Zana za Kilimo Mbeya ilivyofufuka kivingine

Muktasari:

  • ZZK ni miongoni mwa viwanda vichache nchini vyenye karakana zenye uwezo wa kuzalisha vipuri na kufanya matengezo mbalimbali ya mitambo.

Kiwanda cha Zana za Kilimo (ZZK) kilichopo Iyunga Jijini Mbeya ni miongoni mwa viwanda vya zamani ambavyo vilikufa miaka ya nyuma kabla ya kufufuliwa upya na mwekezaji wa kizalendo, Kampuni ya CMG Investment miaka miwili iliyopita.

ZZK ni miongoni mwa viwanda vichache nchini vyenye karakana zenye uwezo wa kuzalisha vipuri na kufanya matengezo mbalimbali ya mitambo.

Hatua ya kiwanda hicho kuanza uzalishaji ni habari njema kwa Mkoa wa Mbeya na ukanda mzima wa nyanda za juu kusini ambako kilimo ndiyo shughuli kuu ya kiuchumi.

Kwa sasa, kiwanda hicho kinazalisha matrekta madogo (powertiller), majembe ya mkono, matoroli, mabati, mashine za kukoboa na kusaga, kupukuchua mahindi na nafaka nyingine.

Kama hiyo haitoshi, kiwanda hicho kinatengeneza nguo za zege zinazoweza kusafirisha umeme.

Meneja wa kiwanda hicho, John Mcharo anasema zaidi ya Sh5 bilioni zimewekezwa kiwandani hapo ili kukidhi mahitaji ya matreka madogo kwa ajili ya wakulima wakati nguzo za zege zikilenga kuokoa uvunaji ovyo wa misitu.

“Tunajenga viwanda kuleta suluhisho kwa mkulima,” anasema Mcharo.

Matrekta

Kabla kiwanda hicho hakijafa kilikuwa kikitengeneza majembe ya mkono na nyenzo mbalimbali za kazi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, bustani na shambani.

Lakini uwekezaji uliofanywa na kampuni ya CMG Investment umeongeza zana zinazotengenezwa kwa kutumia teknolojia bora kama vile uunganishaji wa powertiller, majembe ya mkono, mashine za kukoboa na kupuchukua na kusaga mahindi na nafaka nyingine.

Mcharo anasema kwa sasa wamejikita kwenye uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za msingi zikiwa powertiller na nguzo za zege kwa ajili ya kusambazia umeme.

Uunganishaji wa matrekta hayo madogo ya kukokota, anasema wameupa kipaumbele kutokana na mahitaji yaliyopo nchini hususan Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambako shughuli za kilimo zimetamalaki.

“Uwezo wetu ni kuunganisha kati ya matrekta 20 hadi 25 kwa msimu. Kwa siku tunaweza kuunganisha matrekta matano. Huwa tunaunga kulingana na mahitaji ya wakulima, lakini tunao uwezo wa kutengeneza hata matrekta 10 kwa siku,” anasema Mcharo.

Anasema kasi ya maombi bado ni ndogo kutokana na ushindani uliopo kutoka kwa wafanyabiashara wanaoagiza kutoka nje.

Changamoto nyingine anasema bado wakulima wengi hawafahamu namna ya kuyatumia matrekta hayo jambo linalowazimu kuwafuata mashambani kwao na kuwafundisha.

“Wapo wanaosema matrekta hayafanyi kazi vizuri kumbe tatizo ni kutojua namna ya kuyaendesha,” anasema meneja huyo.

Matoroli na mashine

Kulingana na teknolojia wanayotumia kutengeneza matoroli na mashine za aina tofauti zinampa mteja nafasi ya kuchagua au kuelekeza ukubwa na uwezo autakao.

“Hivi vyote tunatengeneza kwa oda maalumu baada ya mteja kutuambia anataka tumtengenezee zana yenye ukubwa na muundo utakaompendeza,” anasema Mcharo. Mbali na mradi wa matrekta madogo na zana nyingine, kiwanda hicho pia kinatengeneza mabati hivyo kupunguza ulazima wa kuagiza kutoka nje.

Mcharo anasema kwa siku wanaweza kutengeneza mabati 1,000 kutegemea ukubwa wa soko.

“Tunaamini tukimuwezesha mkulima kuboresha maisha yake, umasikini utapungua. Akiwa na zana bora kilimo kitaimarika na akijenga nyumba nzuri atajenga kwa bati zetu nafuu,” anasema.

Nguzo za zege

Uzalishaji wa nguzo za zege za kusambazia umeme ni mradi mpya wa kiwanda hicho na unaelezwa kuwa ndio uliobeba roho ya uwekezaji mzima kwa kuwa umegharimu Sh4 bilioni.

Tayari nguzo hizo zimethibitishwa na Shirika la Viwango (TBS) na kiwanda hicho kinaweza kutengeneza kati ya nguzo 40 hadi 50 kwa siku zenye urefu wa mita 10 mpaka 12. Kila nguzo ina uzito wa kilo 600 na inaweza kudumu kwa miaka 55.

Soko kuu la nguzo hizi ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) hivyo mafanikio ya uwekezaji wa kiwanda hicho yanategemea sana mipango ya shirika hilo.

“Tunaamini katika kutunza mazingira. Nguzo za zege zitumike kusambazia umeme badala ya kuendelea kukata miti,” anasema.

Malighafi zinazotumika kutengeneza nguzo hizo, anasema ni za ndani jambo linalochangia kukuza uchumi na kuongeza ajira hasa kwa vijana.

Tanesco wanasemaje?

Meneja wa Tanesco mkoani Mbeya, Bahati Benedict anasema nguzo za zege zitalisaidia shirika hilo kukabiliana na kukatika ovyo kwa umeme ambao mara nyingi husababishwa na kuoza kisha kudondoka kwa nguzo.

“Hizi ni nguzo za kudumu, haziozi tofauti na za miti ambazo tunahitaji kuzibadili mara kwa mara na mpango wa shirika kwa sasa ni kuhamia kwenye nguzo za zege. Japo kwa mtazamo awali gharama zake zitakuwa juu lakini zitapunguza zile za matengenezo,” anasema.

Changamoto zilizopo

Mcharo anasema uzalishaji unaendelea vizuri na hawajapata usumbufu wowote wa kukatika kwa umeme wala maji na pindi inapojitokeza hali hiyo huwasiliana na mamlaka husika na kurekebisha tatizo husika kwa wakati.

Pamoja na kuanza uzalishaji wa matrekta madogo na nguzo za umeme, kiwanda hicho kinakabiliwa na changamoto kadhaa za uendeshaji.

Kama ilivyo kwa wawekezaji wengine, utitiri na mfumo wa kodi pamoja na sheria zinazokinzana ni miongoni mwa changamoto ziliozopo.

Mcharo anasema changamoto wanayokumbana nayo kwa sasa ni mfumo wa kodi wanazotozwa kwa kuwa zinawaumiza hivyo kuishauri Serikali kuziangalia upya hasa kwa wawekezaji wazawa.

“Suala la kodi na mfumo mzima wa ukusanyaji wake ni tatizo kubwa kwetu, mamlaka zinazohusika ziangaliwe upya kwa kuziweka pamoja,” anashauri.

Anatoa mfano tozo na kodi zinazokusanywa na Osha, TBS, Zimamoto na TRA kwamba kila moja hujitokeza kwa wakati wake jambo linalowafanya watendaji kutumia muda mwingi kuwasikiliza maofisa wa Serikali.

Licha ya hayo, Mcharo anasema mwekezaji anatakiwa kuzingatia sheria nyingi zilizopo kwa mfano za mazingira, afya, vipimo na ukaguzi kabla hajapata vibali vya kuanza uzalishaji.

Meneja huyo anaiomba Serikali kukilinda kiwanda hicho na vingine vyote kote nchini kwa kuwawekea mazingira rafiki ili uwekezaji wao ulinufaishe taifa.

Anasema ipo haja ya kusisitiza matumizi ya bidhaa za ndani kwa Serikali kulinda viwanda vilivyopo na wananchi wawe na imani ili kujenga uchumi imara badala ya kukimbilia bidhaa za nje.

Suala la ajira

Meneja huyo anasema kwa sasa kiwanda hicho kijana watumishi wasiozidi 50 na wote ni Watanzania huku akibainisha kwamba ajira zitaongezeka kadri uzalishaji utakavyoimarika.

“Hatutegemei kuajiri watu kutoka nje kwani nchini wapo wenye uwezo mkubwa kufanya shughuli hizi kwa ufanisi mkubwa endapo tutawatumia ipasavyo badala ya kuweka imani na watu wa nje,” anabainisha