Wazazi wasimulia walivyopoteza watoto wa pekee ajali ya Arusha

Peter Shayo (wa pili kulia) ambaye amepoteza watoto wawili katika ajali ya gari la Shule ya Msingi Ghati Memorial lililosombwa na mafuriko, akiwa na ndugu na jamaa nyumbani kwake Mtaa wa Engosengiu, Kata ya Sinoni jijini Arusha. Picha na Janeth Mushi

Muktasari:

  • Familia mbili kila moja yapoteza watoto wawili wa pekee.

Arusha. Familia mbili zimebaki pweke baada ya kila moja kupoteza watoto wawili katika ajali ya gari la Shule ya Msingi Ghati Memorial, jijini Arusha.

Kila moja kati ya familia hizo zilikuwa na watoto hao pekee.

Ajali hiyo imetokea jana alfajiri baada ya gari kuanguka kwenye korongo la Sinoni lililojaa maji katika eneo la Dampo.

Katika ajali hiyo watoto wanane walifariki dunia pamoja na msamaria mwema aliyeshiriki kazi ya uokoaji.

Gari hilo lilikuwa na jumla ya watu 13, wakiwemo wanafunzi 11, matroni na dereva. Watu watano waliokolewa wakiwa hai.

Wanafunzi walionusurika, wazazi na watu wengine walioshuhudia ajali hiyo wameeleza chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo aina ya Toyota Hiace, aliyeonywa asipite eneo hilo lililokuwa limefurika maji lakini hakusikiliza.


Kilio cha wazazi

Peter Shayo, ambaye katika ajali hiyo amepoteza watoto wa pekee wawili, aliwataja kuwa ni Abigail Peter (11) na Abiabol Peter (5).

Akizungumza na gazeti hili leo Jumamosi Aprili 13, 2024 nyumbani kwake Mtaa wa Engoseniu, Kata ya Sinoni, amesema siku ya ajali jana yeye ndiye alikuwa na watoto kwa kuwa mama yao alikuwa safarini.

Amesema alisita kuwapandisha kwenye gari baada ya kuwa wamechelewa akitaka kuwapeleka kwa gari binafsi, ila baada ya dereva aliyekuwa amewaacha watoto, kumpigia simu aliwapeleka.

"Nilisita kwanza, tulichelewa nikasema sitawapeleka, baadaye dereva akanipigia simu napita chini njoo walete watoto, nikaenda kumbe amesharudi juu akawa amewaacha, nikampigia simu akageuza gari akaja kuwachukua. Nikawapakia watoto na yule mdogo nikampakia mbele," amesema.

"Nikamwambia dereva leo kuna mafuriko chukua tahadhari yasije kuleta madhara kwa watoto, hakunijibu chochote, akaondoa gari kwa kasi sijui alikuwa anawahi, ila ndiyo hivyo nimepoteza watoto wawili ambao ndiyo nilikuwa nao, mmoja alikuwa darasa la tano na mdogo wake wa kiume mwakani alikuwa aingie darasa la kwanza," amesema.

Shayo amesema dakika chache baada ya gari kuondoka, kila alichokuwa anajaribu kufanya hapo nyumbani kilishindikana.

Muda mfupi baadaye amesema alipigiwa simu na jirani yake aliyemuuliza kama watoto wake wameenda shule.

Anaeleza alipomjibu ndiyo, jirani yake alimwambia kuna gari la shule hiyo limesombwa na maji.

"Nilikuwa na kitu mkononi nikakiangusha chini, nikachukua ufunguo wa gari nikakimbia kufika pale sijaona watoto, nilikuta watu wengi tu, ila baadaye ndugu zangu walienda mochwari na kuhakikisha wameona miili ya watoto wetu," amesema.

Shayo amesema, "watoto wetu wamekufa vibaya jamani, dereva ameaswa, amefika pale ameonywa ila kwa dharau hakuonyesha kutii, akawapitisha watoto.”

Amesema, “watoto wakawa wanapiga kelele anko tunakufa, hakuwasikiliza. Sina watoto wengine, wameshaondoka wote, sijabakishiwa mtoto."

Mzazi mwingine, Elizabeth Mollel, ambaye pia amepoteza watoto wawili katika ajali hiyo, ambao nao ni wa pekee katika familia, ameiomba Serikali ichukue hatua madhubuti kuhakikisha madereva wa magari ya shule wanazingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazoepukika.

"Kwa kweli huu msiba kwanza umenisikitisha, maana watoto wangu wamekufa kama vile kifo cha kusukumiwa, maana ukipiga hesabu kuna watu walikuwa wanamsemesha dereva kwamba usiwapitishe watoto hapo, maana hapafai lakini akawapitisha watoto. Anakemewa kabisa na madereva wa Toyo (pikipiki) lakini hakuruhusu kusikiliza ushauri wa watu," alieleza akiwa nyumbani kwake.

"Naomba madereva wachukuliwe wenye leseni, wawe wanaojitambua, maana hatuelewi huyo ni nini kilichomvaa ila kitendo alichofanya si kizuri kwani unatakiwa usikilize watu, hujui wanakupenda au wakuokoe kwa kile unachokifanya," amesema.

Mzazi huyo amesema, "kitu kilichofanyika ni kibaya, watoto wanamuambia anko tunakufa, yeye anacheka. Watoto wengine walikuwa na wadogo zao wanatafuta kuwaokoa wakashindwa. Moyo wangu unauma nimepoteza watoto wote nimebaki mwenyewe inauma sana," amesema.

Emmanuel Mushi, mume wa Elizabeth amewataja watoto wao waliofariki dunia kuwa ni Altrisha Emmanuel na Mogan Emmanuel.


Ufanyike ukaguzi

Mzazi mwingine, Jonas Ernest aliyempoteza mtoto wake, Noela Ernest (4) ameiomba Serikali kufanya operesheni maalumu kwenye shule mbalimbali nchini kukagua madereva ili kupunguza ajali zinazoepukika.

"Serikali kama walivyofanya ukaguzi kuhakikisha hivi vyombo vinavyobeba watoto ni salama, waangalie madereva, wachukuliwe wenye uzoefu na wahakikishe hawajawahi kusababisha matatizo,” amesema.

Diwani wa Kata ya Sinoni, Michael Kivuyo amesema miili itaagwa leo katika Shule ya Sekondari Sinoni na maandalizi ya shughuli hiyo yanaendelea.

"Kutokana na msiba huu yako mengi wananchi wamejifunza, ikiwemo kuchukua tahadhari, na wamiliki wa shule kuhakikisha wanaajiri madereva makini ili kuepusha majanga yanayoweza kujitokeza kutokana na uzembe," amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa amesema idadi ya vifo katika ajali hiyo ni tisa, wakiwemo wanafunzi wanane.

"Tunatarajia kukaa kikao viongozi wa Serikali kujua namna ya kufanya msiba huu lakini kwa awali tutatoa jeneza kwa kila mwili na mkono wa pole ambao tutasema kiasi baadaye," amesema.


Shughuli za uokozi

Katika ya uokoaji uliochukua zaidi ya saa 11 jana, ukiongozwa vyombo vya ulinzi na wananchi, uliwezesha miili saba ya wanafunzi na mtu mzima mmoja kupatikana.

Mwili wa mtoto mmoja umepatikana leo mchana zaidi ya kilomita 37 kutoka eneo la tukio.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Arusha, Osward Mwanjejele amesema miili hiyo ni ya Shadrack William, Noel Jonas, Dolan Jeremiah, Winfrida Emmanuel, Atrichan Emmanuel, Morgan Emmanuel, Abigail Peter na Abiabol Peter.

Amewaomba wakazi wa eneo ilikotokea ajali kujitokeza kuutambua mwili wa mtu aliyekuwa anasaidia shughuli za uokoaji ambaye pia alifariki na mwili wake ulipatikana jana.

Ametoa rai kwa wananchi kuchukua tahadhari wakati huu wa mvua zinazoendelea kunyesha.

Pia amezishauri shule zenye magari ya kubeba wanafunzi kuongeza umakini na madereva wao.