Athari kwa mtoto aliyeachishwa ziwa ghafla

Dodoma. Suala la kuachisha mtoto kunyonya maziwa ya mama linahitaji maandalizi ya kutosha, ili hata anapoachishwa aendelee kuwa na afya nzuri.

Hali ilikuwa tofauti kwa Milka Chedego, aliyemwachisha mwanaye wa umri wa mwaka mmoja na miezi sita ghafla, bila maandalizi yoyote, hali iliyosababisha utapiamlo kwa mtoto.

Milka anasema hali hiyo ilimgharimu fedha nyingi na muda, kumrudisha mwanaye kwenye hali ya kawaida.

Mama huyo ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) mwaka wa kwanza, amesema alilazimika kumwachisha mtoto wake kwa sababu alikuwa hataki kula zaidi ya kunyonya, wakati ambao naye alikuwa kwenye mitihani ya muhula wa kwanza.

Amesema kutokana na maandalizi ya mitihani hiyo na mtoto kukataa kula chakula kingine, aliamua kumwachisha ili akiumwa njaa ale na yeye apate muda mzuri wa kujisomea.

Amesema alifanya hivyo bila maandalizi yoyote kuhusu lishe ya mtoto wake, lakini haikusaidia kwani aliendelea kukataa chakula, hali iliyomfanya mtoto huyo adhoofike.

"Kwanza alianza kuharisha na baadaye kutapika kila alichokuwa anakula, hakuna chakula kilichokaa tumboni," anasema Milka na kuongeza:

"Nilimpeleka hospitalini baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, baada ya vipimo hakuonekana kuwa na ugonjwa wowote. Tulipewa dawa za kufunga kuharisha na zile za kurudisha maji mwilini (oral) lakini hata baada ya kutumia hali ya mtoto iliendelea kuwa mbaya, hakufunga kuharisha wala kutapika."

Amesema wakati huo alimwacha na msichana wa kazi, aliyempa mrejesho kuwa mtoto alikuwa anakula, lakini afya yake haikuwa nzuri na matokeo yake mtoto akaanza kuvimba macho, uso, tumbo, miguu na sehemu za siri hali iliyokuwa inamfanya alie kwa maumivu makali.

"Nakumbuka siku hiyo nilikuwa chuoni najiandaa kufanya mtihani saa 9 alasiri, nilipigiwa simu nyumbani kuwa hali ya mtoto siyo nzuri, nilijikaza nikafanya mtihani.

“Nilipomaliza nilirudi nyumbani na kukuta hali ya mtoto imebadilika, maana alikuwa amevimba mwili wote huku akilia kwa maumivu makali," anasema Milka.

Anasema alimbeba na kumpeleka kwenye kituo cha afya, huko daktari alipomwona alimwambia aende hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwani mtoto alikuwa na utapiamlo mkali, hivyo wao hawawezi kumhudumia.

Milka anasema alikwenda moja kwa moja kwenye wodi ya watoto ya hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma, huko alilazwa ili kuanza matibabu na kwamba huko mtoto alifanyiwa vipimo vingi vikiwemo vya figo.

"Baada ya majibu ya vipimo kutoka ilionyesha ana utapiamlo mkali uliosababishwa na kuachishwa kunyonya na hata wale niliowaachia mtoto, hawakumpa chakula kwa wakati na hivyo kusababisha apate tatizo hilo, ambalo matibabu yake yamegharimu fedha nyingi na muda pia," anasema.

Amesema pamoja na tatizo kugundulika, daktari alimshauri kumwangalia mtoto kwa ukaribu kwa kumpa vyakula vya kujenga mwili.

Mama huyo mwenye watoto watatu, amesema hakujua kumwachisha mtoto ziwa bila maandalizi ya kutosha kungeweza kumsababishia matatizo makubwa kiasi hicho kwani alidhani anamsadia, kumbe anamuumiza.


Njia sahihi

Akizungumzia sababu za utapiamlo kwa watoto, Daktari wa watoto kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk Halima Kassim anawataka wazazi kufanya maandalizi kwa muda wa mwezi mmoja au miwili kabla ya kumwachisha mtoto kunyonya.

Anasema maandalizi hayo yatasaidia mtoto kuendelea kuwa na afya njema, hata baada ya kuacha kunyonya kuliko kumkatiza ghafla.

"Maandalizi yanatakiwa yafanyike kwa mwezi mmoja kabla ya mtoto kuacha kunyonya kabisa, kama alikuwa ananyonya mchana na usiku unampunguzia anaanza kunyonya usiku tu.

“Kama alinyonya mara tatu kwa siku unampunguzia huku ukiendelea kumpa vyakula vingine vya kujenga mwili pamoja na maji mengi, unafanya hivyo mpaka anazoea na mwisho wa siku anaacha kunyonya huku akiwa na afya nzuri," anasema Dk Halima.

Anasema matatizo ya watoto kupata utapiamlo yanawakumba zaidi watoto wa wafanyakazi na wanafunzi kwa sababu hawana muda wa kukaa na watoto, zaidi ya kuwaachia wasaidizi wa kazi za nyumbani ambao husema watoto wanakula ilhali ni uongo, ili wasifukuzwe kazi, lakini mwisho wa siku watoto wanapata utapiamlo.

Anataja watoto walio kwenye hatari ya kupata utapiamlo ni wale wanaozaliwa na magonjwa kama Ukimwi, kifua kikuu na selimundu ambao wanatakiwa uangalizi wa karibu wa wazazi, kwani kinga zao ni rahisi kushuka na kupata maradhi mbalimbali, ikiwemo utapiamlo.

Naye mtaalamu wa lishe kutoka Wizara ya afya, Japheth Kizigo anasema ili watoto wasipate utapiamlo ni lazima wazazi wazingatie kanuni bora za lishe kwa kumnyonyesha bila chochote kwa miezi sita ya mwanzo, ili kumjengea kinga na atakapoanza kula chakula kingine kinatakiwa kiwe bora na si cha aina moja.

"Hapa kuna changamoto nyingine, maana watoto wana tabia ya kupenda aina moja ya chakula na kukataa vingine, hivyo kama mzazi hatakuwa makini, atajikuta anamlisha chakula anachokipenda kisicho na virutubisho vingine, mwishowe anaanza kupata utapiamlo," anasema Kizigo.