Kanumba Day yafufua matumaini ya filamu Bongo

Mama mzazi wa marehemu Steven Kanumba akizungumza jambo wakati wa kumbukumbu ya miaka miwili tangu kufariki mwigizaji huyo mahiri.

Muktasari:

Mwanzoni mwa wiki hii wadau wa filamu walifanya tamasha maalumu la kumkumbuka mwigizaji huyo ambapo ni miaka miwili tangu kitokee kifo chake. Hafla hiyo ilifanyika katika Ukumbi wa Dar Live Jijini Dar es Salaam.

Kila ifikapo Aprili saba, wapenzi na msahabiki kama siyo Watanzania kwa jumla huadhimisha kifo cha mwigizaji mahiri, Steven Charles Kanumba, kwa kufanya mambo mbalimbali.

Mwanzoni mwa wiki hii wadau wa filamu walifanya tamasha maalumu la kumkumbuka mwigizaji huyo ambapo ni miaka miwili tangu kitokee kifo chake. Hafla hiyo ilifanyika katika Ukumbi wa Dar Live Jijini Dar es Salaam.

Mwaka huu tamasha hilo la kumkumbuka lilikuwa tofauti kidogo, kwani kilifanyika kitendo cha kihistoria ambapo pamoja na burudani, kulifanyika uzinduzi wa mfuko wa Steven Kanumba uitwao ‘Kanumba The Great Foundation’.

Hali ilivyokuwa

Kama ilivyo ada ya wadau wa burudani hadi kufikia saa tatu usiku ukumbi ulikuwa umejaa, lakini kwa bahati mbaya umeme ulikuwa tatizo na tatizo liliongezeka zaidi pale jenereta kubwa la ukumbini hapo kuharibika.

Mashabiki walilazimika kusubiri umeme urudi kwa takriban kwa saa tano bila mafanikio hadi waandaaji wa tamasha hilo walipolazimika kukodi jenereta la kuendeshea shughuli hiyo, lakini hilo halikuwafanya mashabiki waliokuwa nje ya ukumbi huo kuacha kumiminika kuja kushuhudia nini kinafanyika katika kumbukumbu ya mpendwa wao Kanumba.

Uvumilivu umefika kikomo

Hadi saa sita kamili usiku shughuli hiyo ilikuwa haijaanza na kulikuwa na giza totoro, kutokana na kutokuwapo kwa njia mbadala. Mashabiki pamoja na kuwa watulivu kwa takriban saa tano wakisubiri kinachoendelea, walianza kufanya fujo, ikiwamo kubeba viti na kutoka navyo nje kufidia kiingilo chao na kuvunja chupa tukio ambalo lilidhibitiwa kwa busara____ na hatimaye saa saba jenereta la kukodi likawasili ukumbini na saa saba na dakika 18, kile kilichokuwa kikisubiriwa kikaanza.

Burudani za kukata na shoka

Mionngoni mwa wanamuziki walioshiriki katika usiku huo na kupagawisha mashabiki ambao kiasi walikuwa wamekata tamaa ni Snura Mushi ambaye kama kawaida aliwapagawisha kwa minyonga yake.

Mbali na Snura pia alikuwapo mwanamuziki kutoka kundi la Tip Top Connection, Khalid Ramadhan ‘Tundaman’. Alifanya mambo yake kwa ustadi mkubwa na kuwafanya mashabiki kusahau shida na kuburudika pamoja. Kundi zima la Jahazi Modern Taarab, hawakuwa nyuma katika kuonyesha na wao wameguswa katika kumbukumbu ya mwigizaji huyo kwa kutoa burudani kamili.

Mkali wa rhythm Afande Sele, aliwainua mashabiki vijana katika ukumbi huo ilipofika saa tisa usiku, baada ya kuchana mistari makini na bendi ya Twanga Pepeta ilifanya mambo yake na kuhitimisha burudani kwa usiku huo.

“Tumesota sana, lakini angalau tumeburudika, lakini natoa angalizo wakati mwingine mambo kama haya yanaweza kuleta vurugu na watu kupoteza maisha yao, kwa kuwa tumedhulumiwa. Mtu analipa sh 10,000 halafu anapata burudani kwa saa tatu badala ya usiku kucha,” alisikika shabiki mmoja akilaumu kitendo cha kukatika kwa umeme na kuharibika kwa jenereta, kitendo kilichosababisha sherehe hizo kuanza saa saba na kumalizika saa 11 alfajiri.

Tukio muhimu lafanyika

Katika hali iliyoashiria nguvu ya Kanumba kuwa bado ipo, ni kitendo cha viongozi wa vyama viwili cha Bongo Movie Unity na Shirikisho la Filamu Tanzania ‘TAFF’, kuungana usiku huo na kufanya kitu kimoja tu, kumuenzi Kanumba.

Tofauti na ilivyozoeleka, pamoja na wasanii kupanda jukwaani na kucheza sebene kwa zamu, waigizaji walikuwa kimya na utulivu ulitawala usiku huo.

“Jamani hawa watu si maadui, kila mmoja anamshutumu mwenzake. Lakini leo wapo pamoja wanatuzuga nini?” walisikika vijana wawili walioketi nyuma ya mwandishi wa makala haya. Simon Mwakifambwa, ambaye ni rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), alizindua rasmi mfuko wa kusaidia watu wasiojiweza, watoto yatima na jamii kwa jumla, ujulikanao ‘Kanumba The Great Foundation’ ilipofika saa nane na dakika 47.

“Nazindua rasmi mfuko huu kwa niaba ya Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, ambaye kabla ya kupata majukumu ya kikazi na kaniteua kumwakilisha aliahidi kuchangia kiasi cha sh1 milioni,” alisema Mwakifambwa baada ya kuzindua mfuko huo.

Pamoja na uzinduzi wa mfuko huo pia kulikuwa na kazi. Vitu mbalimbali alivyokuwa akitumia mwigizaji huyo kama vile gitaa, viatu ambavyo alivinunua Italia na inasemekana hadi sasa hakuna Mtanzania ambaye anavyo, na filamu 15, ambazo aliwahi kuigiza.

“Mimi nimeipenda ile picha Kanumba aliyopiga akiwa na Rais Jakaya Kikwete. Picha ile inaonyesha ni kwa jinsi gani hata Serikali ilimtambua Kanumba kuwa ni nani, ukiachilia hizi wanazopiga wakialikwa kula. Kanumba alipiga picha na rais baada ya kufanya mazungumzo muhimu ambayo pengine yangelipeleka mbali soko letu la filamu nchini. Mara nyingi huwa nadhani ipo siku nitakutana na kijana huyu njiani,” alisikika mama wa makamo aliyejitambulisha kwa jina la Magdalena Richard, huku akiangalia picha hiyo kwenye meza iliyokuwa na vitu vya kumbukumbu za mwigizaji huyo.

Mratibu wa shughuli hiyo, George Wakuganda, aliiambia Starehe kuwa, hakutarajia kama kungekuwa na hitilafu katika jenereta kubwa la ukumbi huo na ndiyo maana hakukuwa na haja ya kutafuta jenereta ya ziada.

“Jenereta ya hapa ni kubwa, ‘huku akimwonyesha mwandishi wa makala haya jenereta kubwa la ukumbini hapo’. Hivyo hatukuwa na wasiwasi na tulihakikishiwa itapona baada ya muda mfupi. Punde lilipogundulika kuwa na tatizo saa zilipozidi kwenda, ndipo tukalazimika kutafuta la kukodi jambo ambalo halikuwa rahisi alisema Wakuganda.