Ndoa yako ina changamoto? Fanya haya kuijenga

Kabla sijaenda mbali na kukuruhusu wewe msomaji kuzama ndani ya makala hii nadhani ni vema niliweke hili wazi kwamba njia hizi ninazozizungumzia sio ndiyo misingi ya ndoa. Misingi ya ndoa ni makala au somo lingine pia nililonalo ingawa labda kuna maeneo utaona kuna kufanana.

Njia hizi ni baadhi ya zile ambazo wengi walishauriwa kuzitumia na zikawasaidia na kwahiyo labda na wewe zinaweza kukusaidia kama wao. Hizi ni njia ambazo ni rahisi kuzielewa ingawa maranyingine zinaonekana ngumu kuzitendea kazi. Pamoja na hayo yote bado njia hizi zimeonekana kuwa msaada kwa wengi.


Epuka maneno yakejei, chunga kinywa

Kejeli ni maneno kama maneno mengine, tofauti ni kwamba haya ni maneno yenye nia ya dhati ila iliyofichwa yenye kusudi la kumshushia hadhi anayeambiwa. Unaweza usijue namna atakavyoyapokea maneno hayo yule anayeambiwa lakini mara ukishayatoa tu yanaweza kuleta madhara moyoni au kwenye hisia za yule aliyeambiwa, hususani pale anapofikiria kuhusu nia au dhumuni la msemaji wa kejeli hizo. Fahamu kuwa mara nyingine maumivu ya ndani yanapoongezeka yanakuja kusababisha milipiko ya magomvi na majuto ya baadae.

Jifunzeni kuyakagua maneno yenu mara kwa mara, waza au fikiri kabla haujasema hilo neno au hayo maneno kwa mwenza wako. Maranyingine maneno yana ncha kali kuliko mkuki na yanaweza kuleta madhara makubwa.


Mwoneshe mwenza wako kiwango cha juu cha tabia njema

Mara nyingine inashangaza unakuta mwanandoa yuko tayari sana kumwonyesha mchungaji wake au kiongozi wake wa dini nidhamu ya hali ya juu kuliko anavyo mwonyesha mwenza wake. Mtu anakuwa mwema kwa marafiki, ndugu na watu baki lakini sio kwa mwenza wake. Inakuwa vipi watu wengine wakusifie kwamba unajua kujali au kusaidia wakati mke wako au mume wako hilo halioni? Jitahidi kuongeza kiwango cha utu wema na kwakufanya hivyo utaongeza kiwango cha hali ya urafiki na furaha kwenye ndoa yako. Acha habari za ukali usio na mashiko, hasira zisizo na tija au kususa kusiko sababu. Jenga badala ya kubomoa.

Heshima au nidhamu ni msingi mmojawapo wa tabia njema unayoweza kuionyesha kwa mwenza wako. Kwa kufanya hivi unazuia hali zote za hofu, hisia mbaya na hata maumivu ya ndani.


Jifunze kuzungumza lugha ya mapenzi kwa mwenza wako

Fahamu kwamba mke au mume wako ana lugha yake moja ambayo ni maalumu kwa yeye kuonyesha au kuwasiliana kimapenzi. Lugha hii inakuwa mojawapo kati ya zile lugha tano ambazo labda unazifahamu au umewahi kuzisikia. 1. Matendo ya kusaidia 2. Maneno ya kupongeza au kusifia. 3. Muda wa faragha. 4. Zawadi 5. Mguso au kugusana .

 Mara nyingi lugha ya penzi ya mwenza wako sio yakwako, kwahiyo kuna umuhimu mkubwa sana wa kujifunza na kujitahidi kwa kufanya mazoezi ili kumudu kuongea na hata kusikiliza lugha yake. Hapa naweka mkazo zaidi kwamba sio tu kuongea lugha yake bali hata kuweza kuisikiliza. Kwa kuongea lugha ya mwenzako unamgusa hisia zake na hivyo kuamsha penzi baina yenu. Kama ungependa kuzifahamu zaidi lugha hizi unaweza kutafuta kitabu cha mwandishi Gary Chapman.


 Usijifanye unafahamu mawazo ya mwenza wako

Maranyingi ni rahisi kudhania ya kwamba unayajua mawazo ya mume au mke wako, labda kwasababu unafuatilia anavyofanya au kusema mara kwa mara na hivyo kila akifanya kitu unatoa hitimisho kwamba nia yake ilikuwa hii au ile na wakati wote unamhesabia kuwa amefanya kitu hicho kwa nia mbaya. Ni kweli kwamba mara nyingi mawazo yetu yana kuwa hasi zaidi juu ya yale wanayofanya wenza wetu kuliko kuwa chanya. Hii imesababisha hata mwitikio wetu kuwa hasi maana hata tafsiri tuliyokuwa nayo ni hasi. Wewe huwezi kuyafahamu mawazo ya mwenza wako na kwahiyo usijifanye unajua. Mungu peke yake ndiye azichunguzaye nafsi na moyo na kuyajua yaaliyondani. Hakuna mwanadamu kwenye uwezo huu.

Ziko njia mbali mbali za kushuhulikia tabia tusizozipenda, hususani kwa kuwaonyesha wenza wetu namna tunavyotamani vitu vifanyike na mara nyingine kwa sisi kuonyesha mfano lakini sio kuwa wakali kwao na tukitoa hukumu kwao huku tukijipa uhakika kwamba wamefanya walichofanya kwa makusudi. Tabia ya kukimbilia kumuwazia mabaya mwenza wako ni mbaya na ya hatari maana inamwaga sumu kwenye mahusiano yenu, na kuna uwezekano ikaja kukugharimu sana huko mbeleni, lakini kama utabadilika na kujenga tabia ya kumuwazia mema na hata anaporudia kufanya kitu kisicho kizuri ukaangalia kwamba sio makusudi utakuwa umejikusanyia nguvu za kumpenda zaidi mwenzako na kuyafurahia mahusiano yenu. Jaribu kufanya majaribio ya tabia hii kwa siku 30 na hautarudi tena ulikokuwa.


 Jifunze kuiombea ndoa yenu

Nafahamu kabisa kuwa unaimani yako inayopewa msukumo na dini yako lakini kwa vyovyote vile maana yangu ni kwamba hata kama mwanaume na mwanamke wanaweza kuishi pamoja na siku zikasonga bado umuhimu wa ninyi wawili kuiombea ndoa yenu unabaki pale pale. Sisemi kwamba kama msipofanya hivyo ndoa itavunjika siku inayofuata, la hasha, lakini wale ambao wamekuwa wakiziombea ndoa zao wamekiri kuishi kwa furaha na misuguano michache sana kuliko wale ambao hawafanyi hivyo. Kuiombea ndoa sio kuwaombea watoto ingawa watoto ni sehemu ya ndoa yenu. Unapoombea familia unawaombea na watoto ndani yake. Kuiombea ndoa kunayahusu mahusiano yako na mume au mke wako. Ziko nyakati utaomba kawaida na ziko nyakati utajikuta unalazimika kufunga ili kuomba kwa kina zaidi. Ndoa zetu hupitia nyakati ngumu sana mara nyingine na kwa hivyo msaada wa Mungu ni lazima.

Itaendelea wiki ijayo