Watoto 172 wafanyiwa ukatili Mtwara

Baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe wa kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto Mkoani Mtwara wakiwa katika maadhimisho ya kilele cha siku16 za kupinga ukatili ambayo kimkoa yamefanyikia katika Mji wa Nanyamba. Florence Sanawa

Muktasari:

Watoto 172 wamefanyiwa ukatili mkoani Mtwara ambapo kati yao 84 walibakwa na 13 wamelawitiwa katika kipindi cha Mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu.

Mtwara. Watoto 172 wamefanyiwa ukatili mkoani Mtwara ambapo kati yao 84 walibakwa na 13 wamelawitiwa katika kipindi cha Mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu.

Katika takwimu hizo zililzotolewa na Jeshi la Polisi zilionyesha kuwa watu wazima ni 223 walifanyiwa ukatili katika kipindi hicho ikiwamo shambulio 96, kujeruhi 37, kudhulumiwa 31 na matusi 30.

Akizungumza leo Jumapili Desemba 11, 2022 katika kilele cha siku 16 za kupinga ukatili Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Dunstan Kyobya kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas amesema kuwa idadi ya watoto kubakwa inatisha.

“Tokomeza ukatili, unaendelea kwenye kazi, majumbani, mashambani, ibadani na mashuleni hali si nzuri ndio maana leo tunapena elimu. Changamoto ni kubwa tuvunje ukimya ndani ya familia”amesema Kyobya

Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia Polisi Mkoa wa Mtwara, ASP Bahati Sembera amesema kuwa jamii imekuwa ikipewa elimu ya kuvunja ukimya uliopo ndani ya jamii ili kufichua ukatili.

“Upo ukatili wa kingono mara nyingi watoto wanabakwa kwa kuwa hawana ridhaa lakini kwenye ndoa ni ukatili wa kingono, ukatili wa kisaikolojia” amesema

Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Mtwara, Thabitha Kilangi amesema katika siku 16 za kupinga ukatili shughuli mbalimbali zilifanyika na wadau mbalimbali walishiriki kutoa elimu ili kujenga uelewa kuhusu ukatili wa kijinsia.

“Tulifanya mijadala na midahalo 38 ilifanyika wananchi 11,147 makongamano 19 yalifanyika wananchi 10,256 walishiriki”

“Wote tunawajibu wa kutoa elimu kwa jamii ili kuwanusuru na vitendo ya ukatili wa kijinsia” amesema Kilangi