Zahanati ya kijiji yafungwa kwa kukosa mhudumu, wananchi wahaha

Zahanati ya kijiji cha Namwangwa ambayo haitoi huduma kutokana na kukosa mhudumu wa afya

Muktasari:

  •  Zahanati hiyo inahudumia takribani wagonjwa 50 kwa siku, huku kijiji ilipo kina wakazi zaidi ya 1,000.

Mbozi. Zaidi ya wananchi 1,000 wa Kijiji cha Namwangwa, Kata ya Hezya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, wamekosa huduma za afya kwa miezi mitatu sasa, baada ya tabibu anayehudumu kwenye zahanati ya kijiji hicho kustaafu.

 Wananchi hao wamekumbwa na changamoto hiyo baada ya mhudumu wa awali kustaafu tangu Novemba, 2023 na Serikali ilipeleka tabibu mwingine Februari, 2024 lakini mwezi uliopita amehamishwa na kusababisha zahanati hiyo ifungwe.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi Digital leo Jumanne Aprili 16, 2024 kijijini hapo, baadhi ya wananchi wamesema zahanati hiyo ambayo ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 50 kwa siku, ilikuwa msaada mkubwa kwao, lakini sasa wanalazimika kufuata huduma maeneo mengine.

“Wajawazito walikuwa wanapata msaada mkubwa hapa, chanjo za watoto lakini sasa imefungwa, huduma hizo hakuna tena,” anasema Amani Mnkondya, mkazi wa kijiji hicho.

Amesema mpaka sasa hawaelewi kwa nini tabibu aliyeletwa baadawa awali kustaafu naye amehamishwa.

Amesema wanakijiji wana imani kuwa Serikali inatambua hitaji la msingi la kijiji hicho, lakini mpaka sasa iko kimya na zahanati imefungwa.

Mkazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Tamiwe Mwazembe amesema; “Tunashindwa kuelewa, sisi tunapata shida ya kutafuta matibabu maeneo mengine, wakati zahanati yetu imefungwa ikiwa na vifaa vyake vyote eti kisa mganga hayupo. Haiingii akilini, Serikali ifanya jambo imalizo kero hii.”

Amesema kitendo cha kumuhamisha mtumishi wakati hakuna mbadala hakuleti picha nzuri. “Ina maana Serikali inaona sisi hatuna maana mpka wanamhamisha mtumishi wao wanampeleka sehemu nyingine? Hii si sawa,” amelalamika Mwazembe.

Naye Flora Mwashiuy,a ameiomba Serikali itatue suala hilo mapema kwa sababu wajawazito na watoto ndiyo wanaoathirika zaidi.

"Tulikosa mhudumu wa afya kwa miezi miwili tangu mwezi wa 11 mwaka jana, mwezi wa pili mwaka huu wakamleta mhudumu amekaa mwezi huo tu wamemuhamisha tena na mpaka sasa hawajaleta mwingine zahanati imefungwa, sasa ilijengwa kwa ajili ya nini,” amehoji Mwashiuya.


Kauli ya mwenyekiti wa kijiji

Akizungumzia kadhia hiyo, mwenyekiti wa kijiji hicho, Komilyasi Mwampashi amesema,"Sisi tunaamini mtumishi akihamishwa analetwa mwingine, lakini kwetu imekuwa tofauti, mhudumu alikuwa mmoja akahamishwa tumebaki kuhangaika kupata huduma za afya.

“Tunaiomba serikali itusaidie kunusuru afya za watu wetu hasa wajawazito.".

Mwananchi Digital ilimtafuta Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Alex Mugeta ambaye amekiri zahanati hiyo kufungwa kwa kukosa mhudumu.

Hata hivyo, amesema tayari wameanza utaratibu wa kumpata tabibu mwingine na watakamilisha muda si mrefu, japo hakutaja ni lini hasa atapatikana.

"Ni kweli mhudumu hayupo, ninatambua wananchi wanakosa kweli huduma, naomba wavute subira muda sio mrefu tutampeleka mhudumu," amesema Dk Mugeta.