Wawili wafariki Same kwa kuangukiwa na gema,  kaya 10 zikiachwa bila makazi

Eneo la Barabara ya Ndungu-Lugulu, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro likiwa limeharibiwa na mvua zilizonyesha maeneo ya milimani ambayo imeporomosha mawe na magogo na kusababisha kukatika kwa mawasiliano ya barabara hiyo. 

Muktasari:

  • Watu wawili akiwemo mwanafunzi wa darasa la sita, Ramadhan Ayoub Mduma(12) aliyekuwa akisoma Shule ya Msingi Lugulu, wamefariki dunia wilayani hapa, baada ya nyumba walizokuwa wakiishi  kuangukiwa na gema kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya milimani.

Same. Watu wawili akiwemo mwanafunzi wa darasa la sita, Ramadhan Ayoub Mduma(12) aliyekuwa akisoma Shule ya Msingi Lugulu, wamefariki dunia wilayani hapa, baada ya nyumba walizokuwa wakiishi  kuangukiwa na gema kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya milimani.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu ambaye amesema yuko njiani kuelekea eneo la tukio amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo usiku wa kumkia leo, Januari 10, 2024.

"Watu wawili wamefariki dunia, akiwemo mwanafunzi wa darasa la sita, aliyekuwa akisoma Shule ya Msingi Lugulu na  kijana mmoja,  tuko njiani kuelekea eneo la tukio kuona hali ilivyo."amesema RC Babu wakati akizungumza na Mwananchi Digital  kwa njia ya simu.

Akizungumzia tukio hilo la  maafa, Mtendaji wa kata ya Lugulu, Janeth Mbwambo amesema mvua zilizonyesha usiku wa kumkia leo Januari 10,2024, wilayani humo zimeleta madhara makubwa kwa wananchi ikiwemo kifo cha mwanafunzi pamoja na nyumba kuangukiwa na gema ambapo kaya zaidi ya tano zimeachwa bila makazi.

"Barabara zimeharibika, nyumba zimeangukiwa na  gema kutokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku na kusababisha vifo katika Kata yangu, huku kwingine bado sijafahamu maana mawasiliano ya barabara hakuna lakini tumeambiwa uongozi wa mkoa unakuja,”amesema Janeth.

Amesema jitihada ambazo zinafanyika kwa sasa ni kuwaondoa watu katika maeneo yaliyoathiriwa na maporomoko ya udongo ili wawe sehemu salama zaidi.

Mtendaji wa kata ya Mtii, Yunis Mndeme amesema katika kata hiyo amefariki kijana mmoja, aitwaye  Noel Gilbert (17) ambapo nyumba aliyokuwa amelala iliangukiwa na maporomoko ya udongo ya mvua na kusababisha kifo chake, huku kaya zaidi ya tano zikiachwa bila makazi.

"Mpaka sasa nyumba zaidi ya tano zimeangukiwa na gema na zimebomoka ambapo wengine  tumeshaanza kuwahamisha, ambapo kuna wengine nyumba zao zimeanguka  lakini wametoka salama,"amesema.

Kulionekana dalili za maporomoko miaka ya nyuma

Maporomoko ya Novemba 11,2009 yaliyotokea usiku katika Kitongoji cha Manja, Kata ya Mamba Miamba yalisababisha vifo vya watu 24.

Watu hao walifunikwa kwa mawe na miamba iliyoporomoka kutoka kwenye mlima Manka. Wananchi walikuwa wakiishi kando mwa mlima huo.

Katika tukio hilo, familia moja ilipoteza wanandugu 15. Maporomoko hayo ya mlima mwenye miamba na majabali makubwa yalitokea wakati mvua kubwa ikinyesha.

Ilielezwa dalili za kuporomoka mlima zilianza kujionyesha mwaka 2008  kutokana na ufa uliokuwepo.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro wakati huo, Monica Mbega, alisema wananchi wa kata ya Mamba Miamba waliona dalili za kuporomoka mlima mwaka mmoja kabla ya tukio hilo, lakini hawakuchukua tahadhari.

Alisema ufa huo uliziba Mei 2009 lakini kwa ndani kulibaki shimo kubwa.

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Same, Ibrahim Marwa alisema tukio la kuporomoka mlima liliwahi kutokea eneo la Hedaru lakini halikusababisha madhara, hivyo kulikuwa na umuhimu wa kufanyika uchunguzi.