Baraza la Wazee CCM launga mkono kazi za JPM

Rais John  Magufuli

Muktasari:

  • Wazee hao wanaunga mkono juhudi za Rais Magufuli katika kupambana na wahujumu uchumi na kuwashangaa watu wenye macho lakini wanajifanya hawaoni na wanataka kumkwamisha Rais.

Sumbawanga. Baraza  la  Wazee wa CCM  Mkoa  wa  Katavi limetoa  tamko la kumuunga  mkono Rais John  Magufuli  katika  jitihada  zake za  kupambana  na  watu wanaohujumu   rasilimali za  nchi  na  kulaani vikali  mauwaji yanayotokea Kibiti na Mkuranga mkoani Pwani.

Tamko hilo limetolewa mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali Mstaafu  Raphael Muhuga katika kikao cha Baraza la Wazee wa CCM Mkoa wa Katavi kilichofanyika katika Ukumbi wa Maji   mjini  humo.

Akisoma  tamko  hilo leo, Jumapili, Julai 9, Mwenyekiti wa Baraza  la   Wazee wa  CCM Katavi,  Thomas Ngozi amesema baraza hilo linamuunga mkono Rais Magufuli katika jitihada kubwa anazofanya kupambana na wahujumu wa rasilimali za nchi.

Amesema wamekaa na kuona nchi inavyokwenda hivyo wameona wamtie moyo Rais kutokana na kazi ngumu anayoifanya ya kuiongoza nchi.

Mwenyekiti  huyo alieleza  kuwa wanatambua upendo alionao Rais Magufuli kwa Watanzania na hasa kwa kuwajali wale walio masikini bila kuwabagua kutokana na umasikini wa watu hao.

Amesema wapo  baadhi ya Watanzania wachache wenye macho  lakini wamekuwa wakijifanya hawaoni na wamekuwa  wakitaka  kukwamisha jitihada zinazofanywa na Serikali ya  awamu ya  tano.

Alieleza  kuwa kama  ni  wizi ulivuka mipaka na Serikali  imekuwa  ikiibiwa kwa kipindi  kirefu hivyo Rais ameamua kupambana na wizi huo hivyo ni vyema jitihada hizo anazozifanya zikaungwa mkono na watu wote bila kujali itikadi za vyama.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali Mstaafu   Muhuga alisema Serikali ya mkoa huo inaunga mkono jitihada  kubwa katika vita ya wahujumu wa uchumi wa nchi.

Amesema vita hii inahitaji Rais aungwe mkono    kwani si watu wote ambao wanaifurahia licha  ya kwamba kwa kipindi hiki kifupi mabadiliko yameanza kuonekana .