Wazazi wakigombana, mtoto anaathirika hivi...

Muktasari:

  • Machi 16, 2024 lilitokea tukio la kusikitisha wilayani Babati mkoani Manyara pale mtoto wa miaka minane kukatisha maisha yake kwa madai ya kuchoshwa na migogoro baina ya wazazi wake.

Machi 16, 2024 lilitokea tukio la kusikitisha wilayani Babati mkoani Manyara pale mtoto wa miaka minane kukatisha maisha yake kwa madai ya kuchoshwa na migogoro baina ya wazazi wake.

Kwa mujibu wa majirani, mtoto huyo alikuwa akishuhudia mara kwa mara mama yake akipigwa kila unapotokea ugomvi na mwenza wake na huenda hali hiyo ikamsukuma achukua uamuzi huo mgumu.

Taarifa ya Jeshi la Polisi ikathibiisha kutokea kwa tukio hilo la mtoto Rafia Adam kujinyonga kwa kutumia mkanda wa gauni la mama yake akisema chanzo ni wazazi wake kugombana hali iliyosababisha mama yake kuondoka nyumbani.

"Mtoto huyo ni mwanafunzi wa shule ya msingi Maisaka alikuwa anasoma darasa la pili na aliamua kujinyonga baada ya kuona wazazi wake wanagombana mara kwa mara wakiwa nyumbani na siku ya tukio hilo wazazi wake walikuwa wamegombana na mama yake mzazi aliomdoka nyumbani na kwenda kwa wazazi wake siku nne zilizopita.

 "Baada ya kutokea hali hiyo ndipo akachukua uamuzi wa kujinyonga kwa mkanda wa mama yake kwenye mti wa mstafeli uliopo mbele ya nyumba yao," alieleza kamanda wa polisi Mkoa wa Manyara George Katabazi.

Usemi wa majuto ni mjukuu unadhihirika kwa baba wa mtoto huyo Adam Ally anayeeleza kamwe hakutegemea migogoro kati yake na mwenza wake ingekuwa na athari kubwa kwa mtoto wake.

 "Ni kweli tulikuwa tumegombana na mama yake ambaye aliondoka nyumbani na kuelekea nyumbani kwao ila sikutegemea kama atachukua uamuzi huo wa kikatili wa kujizuru nafsi yake,".

Kilichotokea kwa mtoto huyu huenda kinaweza kutokea kwa watoto wengine kwa kile kinachoelezwa kisaikolojia kwamba mara nyingi akili ya mtoto haiko tayari kuona wazazi wake wakiwa katika migogoro na hali inayowaondolea furaha.

Baadhi ya wanasaikolojia waliozungumza na gazeti hili wameeleza kuwa tukio hilo lililotokea mkoani Manyara ni kengele kwa wazazi waone ni kwa kiasi gani migogoro yao inaweza kuwa na athari kubwa kwa watoto.

Katika kipindi hiki ambacho takwimu za ndoa zinazovunjika zinazidi kupanda, wanasaikolojia hao wametoa wito kwa wazazi kuwa makini katika kuhakikisha migogoro yao haiachi athari kwenye akili na maisha ya watoto.

Mwanasaikolojia Saldeen Kimangale anasema ni rahisi mno kwa mtoto au watoto kuathirika kisaikolojia kunapokuwa na migogoro ya mara kwa mara ya wazazi.

Anasema inapotokea mtoto anashuhudia migogoro ya aina hiyo kila wakati anaishia kuwa na msongo wa mawazo na kwa kuwa uwezo wake wa kutatua kukabiliana na changamoto ni duni anaweza kuchukuwa hatua mbaya ikiwemo hiyo ya kujitoa uhai.

Kimangale anasema watoto wengine wanaokumbana na hali hiyo hufikia uamuzi wa kutoroka nyumbani ili tu asishuhudie yale yanayoiumiza akili, hisia na mwili wake.

Si hivyo tu, mwanasaikolojia huyu anabainisha kuwa mtoto anayepitia changamoto hii anaweza kujiingiza kwenye matendo ya hatari ikiwamo kujidhuru na kutumia dawa za kulevya ili kujizima asiendelee kupata mateso yatokanayo na kumbukizi ya kile kinachoendelea kwa wazazi wake.

“Wazazi ni nguzo kwa mtoto, kwa maana furaha, amani, usalama, utulivu wa moyo na akili na silika nyinginezo za mtoto zinawategemea wazazi. Mtoto akikwazika popote kimbilio ni mzazi wake, tena mzazi wake wa kumzaa sio wa kufikia wala kumuasili.

“Sasa inapotokea ile nguzo ikawaka ndiyo yenye kupeleka kitisho kwa mtoto kwa kweli mtoto anakuwa katika hali mbaya kiakili na kisaikolojia.

Mara nyingi wazazi hasa wa kike wanapopisha na wazazi wenzao hutishia kuondoka, na kuwaacha”anasema na kuongeza

“Wapo pia ambao huwashirikisha watoto wao masaibu yao kwa njia ya kulia na kuapiza mfano baba yenu anataka kuniua, au bora nife, n.k hali hii huzalisha homoni za kupambana na msongo au mkazo (cortisol na adrenalini) kwa kiwango cha juu sana kwa mtoto, kiwango hiki cha homoni kikizidi huharibu mfumo wa mtoto kurekebisha hisia zake”.

Kimangale anashauri ni muhimu kwa wazazi kuacha ubinafsi na kufikiri kuhusu watoto kabla ya kuruhusu uhusiano wao kutawaliwa na migogoro isiyoisha.

Anasema, “Wazazi tuwajibike kuwalinda watoto, ikiwa wameshindwana watafute namna bora ya kuachana bila kumdhuru mtoto.”

Mwanasaikolojia Jacob Kilimba anasema migogoro ya wazazi ina athari za moja kwa moja kwa watoto kwa sababu imaji ya kwanza ya mtoto ipo kwa mzazi au mlezi wake kwa kuwa ndiye mtu wa kwanza aliyemuona au kukutana naye katika maisha yake yake.

“Mtoto anamchukulia mzazi kama Mungu wake hapa duniani. Ujasiri na hali ya kujiamini aliyonayo mtoto inaanzia kwa aina ya mzazi aliyemlea. Hii imani inakuja kupungua baadaye akishafikia umri wa balehe hivyo kabla ya hapo hakuna mtu mwingine anaweza kumuamini zaidi ya mzazi.

“Kunapokuwa na migogoro ya wazazi mtoto anaathirika kwa kiasi kikubwa. Kitendo cha kuona mzazi wake mmoja analia, mwingine anafoka au anaondoka anaanza kuona kuna tatizo. Sasa inamuwekea kwenye mkanganyiko na mara nyingi wazazi wanapogombana kila mmoja anamlaumu mwenzake hapo ndipo mtoto anaposhindwa kumuelewa amuamini nani,” anasema na kuongeza.

“Wapo wazazi wengine ambao wanakwenda mbali zaidi unakuta anamwambia mtoto kwamba baba yako mbaya au mama yako mbaya hii inampa wakati mgumu mno mtoto na inamuondolea ile imani aliyonayo kwa wazazi wake.”

Mwanasaikolojia huyo anafafanua kuwa mtoto akianza kupoteza imani kwa wazazi au mzazi wake anaanza kujiona hana thamani hivyo anatafuta njia ya kujitenga na hilo linaweza kumsukuma kufanya maamuzi magumu ikiwemo kutoroka nyumbani, kujidhuru au hata kujiua.

Akizungumzia hilo mtaalam wa malezi Jesca Nagwa anasema wakati mwingine mtoto anaweza kukimbia nyumbani au kuchukua uamuzi mwingine mgumu ili asiwe katika nafasi ya kuchagua upande baina ya wazazi wake.

Anataja athari nyingine ni kutengeneza aina ya watu ambao huenda wakajiweka mbali na uhusiano unaolenga kujenga familia kwa kuhofia kupitia ambacho wazazi wake wamepitia.

“Mara nyingi watoto huwatazama wazazi wao kama mfano katika maisha yao ya usoni, utakuta mtoto wa kike kadiri anavyozidi kukua na kufikia muda wa kupata mwenza atatamani kumpata mtu kama baba yake. Kinyume chake ni kwamba baba akiwa anafanya vitu vya ajabu, mtoto anaweza kuogopa wanaume wote akiamini watakuwa kama baba yake.

“Tunaweza kupata watu wanaogopa kuingia kwenye ndoa kutokana na historia za wazazi wao. Hili lipo, kuna watu wanahofia kuwa na uhusiano, wapo wengine wanaoishi kwenye uhusiano wenye changamoto,” anasema.

Mbali na hayo, Jesca anasema; “Migogoro ya wazazi inaweza kuathiri malezi kwa watoto, wengine hawawezi kuhimili hasira zao hivyo anaweza kuzishushia kwa mtoto akamtolea maneno makali na inawezekana akajikita zaidi kwenye kushughulikia mgogoro na akasahau kuhusu jukumu la malezi.

Pia, mtoto anaweza kupata msongo wa mawazo, ugonjwa wa sonona au wasiwasi kupitiliza muda wote akiwa na hofu ya kutokea ugomvi ambao huenda ukamsababisha mzazi wake mmoja kuondoka nyumbani na yeye kuingia matatizoni.”


Anayopitia mtoto kulingana na umri

Kwa mujibu wa mwanasaikolojia wa Uingereza Dan Macdonald mtoto wa kuanzia mwaka sifuri hadi miaka miwili anaweza asipate madhara ya kihisia anaposhuhudia wazazi wake wakigombana au kutengana isipokuwa anaweza kujiona yupo kwenye hatari endapo atakuwa anashuhudia ugomvi na malumbano ya mara kwa mara.

Mtoto mwenye miaka miwili hadi mitano anaanza kuelewa kwamba kuna kitu hakipo sawa na bahati mbaya watoto wenye umri huu wanapoona wazazi wao wakigombana au kutengana huhisi anahusika kwenye ugomvi huo na kama mmoja ataondoka basi itakuwa ni kwa lengo la kumuacha yeye.

Mtoto wa miaka mitano hadi minane uelewa wake unazidi kupanuka, anaanza kuelewa kila kinachoendelea hivyo inawezekana akawa anapitia wakati mgumu kuyakubali yanayoendelea kwa wazazi wake.

Bahati mbaya katika umri huu, tayari anaaza kuwa na marafiki anaowaamini nje ya wazazi wake na ni watu anaozungumza nao kila mara.

Umri wa kati ya miaka 8 hadi 12 ni mgumu mno kwa watoto. Ukaribu wake kwa marafiki unaongezeka maradufu na anaanza kupunguza utegemezi kwa wazazi.

Katika kipindi hiki mtoto huelewa vitu vingi na anapata taarifa nyingi kutoka kwa wenzake, hivyo upo uwezekano mkubwa kujihisi kuwa ndiye chanzo cha ugomvi au unaotokea kwa wazazi wake.

Licha ya kwamba uelewa wao wa mambo unazidi kupanuka huwa ni vigumu kwa watoto wenye umri kati ya miaka 12 hadi 18 kutojihusisha na migogoro ya wazazi wao. Wengi huishia kuathirika kisaikolojia kwa sababu huwa wanajaribu kujifanya hawaelewi kinachoendelea endapo hawajashirikishwa lakini ndani ya nafsi zao wanapitia maumivu makali. Mambo huwa magumu zaidi kwao inapofikia hatua ya wazazi kutengana.