Wizara ya Madini kufuta leseni zisizoendelezwa, wachimbaji wataja sababu

Waziri wa Madini, Dotto Biteko akizungumza kwenye maonyesho ya madini na fursa za uwekezaji Mjini Ruangwa mkoani Lindi. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Wizara ya Madini kufuta leseni kwenye machimbo ya madini yote ambayo hawaendekezi maeneo yao

Ruangwa. Waziri wa Madini, Dotto Biteko amewataka wachimbaji madini nchini kuyaendeleza maeneo yao kwani Serikali ina mpango la kuzifutia leseni zote zisizo endelezwa.

Waziri Biteko akizungumza kwenye maonyesho ya madini na fursa za utalii katika viwanja vya Kilimahewa mjini Ruangwa mkoani Lindi, amesema wenye leseni wanapaswa kuyaendeleza maeneo yao.

"Tutatoa notisi kwa muhusika asipotimiza wajibu wake tunafuta leseni yake kwasababu unakuta mtu anamuuzia mtu mwingine eneo bila kushirikisha Wizara ya Madini…kazi yao ni udalali wa kuuza mahali," amesema Waziri Biteko.

Mchimbaji mdogo wa madini ya Gypsum, katika machimbo ya Makangaga, Hubert John amesema gharama ya kuyaendesha machimbo hayo ni kubwa ndio sababu ya kushindwa kuyaendeleza.

"Inatakiwa tuungane wengi tukafanye kazi sehemu moja kuliko kufuta leseni kwani wachimbaji wadogo wengi wao watarudishwa nyuma kiuchumi, " amesema John.

Mkurugenzi wa kampuni ya Gemini Exploration and Mining Service (GEMS), Alfred Kimbi amewakaribisha wawekezaji na wachimbaji wa madini kwenye maeno tofauti wilayani Ruangwa.

Kimbi amesema madini yanayopatikana kwenye machimbo yake ni madini ya dhahabu, green na ulanga (Kinywe).