Ukiwasahau utotoni ujue uzeeni hawatakukumbuka

Nimekutana na Qambebeda Morogoro. Qambebeda ni rafiki yangu tangu utotoni. Hatujaonana naye tangu tumemaliza darasa la saba. Kwa hakika tunayo mengi ya kukumbusha na kuzungumza. Kubwa ni hekima ambazo naziona kwa Qambebeda. Utu uzima unakuja na busara nyingi za maisha.

Anasema “Kuna umri ukifika maisha hudai vingi.” Ninatafakari ana maana gani. Anaendelea, “Maisha yamebana sana siku hizi. Tunakimbizana na majukumu saa nyingine inakuwa vigumu sana kuwa wazazi.”

Qambebeda ananifanya nijitafakari. Kasema ukweli mchungu. Nawaza vipaumbele vyangu katika maisha. Ni kweli ninapata muda wa kuwa na familia? Je, visingizio vyovyote ninavyovitumia vinaisaidiaje familia yangu?’ Wakati nikitafakari, Qambebeda ananisimulia jambo linalonishangaza kidogo:

“Mzee wangu analalamika kwamba siwasiliani naye. Namwelewa. Inaweza kupita hata mwezi mzima sikumbuki kuulizia hali yake. Kwa umri wake kusubiri kupata habari zake kupitia kwa mke wangu si sawa.” Namfahamu Qambebeda kama mcha Mungu anayejali sana watu. Hili la kumtelekeza mzazi wake limekaaje?

“Hata sijui. Lakini ni kama sina kabisa habari naye. Hata tukionana huwa sina mambo mengi ya kuzungumza naye. Tunasalimiana ndio inakuwa basi. Juzi hapa nilimleta hapa kwangu apate matibabu. Nimetumia fedha nyingi kumtibia. Lakini huwezi amini, aliporudi Karatu, ni kama ufahamu wangu umemfukia.”

Mke wake Qambebeda, mwanamke mwema, mchangamfu na muongeaji, anaingilia kati kidogo kueleza namna anavyosaidia kurejesha mawasiliano kati ya mumewe na baba yake: “Mara zote mimi ndio huwa nakukumbusha kumpigia mzee.

Nilikuwa najiuliza kwa nini huna mawasiliano na baba yako.” “Lakini unaelewa sio kwamba simpendi…” anajitetea Qambebeda na sote tunaangua kicheko cha kumtia moyo.

Ushunuzi unatambua uhusiano mkubwa kati ya malezi na tabia zetu ukubwani. Namuuliza Qambebeda uhusiano wake na baba yake ulikuwaje.

“Baba yangu alikuwa mkali sana. Alikuwa faru. Sikumbuki ni wakati gani nikiwa mdogo niliwahi kufurahia uwepo wake.”

Kwa mbali machozi yanamlengalenga huku akisema; “Kuna siku nakumbuka tunatembea kwenda kanisani. Darasa la nne au tano kama sijasahau. Baba yuko mbele anapiga hatua kubwa za kiutu uzima na mimi na utoto wangu ule nalazimika kumkimbilia na simfikii. Natamani anisubiri anishike mkono niende naye sambamba.

Baba wala hajali kuna mtoto anamfuata kwa nyuma.” Wote tunacheka kwa masikitiko. Tunaponyokwa na pole isiyotarajiwa, “Inatia huruma jamani!” Qambebeda anatuonesha namna mtoto kimaumbile anavyotamani kuwa karibu na mzazi wake.

Ufahamu wa mtoto unatafsiri kujali kama kitendo cha mzazi kupunguza mwendo na kumshika mkono. Masikini baba yake hakuelewa.

Anatusimulia desturi ya wa-Iraq. Baba na mama, kwa kawaida walilala nyumba tofauti kwenye boma lile lile. Baba, kwa kawaida, alilala na wanaye wa kiume.

“Tulikuwa tunalala na baba kitanda kimoja. Kwetu mie nilikuwa mdogo zaidi. Kitu kilichokuwa kinaniuma enzi hizo ni saa za kulala zimefika natamani tukalale na baba na baba hata hana habari.

Niliishia kwenda zangu kulala kinyonge nikiwa very disappointed. Kuna namna nilijisikia kiumbe wa ziada kwenye ratiba za baba.” Utoto wa Qambebeda ulijaa upweke. Moyo wake ulisukwa sukwa na njaa isiyoshibishwa. Hamu ya kuwa karibu na baba haikuwahi kutimizwa.

Tunachojifunza hapa kuna umri ukiwa na nguvu, mzazi unawaona watoto si watu wa maana. Wakikusogelea unawaona kama wasumbufu. Hukumbuki kuwekeza kwenye uhusiano na watoto.

mwingi unautumia na watu wengine. Maisha, wahenga walisema, ni mzunguko. Unapanda ulichovuna. Uliyemtekeleza utotoni, utamhitaji uzeeni. Unamnyanyasa mzazi mwenzako na watoto wanaona na hawasemi. Majibu utayapata uzeeni.