Tahasusi mpya zinavyoibua wasiwasi, matumaini elimu ya Tanzania

Tahasusi ni kundi la masomo anayochagua mwanafunzi pindi anapoanza ngazi mpya ya elimu.

Humwezesha kusoma masomo mbalimbali kwa wakati mmoja na kupanua maarifa. Awali sekta ya elimu nchini ilikuwa na tahasusi 16 ambazo zimedumu kwa miongo zaidi ya sita.

Hata hivyo, hivi karibuni sekta ya elimu imeshuhudia mabadiliko makubwa kwa Serikali kuamua kuongeza tahasusi nyingine 49 na hivyo kuwa na jumla ya tahasusi 65.

Mchengerwa: Tumejipanga utekelezaji wa tahasusi mpya

Tahasusi hizo zimo kwenye makundi saba ambayo ni sayansi ya jamii, sanaa, lugha, biashara, sayansi, michezo na elimu ya dini

Wadau wa elimu wanasema tahasusi mpya zinaendana na sera mpya ya elimu na mitalaa ambayo ilianza kutumika Januari mwaka huu. Kuongezwa kwa tahasusi mpya kuna maana kuwa sasa wanafunzi wanaojiunga na kidato cha tano, watakuwa na wigo mpana wa kuchagua masomo ya kwenda nayo vyuo vikuu.

Wengi wamepokea kwa mikono miwili uamuzi wa Serikali kuanzisha tahasusi hizi, huku baadhi wakitilia shaka kasi ya maamuzi hayo ambapo bado Taasisi ya Elimu nchini (TET), haijaweka bayana mbinu na mchakato wa upatikanaji wa vitabu vya kutekeleza uamuzi huu.

 Vilevile wachambuzi wa elimu wanahoji juu ya ukimya wa kamishna wa elimu katika kufafanua dhana ya tahasusi mpya, kwani ndiye mbobezi na mtekelezaji wa sera za elimu kwa kushirikiana na waziri husika.

Kufuatia sintofahamu hiyo, hivi karibuni Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamedi Mchengera alinukuliwa na gazeti hili akisema, Serikali imejipanga ipasavyo kutekeleza azma ya tahasusi mpya 49, huku akisisitiza kuwa maamuzi ya utaratibu huu yalifanyika baada ya kukusanya maoni mbalimbali kutoka kwa wadau wa elimu.

Kwa mujibu wa Waziri, Serikali imekwisha tenga fedha za kutekeleza mpango huu ambapo Benki ya Dunia imenuia kusaidia Tanzania katika kufanikisha mpango wa kuboresha elimu nchini ili kuleta ufanisi katika ufundishaji wa tahasusi hizi mpya.


Matumaini

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa makala haya, wadau wa elimu walionesha matumaini kwamba Serikali imetoa jibu kwa kilio cha umma, kilichotaka wanafunzi kutobanwa kwenye tahasusi za kwenda nazo kidato cha tano na sita pamoja na vyuo vya ufundi.

Ofisa mtendaji mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Elimu, Benjamin Nkonya alisema tahasusi mpya zinalenga kuzalisha kizazi kinachoweza kuajiriwa.

"Hii ni utekelezaji wa mtalaa mpya unaolenga elimu kwa ajili ya ajira... nguvu ya kutafuta vyanzo vipya vya fursa za kiuchumi," anasema Nkonya.

Anasema kuongezeka kwa tahasusi za lugha, kutakuza uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na mataifa mengine na kuwaandaa wanafunzi kuuzika katika soko la ajira kimataifa.

Kwa mujibu wa Nkonya, tahasusi mpya zinazohusisha lugha za kimataifa zitawasaidia Watanzania ambao wanataka kufanya biashara, hasa kwa kusafiri kwenda nchi nyingine kama China, Ufaransa na Falme za Kiarabu (UAE) kuwasiliana bila kikwazo.

Aliongeza: "Aina hii ya mtalaa ni mwarobaini wa wasiwasi mkubwa katika mfumo wa elimu kwani unawaandaa wanafunzi kuingia kwenye soko na kutumia fursa zilizopo nchini ambazo kwa sasa zinachukuliwa na wageni."

Kwa upande wake, mwalimu mstaafu Gozbert Muganyizi anasema tahasusi mpya zitasaidia kuwaandaa wanafunzi kuwa wataalamu tangu shuleni.

"Tahasusi mpya zitasaidia wanafunzi kunoa ujuzi katika taaluma zao kwa sababu wakifikia hatua ya kujiunga na vyuo vikuu, watakuwa wameiva kikamilifu katika masomo wanayotarajia kusomea," amasema Muganyizi.

Afisa mtendaji mkuu wa jukwaa la kujifunza mtandaoni, Smart Darasa, Elias Elisante alinukuliwa akisema uamuzi wa kuongeza tahasusi mpya 49, umekuja wakati sahihi ili kupanua wigo wa maarifa ya wanafunzi katika ujifunzaji, hasa katika maeneo ambayo yanachochea ubunifu.

Elisante anasema tahasusi kama fizikia, hisabati na sayansi ya kompyuta (PMCs) itawaandaa wataalamu wa teknolojia kwa siku za usoni kuwa na weledi katika msingi ya akili bandia (AI), ambayo kwa sasa inapigiwa chapuo kote duniani.


Wasiwasi uliopo

Pamoja na hisia chanya juu ya tahasusi mpya, wadau wengine wa elimu wameonesha wasiwasi juu ya uwezekano wa kutekeleza azma hii adhimu, hasa kipindi hiki ambacho Serikali bado ina kibaru kigumu cha kutekeleza malengo ya mtalaa mpya.

Wadau wengine walienda mbali zaidi na kudhani kwenye tahasusi zinazohusisha masomo ya dini, huenda Serikali imejipa jukumu la kuandaa masheikh, maimamu, wachungaji na mapadri, suala ambalo wanahisi ni la hiari na ilibidi Serikali ingeliacha mikononi mwa taasisi husika.

Mwandishi nguli na mwanaharakati wa masuala ya elimu, Richard Mabala, alinukuliwa kwenye makala iliyochapishwa kwenye gazeti mtandao la The Chanzo, akisema ana wasiwasi na uamuzi na Serikali kuanzisha jambo nyeti kama kama hili kwa haraka pasipo mikakati madhubuti ya utekelezaji, jambo amabalo anadhani linaweza kuathiri ubora wa elimu nchini.

“Kwa mfano, Tanzania si nchi pekee yenye masomo ya dini kama somo la shule ya sekondari, na je, tunawezaje kuwa na uhakika kwamba itakuwa ni mojawapo ya mchanganyiko unaotumika sana?” alihoji Mabala.

Aliongeza: “Tunaweza kujadili umuhimu wa masomo kama hayo lakini hatujui ni shule ngapi zitafundisha masomo ya kidini kama vile theolojia au masomo ya Kiislamu, labda ni shule za kidini au madrasa tu.”

Mabala anasema Serikali inaweza kudhani ina jukumu la kutafuta mustakabali na fusra za wanafunzi pasipo kuwashirikisha kwa kigezo cha mtazamo wa kitamaduni, kwamba ni wadogo sana kiasi cha kutoweza kufahamu ni nini kizuri kwao, lakini ni sharti tujiulize ni kwa nini wanafunzi hawa huchukua maamuzi kwa vitendo.

‘’Kwa nini wengi hawaoni umuhimu wa kwenda shuleni? Kwa nini wanachagua vyuo vya ufundi badala ya shule za sekondari? Ukisikiliza utagundua wana sababu nzuri tu kama ambavyo wangepaswa kushirikishwa kabla ya kuwaanzishia tahasusi mpya, ’anabainisha.


Angalizo

Katika shule za sekondari za chini, kumekuwa na jaribio la kutambua vipaji tofauti, ndoto za watoto na mbinu za kukuza vipaji vyao.

Nachelea kusema ni mapema mno kung’amua namna ambavyo tahasusi hizi mpya zinaweza kufundishwa pasipo kuathiri ufanisi kwenye suala zima la ujifunzaji.

Hivyo ingekuwa sahihi kutumia mwaka huu kutafakari njia sahihi za kutekeleza ufanisi wa ufundishaji kwa kutumia tahasusi hizi mpya, ndio maana wengi wa wadau wanapenda kujua kama walimu wamejiandaa.

Na swali lingine linalogonga vichwa ni je, kuna kozi katika vyuo vyetu vya ualimu na vyuo vikuu vinavyowatayarisha walimu wa tahasusi hizi mpya?

Ni sharti ifahamike pia kwamba walimu wote wanaopaswa kutekeleza azma ya tahasusi hizi 49 ni lazima wawe wahitimu.

Na hapa siyo tu nina maana ya maudhui ya masomo husika bali ni sharti mbinu zinazohitajika kufundisha tahasusi hizi mpya kwa ufanisi zizingatiwe.

Sasa tujiulize je, vyuo vikuu hutoa kiasi gani cha umakini kwa mbinu za ufundishaji na stadi za maisha?

Zaidi ya hayo, je, vitabu vimeandikwa? Je, vinasheheni mada za masuala mtambuka yanayoshika kasi kila uchao? Au bado tunatembea wakati ulimwengu unakimbia?

Maswali haya yalimuibua Mabala na kuhoji kama ni sahihi kwa taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kuendelea kuhodhi jukumu la uandishi wa vitabu vya masomo.

Hapo awali ilikuwa Taasisi ya Maendeleo ya Mitaala. Hilo, peke yake lilikuwa jukumu kubwa: kuandaa na kuboresha mitalaa pamoja na kuhakikisha vitabu vilivyotungwa na wachapishaji vinaendana na mtalaa husika.

Wakati huo huo, kuruhusu watunzi wengine kufikiria na kuchapisha vitabu vya kiada na ziada, kulijenga ubunifu na wigo wa maarifa kwa wanafunzi wa Kitanzania.

Je, kwa kuipa TET mamlaka ya kuhodhi utunzi wa vitabu kumeongeza ubunifu kiasi gani? Na tunawezaje kutarajia TET itengeneze vitabu vyote vinavyohitajika kwenye mtalaa wenye tahasusi mpya kwa ghafla?

Historia inaonesha kuwa nchini Rwanda, wanafunzi walipitia changamoto kubwa katika uchaguzi wa masomo walivyoanzisha tahasusi mpya.

Hii ilitokana na mageuzi katika mfumo wa elimu ambayo yalifanyika tangu mwaka wa 2008, ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya lugha ya kufundishia kutoka Kifaransa kwenda Kiingereza kwa taasisi zote za elimu.

 Pamoja na hayo, elimu ya msingi iliongezwa kutoka miaka sita hadi tisa. Hivyo tahasusi mpya zinaweza kuathiri sana maisha ya wanafunzi kwa baadaye.

Hata hivyo, kutokana na idadi kubwa ya tahasusi, wanafunzi wanajikuta katika wakati mgumu kufanya uamuzi sahihi.

Miongoni mwa tahasusi hizi ni pamoja na sayansi, sanaa na lugha, na jumla ya masomo 17 hufundishwa vidato vya juu.

Changamoto hizi za uchaguzi wa masomo zinaonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.

Utafiti uliofanya na Dk Mary Boumrind nchini Marekani unaonesha kuwa baadhi ya wanafunzi huchagua masomo kulingana na dhana potofu za mishahara na ugumu wa masomo, badala ya kuzingatia uwezo wao kibinafsi.

Wataalamu wanashauri kwamba sera za elimu zinapaswa kuzingatia zaidi mahitaji ya wanafunzi na uwezo wao binafsi badala ya kufuata tu muundo uliowekwa.

Hii ni muhimu sana katika kuhakikisha kwamba wanafunzi wanakuza stadi na vipaji katika masomo yao na wanaweza kufunya kazi zinazowavutia.

Wakati Serikali inafanya jitihada za kuboresha elimu kwa kuanzisha tahasusi mpya 49 ni muhimu kuzingatia upya njia za kusaidia wanafunzi katika uchaguzi wa masomo.

Hii itasaidia kuhakikisha kuwa vijana wanajiandaa vizuri kwa ajira na maisha ya baadaye pasipo kuingiza siasa.