Watano jela kwa makosa ya ubakaji, kukutwa na nyara za Serikali

Muktasari:

  • Hayo yamebainishwa jana Septemba 4, 2023 na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Muhudhwari Msuya, ambapo amesema, kukamatwa kwa watu hao, kulitokana na ushirikiano mzuri baina ya jamii na jeshi hilo.

Kibaha. Mahakama mkoani Pwani, imewahukumu watu wawili kifungo cha maisha jela, huku wengine watatu wakiamriwa kutumikia kifungo kati ya miaka 20 na 30, baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mbalimbali.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Muhudhwari   Msuya, ambapo amesema, kukamatwa kwa watu hao, kulitokana na ushirikiano baina ya jamii na jeshi hilo.

Amesema watu hao walikamatwa kwa nyakati tofauti, kisha wakafikishwa kwenye vyombo vya sheria, baada ya mahakama kujiridhisha pasipokuwa na shaka juu ya tuhuma zilizokuwa zikiwakabili, imetoa hukumu kulingana na makosa yao.

Kamanda Msuya amewataja waliohukumiwa kuwa ni Salumu Issa, ambaye amehukumiwa kwenda jela maisha, baada ya kukutwa na kosa la kulawiti.

Mwingine aliyehukumia kutumikia kifungo cha maisha gerezani ni Yusuph Athumani, aliyepatikana na hatia ya kukutwa na nyara za Serikali kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, mahakama za mkoa huo, pia zimewahukumu Mazowea Salumu na Albino Anthony, ambao wamekutwa na hatia baada ya kutenda makosa ya ubakaji, ambapo kila mmoja atatumikia kifungo cha miaka 30 gerezani.

“Pia yupo Hamisi Iddi, huyu alitiwa hatiani kwa kosa la kukutwa na nyara za Serikali na hivyo kuhukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 20 jela,” amesema Kamanda Msuya na kuongeza;

“Adhabu hizi zimetolewa hivi karibuni kwa nyakati tofauti na mahakama mbalimbali mkoani Pwani, ambapo kesi nyingi kati ya hizo, zinahusisha vitendo vya ubakaji,” amesema.

Hivyo basi, Kamanda Msuya ametoa onyo kwa watu wanaopenda kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa sheria, akiwataka kuacha kufanya hivyo, kwani Serikali haitawafumbia macho na kwamba mkono wa sheria utawafikia na kuhakikisha wanapata adhabu kulingana na makosa yao.