Mpenzi wako ana hasira? Fanya haya…

Picha ikimuonesha mwanamke mwenye hasira. Picha na tovuti ya goodguys2greatmen

Dar es Salaam. Katika mahusiano ya aina yoyote, hakuna anayeweza kusema hajawahi kukasirika. Mara kwa mara tunakwazana na kukasirishana, ingawa wako wale ambao hasira yao iko karibu zaidi na huja kwa ukali zaidi na mara nyingine huleta madhara katika vitu, watu au hisia za mpenzi mwingine.

Hapa nataka nikusaidie jinsi ambavyo unaweza kufanya pale mpenzi wako anapowaka hasira kali. Kujua hili kutakusaidia kupoza au kuponya hasira za mwenzako na sio kuchochea moto mkubwa zaidi.


Nini cha kufanya?

Ikubali hasira ya mwenzako kama ndiyo nia yake ya kuonyesha hisia zake.

Hasira yake na kulipuka kwake kwaweza kuwa kunaudhi na wala hakuna sababu ya msingi, lakini kubali kuwa ana hali ya kuwa na hasira. Hasira yake yaweza isiwe nzuri kwako, lakini kumbuka haiashirii mwisho wa mahusiano yenu. Mahusiano yaliyo bora huruhusu kwa kiasi fulani mikikimikiki kama hii, huwezi kupinga kwa asilimia mia moja hali kama hizi zisiwepo.


Mfanye mpenzi wako kuwajibika kwa hasira yake mwenyewe

Najua anaweza kukulaumu wewe kwa hasira zake, kataa kukubali wazo hilo, wewe hauhusiki kwa chochote, wala wewe siyo sababu ya hasira hizo bila kujali yeye anasema nini. Yeye ndiye amechagua kukasirika na kufanya hivyo anavyofanya, na mara nyingi ni mbinu yake kukufanya ukubaliane na matakwa yake. Kataa kuchezewa kupitia hasira yake.


Tulia, na uwe na sababu ya kutulia kwako

Hata kama mpenzi wako kavuka mipaka kwa kukutukana, kukulaani, kukupayukia au hata kukupiga, bado waweza kuchagua kuwa mpole na ukiwa na sababu maalumu ya kutulia kwako. Taratibu na kwa upole mtulize kwa kumwonyesha uhalisia wa tukio. Kwa busara na kujizuia kwa hali ya juu, jitahidi kumweleza mawazo yako, hisia zako na ukionyesha jinsi hali hiyo inavyokusumbua mara inapotokea, kamwe usitumie sentensi za “wewe”, mfano “wewe unaudhi sana”, “wewe sikuelewi kabisa”, bali tumia sentensi za “mimi”, mfano “mimi ninaumia sana unapofikia hali hii”. Endelea kutoa mawazo yako kwa ufasaha na hali ya kumjali.


Weka mipaka kwa hasira zisizo na sababu ya msingi

Kama mwenzako anazidi kuonyesha hasira yake isiyo na msingi, anatukana na kuendelea kubwatuka, na hakusikilizi unachotaka kukisema, basi unaweza kuamua kutoka kuwa pembeni ya eneo hilo, kwa upole mwambie kuwa utafurahi kuzungumzia jambo hilo mara atakapopoa ukali na baada ya hapo nenda chumba kingine mpaka atulie.

Jizuie usiombe msamaha au kumtaka radhi, najua wengi, hususan wanawake waliofikia hatua hii, hujiona wao ndio wakosaji na hivyo kukimbilia kuomba radhi. Kumbuka mpenzi mkorofi, na mtukanaji hastahili kuombwa radhi. Ndiyo yawezekana wewe ni sababu kwa kiasi fulani kwa tatizo hilo, lakini kwa kule kukasirika kwa staili hiyo haumfanyi astahili kuombwa radhi, maana kwa kufanya hivyo utaendeleza tabia yake hiyo mbaya. Msamaha au radhi yaweza ikafaa baadaye kidogo wakati mpenzi wako ametulia na ameiweza hasira yake. Jaribu kuihifadhi samahani yako mpaka wakati huu ufike.

Mpongeze mpenzi wako mara tu anapoamua kufanya lile lenye staha na siyo anapoonesha hasira.

Wakati wowote mpenzi wako anapoonesha kushuka na kujielewa kuwa analofanya sio jema, mpongeze, mtie moyo kuendelea na tabia hiyo njema kwa kumwonyesha utayari wa kumsikiliza kile anachotaka kusema ili mfikie maafikiano.


Jipongeze pia

Kamwe usiruhusu matukano, kejeli na kashfa za mpenzi wako zikuvunje moyo na kukushusha thamani yako. Usijione mnyonge kwa lawama zake, labda tu uchague kukubali anachokisema kwako.

Jione bado kuwa wewe ni mwema na ulikuwa unafanya mambo kwa nia njema. Ukiweza jipongeze kwa kufanya kile ambacho hisia zako zitaona zimepongezwa. Mfano, jitoe mtoko, nenda kwenye filamu, jipikie kitu kizuri, fanya nafsi yako ijisikie iko juu.

Kama unajiona kuwa huwezi au unapata shida kuzifuata njia hizi basi jitahidi kumtafuta mshauri wa kisaikolojia kwa msaada zaidi.