Zabuni ujenzi daraja la Jangwani yatangazwa

Muktasari:

  • Zabuni kwa ajili ya ujenzi wa daraja la juu 'Fly Over' kuanzia Magomeni kupita Jangwani hadi Faya, chini ya mradi wa uendelezaji wa mji katika Bonde la Mto Msimbazi, imetangazwa na mkandarasi atakayejenga atajulikana hivi karibuni.

Dar es Salaam. Mkandarasi atakayejenga daraja la juu ‘Fly Over’ kuanzia Magomeni kupita Jangwani hadi Faya atajulikana hivi karibuni baada ya zabuni kutangazwa.

Ujenzi huo ambao uko chini ya mradi wa uendelezaji wa mji katika Bonde la Mto Msimbazi, unaratibiwa na Ofisi ya Rais Tamisemi chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 7, 2024 jijini Dar es Salaam, mratibu wa mradi huo, Humphrey Kanyenye kutoka Tamisemi amesema wameshatangaza zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi.

“Tenda ilishatangazwa na tuko katika hatua za mwisho kumpata mkandarasi na mtaalamu wa ushauri wa usimamizi wa ujenzi wa daraja,” amesema.

Pia amesema mradi utahusisha ujenzi wa kingo za Mto Msimbazi. Amesema mwisho wa mwezi Februari watakuwa wameshakamilisha zabuni kumpata mkandarasi na msimamizi wa ujenzi.

Amesema wakati wa utekelezaji wa mradi huo, kituo kikuu cha mabasi yaendayo haraka kitahamishiwa Ubungo Maziwa kutoka Jangwani ambapo kimekuwa kinajaa maji kila mvua zinaponyesha.

Thamani ya mradi huo ni Sh650 bilioni ambazo ni mkopo usio na riba kutoka Benki ya Dunia na utakamilika ndani ya miaka sita kutoka sasa.


Fidia zaanza kulipwa leo

Katika hatua nyingine Kanyenye amesema Sh4 milioni zilizotolewa na Serikali kwa kila kaya kwa ajili ya fidia ya ardhi kwa wakazi wa eneo lililopitiwa na mradi, zimeanza kulipwa leo Februari 7, 2024.

Fedha hizo hazihusiani na fidia za majengo ambazo wakazi wa eneo hilo, walikwishalipwa.

Kanyenye amesema hatua hiyo inakuja baada ya kukamilika kwa taratibu zote za malipo pamoja na kujiridhisha.

"Serikali iliamua kulipa fedha hizo ili wahusika wakapate sehemu nyingine (kununua viwanja) wajenge, baada ya kufanya tathmini ya maeneo kama Chanika, Kigamboni yenye thamani hiyo ya viwanja," amesema.

Amesema wakati hatua za kuwahamisha wakazi hao zinaanza mwaka 2022, walipata waathirika 2,592 ambao walipitiwa na mradi.

"Kati ya hao waliofanyiwa tathmini ni 2,329 na waliokwishalipwa hadi sasa ni 2,102, huku 227 hawajalipwa kutokana na kuwa na migogoro ya kifamilia na wengine hawajajitokeza.

Amesema kuna watu 184 ambao waligoma kusaini fidia wakidai ni ndogo na wengine 186 hawakufikiwa kutokana na mazingira au kutokuwepo eneo la tathmini.