Mabadiliko ya Katiba yanapaswa kuhojiwa

Wiki iliyopita tuliishia pale Mchungaji Christopher Mtikila aliposhinda kesi ya mgombea binafsi na Serikali kukata rufaa ikashindwa, hoja za Serikali zilishindwa kwa hoja kama ifuatavyo.

Uamuzi wa Mahakama ya Rufaa Tanzania ulisomwa na Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufaa, Ferdinand Wambali, kwa niaba ya jopo la majaji watatu, ambao ni John Mroso, Edward Rutakangwa na Engela Kileo.

Mwaka 1993, mbele ya Jaji Khawa Lugakingira (sasa marehemu), Mchungaji Mtikila alishinda kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma. Hata hivyo, Bunge lilishindwa kutunga sheria ya kuruhusu mgombea binafsi katika chaguzi zilizofuata.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliwasilisha rufaa iliyopewa namba 20/2007 akiomba Mahakama ya Rufaa itupilie mbali uamuzi wa Mahakama Kuu wa kuruhusu mgombea binafsi kwa kuwa umeonekana kuwa na dosari za kisheria.

Serikali ikafanya mabadiliko ya Katiba kwa hati ya dharura ikabadili Katiba na kuchomekea kiubatili, shurti la mgombea kudhaminiwa na chama cha siasa, Mchungaji Mtikila akafungua kesi nyingine Namba 10 ya mwaka 2009 kupinga marekebisho hayo ya 8 ya Katiba na kuyaita ni ubatili.

Kwa ajili ya kulinda heshima ya Mhimili Mahakama na mimi kwa vile ni wakili hivyo ni pia ni ofisa wa Mahakama, ili nisije kuonekana ni mtovu wa nidhamu, kwa kuivunjia heshima Mahakama, naomba kukuwekea sehemu ndogo tuu ya hukumu yenyewe:

“Ili kuruhusu matakwa ya watu kutawala kama wagombea hao [huru] wanafaa au la”.

“Tuna uhakika kwamba Mahakama sio wasimamizi wa matakwa ya watu. Hiyo ni mali ya Wabunge wa kuchaguliwa”. Hapa Mahakama ya Rufaa, haikuwatendea haki kabisa Watanzania.

Katiba ndiyo “the will of the people”, yaani matakwa ya wananchi, Katiba imekiukwa Serikali kupeleka bungeni muswada wenye kipengele batili kinachokwenda kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT) na Bunge likaitunga sheria hiyo batili, rais akaisaini kuidhinisha ianze kutumika, Mahakama Kuu ikaibatilisha kuwa ni batili.

Serikali ikapeleka bungeni mabadiliko ya Katiba kwa hati ya dharura kuuchomekea ubatili ule ndani ya Katiba yetu, Bunge likauchomeka, Mahakama Kuu ikatoa hukumu ya pili kuwa huo ni ubatili na mabadiliko hayo ni batili, Mahakama ya Rufaa, ikaurudisha ubatili huo kwa mhimili wa Bunge kuuondoa. Huku sio kuwatendea haki Watanzania.

Kwenye suala la ukiukwaji wa Katiba, Mahahakama ya Rufaa, ilipaswa iiheshimu hukumu ya Mahakama Kuu, kwa sababu hukumu hiyo, imezingatia uvunjwaji wa Katiba ya JMT, uliofanywa na Bunge la JMT. Uamuzi wa Mahakama ya Rufaa, umezingatia uwezo wa Mahakama Kuu, kuliamuru Bunge kuuondoa ubatili uliochomekewa ndani ya Katiba kiubatili.

Kwa lugha ya kisheria, kitu kikishaamriwa ni batili, kitu hicho kinakuwa hakipo toka amri inapotolewa. Kwa vile hakuna ubishi kuwa kifungu hicho ni batili, wala hakuna ubishi kuwa Katiba yetu imebadilishwa kiubatili, kwa kuchomekewa kipengele batili, Mahakama ya Rufaa, ilipaswa kwanza kujikita kwenye kuzungumzia ubatili jambo ambalo ndilo kubwa la msingi na sio kuangalia uwezo wa Mahakama Kuu, kuliamuru Bunge kuuondoa huo ubatili.

Swali linalobakia hadi leo ni, licha ya kuwepo ubatili kwenye Katiba yetu na sheria zetu, Mahakama Kuu ikaamuru uondolewe, Mahakama ya Rufaa ikalimuru Bunge liuondoe, kwanini ubatili huu mpaka leo bado umo ndani ya Katiba yetu na sheria zetu?

Toka Mahakama Kuu ilipotoa uamuzi wa ubatili huo, ubatili huo unakuwa umebatilishika pale pale, hivyo serikali haikupaswa kukata rufaa, lakini serikali yetu ilikata rufaa na wakati huohuo serikali ilipeleka bungeni kwa hati ya dharura, sheria Namba 34 ya mwaka 1994, kufanya marekebisho ya 8 ya Katiba ya JMT na kukichomeka kipengele hicho mgombea kudhaminiwa na chama cha siasa, ndani ya katiba, hivyo kuibatilisha ile hukumu ya Jaji Lugakingira. Hapa ndipo ubatili wa kuinajisi Katiba yetu ulipoanzia serikali yetu kuchomekea ubatili ndani ya Katiba yetu kiubatili.

Kwa vile hukumu za Mahakama ya Rufaa ndio hukumu za mwisho (final and conclusive), hukumu za Mahakama za Rufaa, lazima ziwe ni hukumu ambazo kitaalamu wanaita SMART (Specific, Measurable, Achievable, Relevant, and Time-bound).

Kitendo cha hukumu hii kutotekelezwa mpaka leo, maana yake hukumu hii sio relevant ndio maana imepuuzwa na Mahakama imekaa kimya.