Waziri Ummy aipa siku 14 NHIF kukamilisha maboresho Toto Afya

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu leo Jumamosi Februari 11 wakati akiweka jiwe la msingi katika jengo la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Muktasari:

  • Zikiwa zimepita siku mbili tangu mzozo baina ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na wananchi kufuatia mfuko huo kuondoa kifurushi cha TotoAfya Card, Waziri mwenye dhamana ya afya, Ummy Mwalimu ameiagiza taasisi hiyo kukamilisha maboresho ndani ya wiki mbili.

Dar es Salaam. Waziri wa Afya Tanzania, Ummy Mwalimu ametoa wiki mbili (sawa na siku 14) akiuagiza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuhakikisha inarudi na mfumo rafiki kwa ajili ya kundi la watoto wa mwaka sifuri mpaka miaka 18.

Agizo hilo amelitoa leo Jumatano Machi 15, 2023 wakati wa mjadala wa Mwananchi Twitter Space ambao umeangazia miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan madarakani tangu alipoapishwa Machi 19, 2021.

Ummy ameyasema hayo baada ya swali aliloulizwa na baadhi ya wachangiaji akiwemo Mhariri wa Habari wa Gazeti la Mwananchi ambaye alichokoza mada Lilian Timbuka akitaka ufafanuzi kuhusu sakata hilo lililodumu kwa siku mbili.

“Tunahitaji kujua kwa changamoto zilizopo sasa, mnakwenda kujipanga vipi kwa miaka hii miwili iliyosalia? Juzi tumeona kuna mzozo wa bima ya afya kwa mtoto na kwa sasa hivi tunaona kulikuwa na mkwamo wa bima ya afya kwa wote,” amehoji Timbuka.

Hata hivyo, Waziri Ummy amesema hataweza kulijibu kwa kina kwa sasa huku akiwataka Watanzania wawe watulivu katika kipindi hiki cha mpito na kutoa maagizo.

“Miaka saba tangu kuanzishwa kwa bima ya TotoAfya Kadi ambayo tulilenga kutoa matibabu kwa watoto mwaka sifuri mpaka miaka 18 waliopo shuleni wamejiandikisha watoto zaidi ya 200,000 pekee na asilimia 90 ya hawa watoto wamekatiwa bima tayari wakiwa ni wagonjwa.

“Hii imeondoa dhana ya bima ya afya, ambayo ni kuchangiana wanatakiwa watoto 100 wanaoweza kuwachangia wenzao 10 kama itakuwa tofauti hiyo bima haiwezi kuwa stahimilivu,” amesema Waziri Ummy na kuongeza;

“Nimewaagiza Mfuko wa Bima wa Taifa (NHIF) wakalimishe hili haraka, waweke mfumo rahisi ili tupate watoto wengi tuweze kujenga utaratibu wa kuwa na bima ya afya ili kufikia afya kwa wote.Tuwaache NHIF ndani ya wiki mbili wakamilishe hili,” amesisitiza.