Watoto 133,438 kupata chanjo ya surua, rubella Mbeya

Muktasari:

  • Kampeni ya kutoa chanjo ya surua na rubella kwa watoto wenye umri kuanzia miezi tisa mpaka miaka mitano, itaanza Februari 15 hadi 18 2024 itahusisha.

Mbeya. Jumla ya watoto 133,438 wenye umri kati ya miezi tisa mpaka miaka mitano mkoani hapa wanatarajia kupatiwa chanjo  ya ugonjwa wa surua na rubella.

Akizungumza baada kuzindua kampeni ya chanjo hiyo jana Februari 9, 2024 Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amewaomba viongozi wa dini kuisaidia Serikali kutoa elimu ya ushiriki wa wananchi kupeleka watoto kupata chanjo.

“Niombe viongozi wa dini na wa mila kushirikiana na Serikali kuisemea kampeni hii katika jamii, kwani mna kundi kubwa la watu wanaowaamini. Zungumzeni na watu kuhusu udanganyifu, dhana na mila potofu kuhusu chanjo hiyo kuwa na madhara,” amesema.

Akizungumzia dalili za ugonjwa wa surua, Malisa amesema ni pamoja na homa, mafua, kikohozi, macho kuwa mekundu na kutoa majimaji na vipele vidogo vidogo ambavyo huanza kujitokeza kwenye paji la uso, nyuma ya masikio na kusambaa usoni na mwili mzima.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa ametaka katika kampeni hiyo wenyeviti wa Serikali za mitaa, madiwani washirikishwe ili kuwasaidia wataalamu wa afya wanapofika katika maeneo yao.

“Madiwani, wenyeviti watusaidie kuandaa wananchi ili kuhakikisha kila mtoto mwenye umri huo anapata chanjo ya surua na rubella ili kulinda afya yake na kutimiza ndoto zao,” amesema.

Kwa upande wake Janeth Thomas mkazi wa Mabatini jijini hapa, amesema kikubwa ni elimu kuanza kutolewa kwa wananchi hasa kuhusu imani kuwa chanjo nyingi zina madhara kiafya.