Ni kweli dalili hizi kwa mjamzito zinatafsiri jinsia ya mtoto?

Mama yangu mzazi aliwahi kuniambia kuwa hakuwahi kuijua jinsia yangu kwa muda wote wa ujauzito hadi siku niliyozaliwa. Nina imani mama yangu ni mmoja wa wanawake walio wengi, na kama sio karibu wanawake wote ambao kwa muda wote wa uja uzito huwa hawajui jinsia za watoto wao hadi siku ya kujifungua.

Hii haijawahi kuwa ajabu na hasa kwa miaka ya nyuma ambayo sayansi na teknolojia ilikua bado ni ya kiwango cha chini, lakini habari njema ni kwamba sasa hivi wanawake tunaweza kuwafanyia vipimo na kugundua jinsia za watoto wao wangali bado wakiwa tumboni ikiwa wanahitaji iwe hivyo. Japo pia huduma hizi hazijafanikiwa kuwafikia wanawake wote na hasa wale waishio vivijini kutokana na uhaba wa vifaa vya radiolojia kama vile mashine za “ultrasound” ambazo ndizo zinazotumika kuona jinsia ya mtoto akiwa tumboni.

Lakini pia bado nimeona kuna baadhi ya wanawake huchagua kutojua jinsia ya mtoto hadi siku atakayojifungua kwa dhana ya kwamba, jinsia ya mtoto ni “surprise” kutoka kwa Mungu mwenyewe. Lakini pamoja haya yote, kama inavyofahamika, tangu siku ya kwanza mwanamke anapojigundua kuwa ni mjamzito hadi siku ya mwisho anapojifungua, mwanamke hupitia safari ya miezi tisa iliyochanganyikana na mabadiliko mengi sana.

Mabadiliko haya huja kwa sura tofauti na kugusa mifumo karibu yote kwenye mwili wa mwanadamu, na hasa, kisaikolojia, kwenye mfumo wa chakula, mfumo wa vichocheo, na mfumo wa uzazi wa uzazi wenyewe kutokana na maendeleo ya ukuaji wa mtoto akiwa tumboni.

Mabadiliko haya mbalimbali yanapotokea, husababisha pia dalili mbalimbali zinazojionesha mwilini na kupitia dalili hizi, wanawake wenyewe huzitumia kama ni ishara za kutafsiri jinsia ya mtoto kama ni wa kike au wa kiume kulingana na dalili husika ambayo mjamzito mwenyewe huipitia.

Na inasemekana kwa miaka iliyopita zimekuwa dhahiri na hata sasa baadhi ya wanawake wanazisadiki na kukiri kuwa ni kweli dalili hizi zinatafsiri jinsia ya mtoto.

Lakini je, hii imekaaje kisayansi?

Dalili ya kwanza ni uchovu mkali wakati wa asubuhi au “morning sickness” kwa kitaalamu. Wajawazito zaidi ya 6 kati ya 10 hupitia tatizo la uchovu mkali asubuhi baada ya kuamka hasa kwa miezi mitatu ya kwanza. Wanawake wengi wanasadiki kuwa hali hii mara nyingi inaashiria kuwa mtoto atakayezaliwa ni wa kike. Kisayansi ipo hivi, mwanamke mwenye ujauzito wa mtoto wa kike anakuwa na kiwango kikubwa cha vichocheo na kusababisha uchovu kuwa mkubwa, lakini mwanamke mwenye uja uzito wa mtoto wa kiume wanabeba kiwango kidogo cha homoni au vichocheo na hivyo kumfanya awe na uchovu wa kawaida hasa wakati wa asubuhi.

Dalili nyingine kubwa ni mihemko ya hisia. Kuna baadhi ya wajawazito wanakuwa na tabia za kubadilika badilika. Wanakuwa wepesi kubadilika na kukasirika bila sababu ya msingi. Watu wengi hudhani kuwa wajawazito wa namna hii watazaa watoto wa kiume na wale ambao wanakuwa sio wa kubadilika badilika watazaa watoto wa kike. Lakini ukweli ni kwamba wajawazito wote hupitia hali ya mabadiliko ya mihemko hasa muhula wa kwanza, na wa tatu wa ujauzito. Na pia kubadilika kwa mihemko kunachangiwa na mambo kadha wa kadha kama vile msongo wa mawazo, vichocheo, na sababu zingine za kisaiokolojia hivyo dalili hii haina uhusiano na jinsia ya mtoto.