Watanzania na fursa mpya za bima

Muktasari:

  • Machungu ya matukio ya moto kwenye masoko na nyumba za makazi yaliyoshika kasi kwa siku za hivi karibuni, huenda yakapata ahueni kutokana na Watanzania hususan wafanyabiashara kuhamasishwa kujiunga na huduma za bima.

Machungu ya matukio ya moto kwenye masoko na nyumba za makazi yaliyoshika kasi kwa siku za hivi karibuni, huenda yakapata ahueni kutokana na Watanzania hususan wafanyabiashara kuhamasishwa kujiunga na huduma za bima.


Tayari, Benki ya NMB ambayo ni mdau mkubwa imezindua kampeni maalum yenye lengo la kutoa hamasa na elimu kuhusu umuhimu wa bima kwa jamii ili kuongeza idadi ya wanaotumia bima kutoka asilimia 15 ya sasa hadi 50 ifikapo mwaka 2030.


Kampeni hiyo maarufu kama "Umebima? Imezinduliwa leo Jumanne ya Machi 8, 2022 kwenye viwanja vya Soko la Karume, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na kampuni 10 za bima nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi amesema licha ya umuhimu wa bima kwa maisha ya Watanzania na shughuli za kila siku, bado muitikio wa watu kukata bima ni mdogo.


"Pamoja na elimu kutolewa bado idadi ya watu wanaoweka bima ni ndogo, ni asilimia 15 tu ya Watanzania ndio wanaotumia huduma za bima, idadi hii bado ni ndogo," amesema Mponzi na kuongeza: “Lengo la NMB kupitia kampeni hii ni kueneza elimu na hamasa juu ya uwekaji wa bima ili idadi hii ya Watanzania wenye bima iongezeke kutoka asilimia 15 hadi 50 ifikapo mwaka 2030”


“Kwa sababu za Kijiografia, tunatambua kuwa kampuni hizi za bima hazijafika maeneo yote nchini, lakini NMB iko nchi nzima tumeona tushirikiane na sasa zitapatikana kila tawi la NMB hapa nchini.”
Mponzi amesema pamoja na kupatikana kwa huduma ya bima kwenye matawi yao, lakini elimu kuhusu bima na umuhimu wake itatolewa.


Mkuu wa Idara ya Bima wa NMB, Martine Massawe amesema kampeni itakuwa endelevu na itasambaa kwenye mikoa mbalimbali nchini.


“Leo tunazindua hapa Karume, Dar es Salaam lakini pia mikoa kadhaa inafanya uzinduzi na tutasogea kila mikoa ili kuhakikisha elimu hii ya bima inawafikia Watanzania wengi,” amesema Massawe


Katika huduma hiyo ya bima, NMB inashirikiana na kampuni za Sanlam Life, UAP, Shirika la Bima la Taifa (NIC), Jubilee Insurance, Jubilee Life, Metropolitan Life, Britam Insurance na Shirika la Bima Zanzibar (ZIC).