MAONI: Kwa nini wanafunzi waendelee kutembea umbali mrefu

Picha na Juma Mtanda

Muktasari:

Maswali yanayokuja ni mengi; je kulikuwa na ulazima upi kwa mwanafunzi huyo kuandikishwa shule ya mbali? Je, hakuna shule ambayo iko karibu na maeneo anayoishi? Je, hakuna uwezekano wa kuhamia shule iliyo karibu?

Inasikitisha kuona bado wanafunzi katika maeneo mengi nchini wakitembea umbali mrefu kutoka nyumbani hadi shuleni

Maswali yanayokuja ni mengi; je kulikuwa na ulazima upi kwa mwanafunzi huyo kuandikishwa shule ya mbali? Je, hakuna shule ambayo iko karibu na maeneo anayoishi? Je, hakuna uwezekano wa kuhamia shule iliyo karibu?

Ninatambua kuwa hapo zamani wanafunzi wengi walilazimika kutembea umbali mrefu kuzifuata shule ambazo zilikuwa ni chache. Hivyo ili mtoto apate elimu ilimbidi atembee umbali mrefu kuifikia shule. Lakini watoto wengi siku hizi hawana uwezo wala ulazima wa kutembea umbali unaozidi kilomita nane kwa siku kutokana na mazingira na hali ya sasa.

Jambo la ajabu ni kuwa hata maeneo ya mijini pia tatizo la umbali bado lipo. Baadhi ya wanafunzi, hulazimika kuamka na kuanza safari alfajiri na mapema ili kutafuta usafiri.

Kwa mfano, jijini Dar es Salaam wapo watoto wanaokaa Kimara lakini wanasoma shule za katikati ya jiji. Hii imewafanya wengi kusumbuka kutafuta daladala, na mara nyingi wamekuwa wakionekana vituoni nyakati za jioni; wakati mwingine hata usiku; wakihangaika kutafuta usafiri wa kuwarudisha nyumbani. Kwa upande wa sekondari, Serikali ilianzisha shule za kata ili kusogeza huduma ya elimu karibu na wananchi na kupunguza umbali kwa wanafunzi kuzifikia.

Lakini hali imekuwa tofauti, bado wanafunzi wanatembea umbali mrefu kwenda na kurudi kutoka shule. Kwa mfano, kwa mujibu wa gazeti moja la kila siku la Aprili 8, huko mkoani Singida, wanafunzi wanaotoka kijiji cha Mnoro wilayani Mkalama, hulazimika kutembea umbali wa jumla ya kilomita 20 kwenda shule ya sekondari Kinyagiri na kurudi nyumbani.

Umbali huu si wa kuupuuzia hata kidogo; mwanafunzi anafika shuleni akiwa amechoka, anasikia njaa, anakosa usikivu kutokana na kuchoka. Pengine angehitaji kupumzika kwanza na si kuingia darasani moja kwa moja ili kupokea mafundisho.

Je, shule hizi zina utaratibu wa kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi? Mwanafunzi mwenye njaa na anayetembea umbali mrefu bila kupata lishe nzuri, afya yake huzorota na huwa mlegevu. Hivyo, hawezi kushiriki vizuri kimasomo darasani.

Athari za shule kuwa mbali na maeneo wanayoishi wanafunzi ni pamoja na utoro kutokana na adhabu wanazopata pindi wakichelewa kufika shuleni. Masomo huanza saa mbili kamili asubuhi, je mwanafunzi anayetembea kilomita 10 kwenda shule anapaswa kuanza safari saa ngapi ili awahi shuleni?

Wazazi kama kiungo muhimu kwa maendeleo ya wanafunzi hawana budi kufuatilia mahudhurio ya watoto wao shuleni. Na pengine kwa kutambua umbali ambao mwanafunzi anatembea, ni vizuri kila mzazi ajaribu kutambua ni njia zipi ambazo mwanawe huwa anatumia kumfikisha shuleni bila kuchelewa.

Wanafunzi wa sekondari sehemu nyingine imebidi kuwaomba wazazi wao wawapangie vyumba ili waishi karibu na shule. Lakini kutokana na kuwa na uhuru wa kuishi wenyewe bila usimamizi, wanafunzi wengi huharibikiwa na kuishia kufanya yale yasiyopendeza katika jamii kama vile uvutaji wa bangi, sigara, ulevi, na kujiingiza katika mapenzi katika umri mdogo.

Jambo la muhimu zaidi ni kwa Serikali, wazazi jamii kwa jumla kuchukua hatua za kujenga shule karibu ili kuwawezesha watoto wao kusoma karibu na maeneo wanayoishi.

Mfano mzuri ni ule ulioonyeshwa na Manispaa ya Ilala iliyotoa eneo la ekari 25 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi mtaa wa Lubakaya, kata ya Zingiziwa kule Chanika. Hii ilikuwa ni baada ya eneo hilo kukosa shule ya msingi kwa kipindi kirefu jambo lililosababishia wanafunzi wa mtaa huo kutembea umbali mrefu kufuata shule.

Ili kupunguza tatizo hili, ni vyema wadau wa elimu kwa pamoja wakaangalia uwezekano wa kujenga hosteli kwa ajili ya wanafunzi, hasa wanaotoka mbali. Hii itasaidia kuwapa muda mzuri wanafunzi kujifunza na kutafakari kwa utulivu yale waliyojifunza.

Pia itapunguza tatizo la mimba kwa wanafunzi wa kike, ambao wamekuwa wakishawishiwa kuingia kwenye mapenzi na madereva wa malori, mabasi na pikipiki wanaowapa lifti ili wawahi kufika shule kutokana na umbali wake.

Pia, wizara inayosimamia elimu pamoja na wazazi wahakikishe wanafunzi wanaandikishwa, kupangwa au kuchaguliwa kusoma katika shule zilizo karibu na maeneo wanayoishi.

Iwapo umbali anaotembea mwanafunzi utapungua, utampa muda mzuri wa kupitia masomo aliyojifunza siku hiyo na hata kusaidia shughuli ndogondogo nyumbani.

Naomi Mwakilembe ni Ofisa programu, Idara ya ushiriki na uwajibikaji wa jamii, HakiElimu. [email protected]