10 mfululizo kutoka mwaka 2006/07 mpaka mwaka 2016/17. Alisema hasara hiyo ilipunguza mtaji wa kampuni mpaka kufikia mtaji hasi.

Taarifa hiyo ilibainisha kwamba katika miaka mitatu kufikia 2017/18, CAG alianza kuona mwenendo mzuri wa kampuni maana hasara ilipungua kutoka Sh38.7 bilioni ya mwaka 2005/06 mpaka Sh16.2 bilioni mwaka 2016/17, ambalo ni punguzo kwa takribani asilimia 58.

CAG alibainisha kwamba kupungua kwa hasara hiyo kumetokana na kuongezeka kwa mapato kwa asilimia 20 na kupungua kwa gharama za uendeshaji kwa asilimia 27.

CAG alipendekeza kwamba ATCL iendelee kuimarisha utendaji wake wa kazi ili kuweza kupata faida kwa kuongeza mapato na kupunguza gharama za uendeshaji kwa kutoa huduma nzuri kwa wateja, kutumia vizuri ndege zilizopo, na kubuni mbinu za kupunguza gharama zaidi.

Pia, alipendekeza Serikali itoe msaada wa kifedha kwa kampuni ili kuiwezesha kulipa madeni ya nyuma yanayoiongezea gharama kupitia ulipaji wa riba ambazo zinachukua nafasi kubwa ya gharama.

Hata hivyo, Desemba 2018 wakati wa mapokezi ya ndege aina ya Airbus, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas aliandika katika ukurasa wake wa Twitter akimnukuu hayati John Magufuli akisema “Tangu ndege zetu zianze kufanya kazi, zimeshaingiza faida ya Sh28 bilioni.”