Maisha ya umaarufu ni mafupi mno

Muktasari:

  • Nathubutu kusema maisha ya umaarufu kwa asilimia 80 ya wasanii wengi nchini hayazidi miaka mitano. Wachache wamebahatika kudumu kama Profesa J, Sugu, AY, Jay Dee na FA.

Kuna wasanii sasa hivi akiandikwa inabidi atambulishwe kwa kukumbushia kazi zake alizowahi kufanya. Kwa wale wa kizazi cha zamani kidogo wanaweza kumtambua ila kwa wasomaji wa kizazi kipya watamwona chipukizi.

Sanaa imepitia mengi nchini na kuna wasanii waliwahi kuwa chipukizi, wakawa mastaa halafu wakarudi tena kuwa chipukizi.

Wapo wanapotaka kutoka wanawapigia magoti waandishi, baada ya miaka miwili wanawadharau, miaka mitano baadaye wanaanza kulazimisha waandishi waandike au watangaze habari zao. Wakiambiwa haziandikiki wanadai wanabaniwa au kutuhumu kuuliwa vipaji vyao.

Nathubutu kusema maisha ya umaarufu kwa asilimia 80 ya wasanii wengi nchini hayazidi miaka mitano. Wachache wamebahatika kudumu kama Profesa J, Sugu, AY, Jay Dee na FA.

Kwa maana hii wasanii wanakabiliwa na changamoto za kiuchumi hasa baada ya umaarufu wao kushuka.

Wengi huanza kupata fedha katika umri mdogo na umaarufu hudumu kwa kipindi kifupi.

Kipindi cha umaarufu wake ndiyo huwa cha kupata fedha. Mialiko ya matamasha, mikataba ya matangazo na dili nyingine huja wakati huu, lakini umaarufu unapopungua na mirija yote ya fedha hukata na hapa ndipo yanapoanza matatizo ambayo tumeshuhudia yakiwasukuma wasanii kujiingiza katika vitendo visivyofaa na kuwatafuta wa kuwapa lawama.

Utafiti uliofanywa miaka mitatu iliyopita na Taasisi ya Marekani ya National Bureau of Economic Statistic inasema, msanii wa Afrika anaweza kuingiza mpaka Sh4 bilioni katika kipindi cha miaka mitano ya mafanikio yake.

Swali linabaki je, msanii huyu anazifanyia nini fedha hizi wakati zinaingia au anaishia kuzitapanya akiamini kuwa kesho zitakuja nyingine?

Niwakumbushe tu kujituma katika kipindi hiki cha miaka mitano ya umaarufu kwa kuwekeza na pia angalau kuhakikisha baada ya muda huo jina halishuki moja kwa moja.